July 11, 2016

KIIZA
Imefika tamati! Simba imeamua kutegua kitendawili na kukiri kuwa msimu ujao hawatakuwa na mshambuliaji Mganda, Hamis Kiiza na tayari wamemalizana kwa amani.

Tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Bara 2015-16, kumekuwa na taarifa mbalimbali juu ya kutemwa kwa mshambuliaji huyo kutokana na sababu za utovu wa nidhamu lakini hakukuwa na kiongozi aliyewahi kuthibitisha kuhusiana na hilo zaidi ya kutoa kauli zenye viashiria vya hali kama hiyo.

Aidha, ilielezwa kuwa Kiiza anaweza kutemwa pamoja na Mganda mwenzie, Juuko Murshid kutokana na kufuata mkumbo wa kugoma kuichezea timu hiyo mpaka wapewe mishahara yao.

Rais wa Simba, Evans Aveva amesema kuwa sasa ni rasmi wameshampa Kiiza mkono wa kwaheri na hakuna tena kilichopo baina yao na zaidi wamemtakia kila la kheri huko aendako pamoja na kumshukuru kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa timu hiyo msimu uliopita.

“Niseme tu kwamba tumemalizana kistaarabu kabisa na Kiiza na tunamtakia mema, kila la kheri huko aendako lakini pia kwa kweli tunamshukuru kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Simba msimu uliopita,” alisema Aveva.


Kiiza aliyewahi kuichezea Yanga anaungana na wachezaji wengine wa kigeni waliotemwa msimu huu klabuni hapo; Mkenya, Raphael Kiongera, Mrundi, Emiry Nimubona na Mganda, Brian Majwega.

SOURCE: CHAMPIONI.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic