July 9, 2016

MAHADHI
Daktari wa Yanga, Edward Bavo amemthibitishia kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm kwamba kiungo wao Juma Mahadhi atakuwa fiti kucheza dhidi ya Medeama ya Ghana wikiendi ijayo.

Mahadhi alikuwa anafanya mazoezi ya binafsi kwa muda wa wiki moja na nusu akisumbuliwa na majeraha ya nyonga aliyoyapata wakati Yanga ilipocheza na TP Mazembe kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kiungo huyo aliyejiunga na Yanga hivi karibuni akitokea Coastal Union ya Tanga, aliichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza katika Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe na sasa atacheza dhidi ya Medeama.

Juzi jioni Mahadhi alifanya mazoezi ya nguvu na wenzake kwenye Uwanja wa Boko Veterani huko Boko jijini Dar es Salaam akijiandaa na mchezo huo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho. 

Kocha wa Yanga, Pluijm raia wa Uholanzi amesema: “Nafurahi kuona Mahadhi amerejea na kupunguza idadi ya majeraha kwenye kikosi changu, nina uhakika atacheza dhidi ya Medeama nimemuweka katika orodha yangu.”

Naye daktari wa timu hiyo, Bavo alisema: “Mahadhi kwa jinsi  anavyokwenda ni wazi atacheza mechi na Medeama kwani ameonyesha maendeleo makubwa sana, ni furaha kwa kikosi chetu.”

Yanga itacheza na Medeama Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuwakubalia ombi lao la kucheza siku hiyo.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic