July 25, 2016

MSANII MAARUFU NCHINI, DIAMOND

Na Saleh Ally
GAZETI la Championi lilianza kujulikana kabla ya ujio wa Nasibu Abdul ‘Diamond’. Ninaamini litaendelea kubaki nikiwa ninamaanisha hivi, ataliacha likiendelea kusikika kwa miaka mingine mingi.

Championi litaendelea kusikika kwa kuwa linaundwa na watu wengi makini wanaotaka liendelee kufanikiwa. Zaidi linajengwa na timu, ndiyo maana litakuwa na nafasi ya kufanya vema zaidi kwa kuwa iko makini.

Diamond Platnumz, anaweza kuendelea kudumu kama Championi kama angekuwa ametanguliza umakini na ikiwezekana angependa kuumiza akili yake zaidi na mwisho, asianze kuamini Watanzania wengi ni wajinga na hawajui kabisa.

GARI; DIAMOND 
GARI LIL WAYNE

Juhudi za Diamond ambaye alikulia katika maisha ya shida kutoka katika Kitongoji cha Tandale katika Jiji la Dar es Salaam, zinapaswa kupewa sifa na kuthaminiwa kwa kuwa zinasaidia vijana wengi kutaka kukua zaidi.

Lakini kadiri siku zinavyosonga mbele, inaonekana hivi; Diamond amekwama kiakili, timu inayomuongoza imekwama pia na inawezekana ina watu walioridhika, wanaoamini wamefika au wanafikiri, hakuna anayeweza kumfikia tena Diamond kwa kuwa hakuna kama yeye.

Wanawaza hivyo kwa kuwa wamesahau mengi yaliyopita, kwamba hakuna shoo zilizokuwa zinajaza kama za 2 Proud au Mr II au Sugu. Baadaye ikawa hakuna kama Profesa Jay, Juma Nature, Lady Jaydee na wengine kama makundi ya East Coast, Wanaume TMK na kadhalika lakini sasa wanaonekana ni wa kawaida kabisa.

Huenda wale wana makosa yao, lakini kosa kubwa la Diamond linataka kulingana kabisa na vifo vya bendi za dansi ambazo zilikubaliana na kuamua kuiga kila kitu cha bendi za DR Congo na baada ya hapo zikataka kushindana sokoni na Wakongo.


ANARUKA DIAMOND...

ANARUKA LIL WAYNE
Leo unamuona Koffi Olomide ambaye Muumini Mwinjuma alimkuta sokoni, amemuacha na Mwinjuma kuinuka inaonekana ni hadithi itakayokuwa haina mhadithiaji.

Kwa nini inakuwa hivyo, ni kwa kuwa aliyeanza chake, mara zote anakuwa bora zaidi kuliko anayeiga na tabia ya watu ni kupenda vilivyo bora hasa kwa vile vinavyokuwa vimeanzishwa.

Mafanikio ya kibiashara ni ubunifu mpya kwa kuwa macho na masikio ya mwanadamu huvutiwa na kuona au kusikia mambo mapya na si kurudia na hasa inapozungumziwa ubunifu.


DIAMOND AMETUPA FEDHA, WASIOCHANA WALIOKUWA KANDO YA BARABARA WANAGOMBEA

LIL WAYNE AMETUPA FEDHA, WASIOCHANA WALIOKUWA KANDO YA BARABARA WANAGOMBEA

Kuona, kusikia na kuamini Diamond amekopi halafu akapesti na akarudia mara nyingine ndani ya mwaka mmoja zaidi ya mara tatu, ni kujinyonga kwa njia ya mkato na kutengeneza mwisho wake ingawa yeye anaamini haitatokea.

Diamond Platnumz alimshirikisha AKA wa Afrika Kusini katika Wimbo wa Make Me Sing, ulipotoka watu wengi badala ya kujadili ubora wa wimbo wenyewe, suala la kuiga Wimbo wa Got Money ya Lil Wayne ndiyo likawa mjadala kwa kuwa ilikuwa ni copy & paste bila ya aibu hata kidogo!

Wakati Diamond anatoa wimbo wake, tayari huo wa Lil Wayne ulikuwa umetazamwa na watu milioni 57. Wake ndani ya wiki chache ukawa umetazamwa na watu zaidi ya 600,000. Hapa utajifunza ubora wa usahihi, lakini jiulize hao milioni 57, wangapi waliingia katika 600,000 ya Diamond na wataweza vipi kukichukulia ni kitu kipya na wanapaswa kufurahia. 

WANENGUAJI WA DIAMOND 
WANENGUAJI WA TAYLOR SWIFT

Tena unaona Video ya Got Money ilitoka mwaka 2008, ya Diamond ni miaka zaidi ya mitano baadaye, huenda anadhani Watanzania ni mazumbukuku, hivyo hawawezi kuwa wang’amuzi.

Suala hilo la Diamond kukopi, liliandikwa na gazeti hili Februari 19, mwaka huu kwa kichwa cha habari, “Sare-sare maua”, mwandishi akiwa ni Hans Mloli. Diamond amekaa si zaidi ya mwaka, amerudia jambo kama hilo, ambalo nalo mjadala wake ni “copy & paste”.
Safari hii ‘kahamishiaa’ video kadhaa ndani ya video yake moja ya wimbo wa Kidogo ambao ameshirikiana na P Square. Wimbo ni mpya, mzuri na gumzo lakini video yake imerudi palepale, “ya kuiga”,

Kuiga bila ya kuboresha ni uzembe wa kufikiri, kutojiamini na ikiwezekana naweza kuiita udanganyifu au kuwapotezea watu muda kwa kuwa sina sababu ya kuangalia video ya msanii wa Marekani, halafu nikirejea kuangalia ya Diamond nayo iwe vilevile.

JASMINE V, KIPANDE CHAKE HIKI KIMEIGWA KWENYE WIMBO WA DIAMOND SEHEMU ALIYOIMBA PETER OKOYE WA P SQUARE, ANGALIA PICHA YA CHINI.

Au Diamond anaamini anavijua vitu vya Marekani yeye peke yake pamoja na meneja wake, Babu Tale, Said Fela, Sallam Sharaff maarufu kam SK, wengine wote hawajui au hawajawahi kuona, hivyo hawatang’amua hata kidogo!

Maana katika video ya Kidogo, ndani yake amechukua sehemu zinazofanana kabisa kwa utengenezaji na matukio katika video za wasanii Tyga na Jasmine V.

Ameiga mambo ya video ya Wimbo wa Right There ya Jasmine V, kafanya hivyo kwenye For The Road ya Tyga na kinachoshangaza hadi kukaa na mbwa mweupe, mavazi ya warembo ambayo ni rangi ya njano na bluu na hata mshono.

Hii unaona katika video yake ya Make Me Sing aliiga vitu kama mavazi, aina ya gari, aina ya uvamizi, fedha kutupwa barabarani na wanaogombea ni wasichana ili kuzuia gari la polisi. Unajiuliza, hivi Diamond na timu yake hawana uwezo hata kidogo tu wa kufikiria? Wamechoka au ndiyo wamefika mwisho? Au Diamond alifika hapo kwa nguvu zake na sasa alionao ni wasio na mawazo sahihi na hajui wanamtumbukiza shimoni?


DIAMOND AKIWA KWENYE MAVAZI MEUPE, MBWA MWEUPE ALIYE KULIA KWAKE KAMA ALIVYOFANYA TYGA KWENYE VIDEO YAKE, ANGALIA PICHA YA CHINI!

Mimi najiuliza, hata kama wale wanamtumbukiza shimoni, yeye mwenyewe haoni au hawezi kujiuliza kwamba mambo anayofanya yatamuangusha kwa kuwa kazi zake zinavuka mipaka hivyo itafikia siku moja anachaguliwa kwenye tuzo ya BET au nyinginezo halafu video yake iliyotazamwa na watu 600,000 inashindana na ile yenyewe iliyotazamwa mara milioni 57 na yeye akiwa ameiga.

Vipi Diamond wakati anaingia kimataifa zaidi ndiyo anashindwa kuwa mbunifu zaidi? Anaiga vya wale anaokwenda kushindana nao badala ya kutengeneza ladha mpya? Hata kama Watanzania hawajui kama anavyoamini, ataweza vipi kushindana kimataifa kwa “copy & paste”, tena ya waziwazi na inayoshangaza kama kweli walioamua walikuwa hawajachoka!

Kama watu wanaamini Diamond ndiye bora kuliko wasanii wote kutokana na mafanikio yake, je, wanaomfuatia wanaweza vipi kuiga anachofanya kama mfano au changamoto kama atakuwa anaiga video ya msanii mwingine akashindwa hata kubadili nguo, gari na aina ya kukaa?

MEMBA WA P SQUARE AKIWA KATIKA SEHEMU YA WIMBO WA DIAMOND AMBAO UMEKOPIWA KUTOKA KATIKA WIMBO WA MSANII TYGA HAPO CHINI!


Mfano huyu akiwa na mbwa mweupe, basi Diamond alishindwa hata kutafuta mbwa mweusi ili kuwa kitu tofauti! Jiulize hata ukaaji na upande alivyokuwa amekaa Tyga na Diamond alishindwa kubadili, jamani huyu ni Diamond yuleyule? Au amekubali kutengeneza kifo chake kimuziki, mapema kabisa!

Siku chache zilizopita, unamuona muigizaji maarufu wa Hollywood na duniani kote Terrance Howard akiwa amekaa na simba. Halafu siku chache zinazofuata, unamuona Diamond akiwa naye amekaa na simba kwa mkao uleule akionyesha uvivu wa kufikiri kwa kiwango cha juu tena ajabu zaidi, simba wakiwa wanatokea Afrika na kwenda kufanyiwa kazi Marekani kabla ya Tanzania na yule anayetokea kwenye simba wengi anakubali kuiga vilevile.

Nikajiuliza tena, hivi, kuliko Diamond kukaa kwani angemshika simba akiwa amesimama au anatembea, ugumu ungekuwa nini! Bado ingewezekana Diamond kutafuta mnyama mwingine ili kuepuka kuendelea kuonekana ni aliyechoka.

Inawezekana kabisa, mashabiki wa Diamond wameamua kuamini kila kitu chake ni bora bila ya kuchunguza. Watanzania wote hawawezi kuwa na akili zinazolingana na kwa utandawazi wa kiwango cha juu, dunia sasa ni kijiji. Taratibu ataanza kupoteza mashabiki mmoja baada ya mwingine.

Akiendelea hivi, Diamond lazima akumbuke ‘atajiua’ mwenyewe kwa kuwa wako wengine ‘walijiua’ na leo wanasuasua kurejea kileleni.

TERRANCE NA SIMBA, DIAMOND NAYE AKAKOPI VILEVILE AKIWA NA SIMBA...!!

Kwanza ni lazima abadilike na kama ataendelea hivi, hakuna ubishi, atakwisha na kumalizika kabisa kisanii na mwisho, itabaki stori. Inawezekana anaona sawa kwa kuwa wengi waliopaswa kumkumbusha hasa wanaohusika na sanaa kwenye vyombo vya habari hasa redio na runinga mbalimbali, wamegeuka kuwa wapambe kwake na wanachofanya ni kufurahia kila anachofanya na kusifia ili kuepuka kupoteza urafiki naye!


Mwisho, Diamond anapaswa kukumbuka, miaka sita iliyopita, hakuwa maarufu alivyo sasa na kuna wengine walikuwa wakitamba. Akiendelea hivi, miaka sita ijayo Mwenyezi Mungu akimjaalia uzima, atakuwepo lakini wengine watakuwa wakitamba zaidi yake kwa kuwa watapita katika mashimo ya udhaifu wake wa kuamini Watanzania hawajui lolote, kumbe kuna wengi kwa wingi wanajua mengi zaidi yake kuhusiana na muziki wa ndani na nje ulikotoka na unapokwenda.

6 COMMENTS:

  1. Tumekuchoka wewe Salehe kwa umbumbumbu wako,kama yeye amekopi nawe kakopi uandika kutoka kwa kubwa jinga wa blog fulani!

    ReplyDelete
    Replies
    1. Saleh mbona na wewe una copy kwa gazeti la UK..dailmail? najuae the sun uwezi kupata habari zote mpk ulipie...

      Delete
    2. tatizo letu tunaweka sana mapenzi ata kwa kitu kisichotumia upenzi.... Salehe hana kosa,bali anataka Diamond afanikiwe zaidi,DIAMOND na management yake wanatakiwa wawe wajuzi wa kufikiria ili wakitoa video iwe new ata wa marekani na nchi nyingine waikubali...... safi sana Salehe Jembe...na kama kuna wengine waumbue tu

      Delete
    3. tatizo letu tunaweka sana mapenzi ata kwa kitu kisichotumia upenzi.... Salehe hana kosa,bali anataka Diamond afanikiwe zaidi,DIAMOND na management yake wanatakiwa wawe wajuzi wa kufikiria ili wakitoa video iwe new ata wa marekani na nchi nyingine waikubali...... safi sana Salehe Jembe...na kama kuna wengine waumbue tu

      Delete
    4. tatizo letu tunaweka sana mapenzi ata kwa kitu kisichotumia upenzi.... Salehe hana kosa,bali anataka Diamond afanikiwe zaidi,DIAMOND na management yake wanatakiwa wawe wajuzi wa kufikiria ili wakitoa video iwe new ata wa marekani na nchi nyingine waikubali...... safi sana Salehe Jembe...na kama kuna wengine waumbue tu

      Delete
  2. Duh watu hawataki kukubali je wimbo wa diamond wa je utanipenda nao kakopi kila kitu kwenye wimbo wa r city unaitwa locked away .... huu ni uvivu wa kufkiria wa dimond namkubali sana ila kazidi kutuibia

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic