July 13, 2016


Timu ya vijana ya Kenya, imefuta ziara yake ya kwenda Dar es Salaam kwa ajili kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys.

Mchezo huo ulipangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Julai 23, 2016.

Kwa mujibu wa barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), Robert Muthomi kwenda Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kufuta kwa ziara hiyo kunatokana na nafasi ambayo Kenya imeipata.

Timu ya Taifa ya Vijana ya Kenya imeteuliwa kushiriki michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la COSAFA inayotarajiwa kuanza Julai 22, 2016 hadi Julai 31, 2016 mara baada ya Msumbiji kujitoa kwenye mashindano hayo.

“Tunaomba kukutarifu kuwa timu yetu imetuliwa katika michuano ya vijana ya COSAFA, hivyo ziara yetu Tanzania haitakuwako kama ambavyo sisi wenyewe tuliomba mchezo huo kwenu (TFF) ufanyike Julai 23, 2016,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Muthomi.

Licha ya kwamba mchezo huo hautakuwako, ratiba ya Serengeti Boys ambayo inapambana kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa Afrika hapo mwakani, imebaki vilevile kwa timu kuingia kambini Jumapili Julai 17, 2016 kwenye Hosteli za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo inayonolewa na Bakari Shime itapiga kambi ya wiki moja katika hosteli hizo, kabla ya kwenda Madagascar ambako itapiga kambi ya takribani wiki mbili ikiwa ni ahadi ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi ambaye alitoa ofa hiyo baada ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa.

Serengeti Boys inatarajiwa kucheza na Afrika Kusini kati ya Agosti 5, 6 au 7, 2016 huko Afrika Kusini kabla ya mchezo wa marudiano utakaofanyika saa 9.00 alasiri, Agosti 14, 2016 kwenye  Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi, Dar es Salaam.


Mshindi wa jumla katika michezo hiyo, itacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic