June 6, 2016



Na Saleh Ally
KIKOSI cha Taifa Stars kimemaliza kazi. Sasa hakitashiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika nchini Gabon wala michuano ya Kombe la Dunia, hii ni baada ya kufungwa mabao 2-0, juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Stars imefungwa mabao 2-0 na Misri ambao walisafiri kutoka Cairo wakiwa wanataka sare yoyote lakini mwisho wakabeba pointi tatu na kujihakikishia kwa pointi 10 lakini Stars ina pointi moja tu ikiwa mkiani.

Gumzo kubwa mtaani baada ya kutolewa kwa Stars ni mshambuliaji nyota na nahodha mpya, Mbwana Samatta kukosa penalti. Lakini hilo si gumzo namba moja kama lile la Haji Mwinyi Mgwali.

Gumzo kubwa kwa mashabiki ni Mwinyi kufungisha. Wanaamini mabao yote mawili yametokea kwake na straika Mohamed Salah, anayekipiga AS Roma ya Italia, akaimaliza Stars kwa kufunga mabao yote mawili.

Bao la kwanza, Mwinyi aliruka kufanya ‘takolin’, akaugusa mpira lakini akamwangusha mtu wakati akizuia asipige.  Ikawa faulo na Salah akafunga.

Bao la pili, Misri wakafanya ‘one two’, walipoingia kwenye eneo la hatari, Mwinyi akashindwa kumdhibiti Salah akionekana amezidiwa nguvu.

Achana na kwamba alicheza na watu wanaojua sana, ukweli ni kwamba, Mwinyi alicheza mechi hiyo akiwa anatetemeka kuanzia mwanzo. Hakuwa katika kile kiwango chake na muda mwingi alionekana kutoa pasi fyongo huku akiua ‘muvu’ za Stars kutokana na kutokuwa makini.

Mara nyingi alionekana kupoteza uhakika wa kuirukia mipira ya kuokoa, hasa ile ya kulala chini. Krosi zake zilikuwa dhaifu kabisa na hakika hakuwa msaada.

Mjadala wake umekuwa mkubwa sana na huenda ukamuathiri kisaikolojia kwa kuwa nimemuona si mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuvumilia kashkash za mashabiki. Ndiyo maana nikaamua kuzungumza naye hapa hadharani.


Tukubali Mwinyi hakucheza vizuri mechi hiyo na kweli alikuwa sehemu la tatizo lakini hakuna ubishi timu yetu yote haikucheza vizuri na hatuwezi kumlaumu yeye pekee wala Samatta.

Huenda Kocha Charles Boniface Mkwasa alipaswa kuwa mwepesi kujua dakika 45 za kwanza hazikuwa nzuri kwa Mwinyi, alipaswa kutorejea tena lakini akamrudisha, hii ilimuathiri zaidi.

Kweli hakuwa amecheza mechi nyingi za ushindani lakini Mwinyi anapaswa kutulia na kucheza mpira hasa. Anapaswa kujiamini na kuachana na uoga usio na sababu.

Lakini lazima akubali kwanza kweli hakuwa vizuri na alikuwa tatizo. Aangalie ambayo anaamini kweli yanamhusu na arekebishe badala ya kubishana na ukweli au kumalizwa na yale ambayo anaamini hakufanya.

Akitaka kushindana na ukweli, amekwisha. Akikatishwa tamaa na maneno pia atakuwa amejimaliza kabisa. Umri unamruhusu na tumeona kuwa amecheza mechi nyingi za kimataifa na kuisaidia Yanga kufanya vema.

Hakuwa amecheza muda mrefu, mwalimu sijui kwa nini hakuliona hilo. Lakini huu ni wakati mzuri wa tathmini kwake kwamba alipokosea, njia sahihi ni ipi kupajenga. Lakini anapoona anasingiziwa, njia nzuri ni kupuuzia na kuamini kwenye kujenga badala ya kulazimisha kupambana.

Kuna tuhuma anazopewa, kama ni kweli basi lazima azirekebishe mapema. Kama ni za uongo yeye atakuwa anajua moyoni mwake, anapaswa kuzipuuzia kwa nguvu ili arejee katika kupambana.

Kwa wengine, nafikiri lazima tuamini Mwinyi bado ni mgeni katika soka la kimataifa, amecheza mechi chache sana hasa timu ya taifa. Hivyo tusikubali ‘kumuua’ kisoka kwa makosa ya mechi moja na tukasahau mazuri yake ya mechi nyingi kabisa.

Kumjadili kishabiki kwa kuwa Mkwasa aliacha kumuingiza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, haitakuwa na tija hata kidogo. Badala yake tuangalie utaifa zaidi na tujali kile ambacho kinaweza kumsaidia Mwinyi na kuendeleza kipaji chake na si kummaliza kabisa, hasara itaendelea kubaki kuwa yetu pia, kumbuka bado tuna uhaba wa wachezaji wenye miguu ya kushoto.




1 COMMENTS:

  1. Makosa si ya Mwinyi ila lazima mjue kuwa timu nzima haikucheza vixuri!! Salah alisoma mchezo na kugundua kuwa stars walikuwa wanatumia full backs kushambulia na kupiga cross ila full backs zinapopanda hakuna watu waliokuwa wanashuka kutake cover hivyo kuwa exposed nyuma!! Tatizo ilikuwa mfumo na ndio maana hata Abdul hukucheza kwa kiwango chake. Alifika sehemu akaogopa kupanda, mtu kama ulimwengu alicheza kifarther mno!! Mchezaji anapoteza mpira anatembea na stars kwa ujumla walikuwa hawakabi kabisa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic