July 11, 2016


Na Saleh Ally
ACHANA na sakata kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Yanga liendelee, ingawa mimi nashangazwa na mengi katika hili hata kama wengi watakuwa wanaona ni jambo la kawaida.
Wakati nashangazwa na hilo, nimekuwa nikiumizwa kutokana na kuona Watanzania wanaendelea kuwa ni gundi ya uelewa katika suala la umoja na upendo na wanazidi kuonyesha picha mbaya na ya hovyo kabisa.

Picha ya hovyo kwa kuwa wakati Yanga imefanikiwa kuingia katika hatua ya nane bora kwa mara ya kwanza katika michuano ya Kombe la Shirikisho, sasa wako vitani dhidi ya TFF.

Baba na mtoto wakipambana wenyewe kwa wenyewe wakati adui anaendelea kujiandaa kushambulia nyumba yao kwenda kwenye mafanikio. Hata wewe nitakuuliza, nani hapa anaonekana si mwenye kufikiri, asiyejua au kujali kulingana na wakati wa kushughulikia tatizo fulani?

Unaweza ukaniambia hivi; kama mtoto ni mjeuri basi baba anaweza akamfundisha adabu kwa kumpa adhabu. Lakini unajua kama wazazi wakipishana kitu wakiwa sebuleni wanatakiwa kuendelea kucheka tu hadi watakapoingia chumbani na kumalizana!

Huenda huu ungekuwa ni wakati wa baba kuangalia huyu mwanaye anafanyaje wakati huu. Halafu akajua namna ya kulishughulikia hilo suala. Maana mwendo ulivyo unavuka hadi katika suala la msemaji wa klabu, halafu inaonekana kama TFF ingefurahi sana Yanga kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) au serikali. Tena imegeuka hadi kuwa mkusanya kodi, maana iliandika barua ikitaka eti walipe kodi kwa kuwa wameingiza watu bure.

Lakini siku chache Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikatoa tamko na kuimbua TFF ambayo ilionekana imekurupuka na ilipenda kuona Yanga inaadhibiwa au kupata hasara. Hakuna anayeweza kukataa kuhusiana na suala la kwamba TFF imekerwa na ina hasira na suala la Yanga kuingiza mashabiki bure.

Inawezekana Yanga wamejipa hasara kubwa, lakini vipi TFF ndiyo wanaumia sana? Kwani wamekosa kipi, ni yale makato ya mgawo pekee, au kumekuwa na kitu nyuma ya pazia? Kama hakuna, vipi ugomvi unakua na inaonekana ni kama kuonyeshana mabavu.

Siku nne baada ya Jerry Muro kuonekana amewavuruga TFF, kamati ya Maadili ilikaa, ikaonekana mwaliko wake ulikosea, haikupita wiki ikakaa tena, hii inashangaza sana.

Maana TFF hadi leo haijakaa katika makosa kibao likiwemo lile la Donald Ngoma wa Yanga kumshambulia Hassan Kessy wa Simba (wakati huo) kwa kumpiga kiwiko katika mechi ya mzunguko wa kwanza wakati Yanga na Simba walipokutana.

Lakini hili ndani ya wiki mbili, tayari kamati imekaa mara mbili na kuhakikisha inafikia maamuzi ambayo ilikuwa imepania kuyafikia na kukata kiu ya matamanio ya mabosi au watu waliotaka kuonyesha nguvu zao.

Kuna walakini wa hali ya juu ambao hakika ni harufu mbaya ya uozo wa kushindwa kujitambua, harufu mbaya ya kutoelewa ukitendacho kama nani katika nafasi ipi na unatakiwa kufanya kipi kwa wakati gani!

TFF ilikuwa lazima imshughulikie Muro haraka sana, iingie katika malumbano na Yanga. Wakati huohuo imekaa kimya kuhusiana na madudu kibao kama hilo la Ngoma. Wakati ule walikaa kimyaa wasiivuruge Yanga au walikaa kimya ili waikomoe Simba au walifanya hivyo kwa kuwa suala hilo haliwaumizi na si maslahi yao?
Naendelea kuwa mstari wa mbele kusema nina hofu sana na mwendelezo wa mambo ya TFF ambayo inajitahidi kumziba mdomo kila anayejaribu kuikosoa. Inajitahidi kuhakikisha inakuwa safi kwa kujipaka vumbi ikiamini halichafui sana kama kujipaka tope.
Kinachoendelea sasa kati ya TFF dhidi ya Yanga ni sawa na kuku anayejaribu kuyachezea mayai yake mbele ya kenge mwenye njaa. TP Mazembe, MO Bejaia wanashirikiana na mashirikisho yao, wanaendelea kujiandaa, TFF inaendelea kuyasogeza mayai yake mdomoni mwa kenge!




2 COMMENTS:

  1. Hiyo ndio TFF mweeh!
    MUDA WAO UFIKE WAONDOKE,WANACHOSHA.

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli nakupongeza sana kwa uchambuzi wako makini na mara nyingi sana hufuatilia blog yako jinsi unavyoelimisha jamii na kutupa habari za kila siku za michezo ulimwenguni Mungu akupe umri mrefu na ufanisi zaid wa kazi zako (Amin) Ni wakati wa kukaa na kujiuliza (TFF) wapi wanalipeleka soka la Tanzania jee huu mwelekeo wanaokwenda na sahihi na lazima wajifunze wamekosea wapi na wajirekebishe vipi sio kujifanya wababe tu mbele ya vilabu ambavyo vinawaingizia mamilion ya fedha za kuendeshea maisha yao na familia zao huo mwenendo wao wa uongozi wa soka hakuna sehemu yeyote ulimwenguni (ubabe kwenda mbele) huo si uongozi uliotarajiwa na wapenda soka wote Tanzania watu walitarajia maendeleo sio kugombana na vilabu ni vyema muondoke kwa kweli mmefeli kw asilimia mia kwa mia hamfai na sis tushawachoka ondokeni wakae wengine wasio na njaa kama uongozi wa soka wa sasa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic