July 29, 2016


MURO
Na Saleh Ally
METHALI inayonivutia katika zile za Kiswahili ni ile ya “simbiko haisimbuki ila kwa msukosuko”.

Yaani “Chombo huchakaa kutokana na matumizi yake”. Hakuna anayeweza kukataa tena kwamba mpira wetu umechakaa. Kwa kuwa matumizi yake ni mabaya na yamekuwa matumizi binafsi zaidi.

Matumizi ya soka nchini ni kwa ajili ya watu wachache, wanaoturudisha nyuma katika zile enzi za akina Muhidini Ndolanga na Ismail Aden Rage, kila kukicha ni migogoro na hakukuwa na faida ya soka uwanjani, badala yake mezani.
Wakati Chama cha Soka Tanzania (Fat) kinahama, ilikuwa ni faraja kwa wapenda soka, maana kila mmoja alitamani kiende zake, walichoka kwa kuwa kilikuwa ni chama cha migogoro na faida za wachache.

Wakati ameingia Leodegar Tenga na kuwa mtu wa kwanza kuongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kukawa na matumaini makubwa na mwenendo wake ukaonyesha nafuu, soka likarejea uwanjani na malumbano yakapungua kwa asilimia kubwa. Huenda hata ugombeaji wake wa madaraka ulikuwa rahisi, wengi walimkubali ndiyo maana akapita mihula miwili kwa ulaini kabisa kama ilivyokuwa kwa Barack Obama wa Marekani.

Inawezekana kabisa, Tenga atabaki kuwa mgombea pekee wa TFF aliyeonekana angalau angegombea hata mhula wa tatu kwa kuwa waliokuwa wakigombea mhula huo, hakuna aliyeonekana ana uwezo wa kuvaa viatu vyake vizuri na kuendeleza mambo. Ukweli haujifichi, angalia sasa mambo yanavyokwenda.

Ninaamini sana methali hii; “Adui shujaa ni bora kuliko rafiki mwoga.” Kinachoiua TFF ni kwa kuwa uongozi wake umekubali kuwakumbatia marafiki wao, marafiki ambao hawawezi kusema ukweli pale uongozi huo unapoyumba au kukosea na wako tayari kushiriki katika kila udhaifu wao kama sehemu ya kuwaridhisha mabosi na kulinda nafasi zao.

Uongozi wa TFF, hautaki maadui mashujaa, wanaoweza kusema kweli kuwa suala la kufungia watu kwa visasi, ili mradi au kuwakomoa kwa kuwa wanaonekana ni tatizo kwa uongozi wa shirikisho hilo ni kujirudisha nyuma.

Nilizungumza awali, kwamba mdau wa soka nchini, Dk Damas Daniel Ndumbaro alifungiwa akizitetea klabu dhidi ya ubabe wa TFF, wadau na waliokuwa wanatetewa wakawa waoga na kunyamaza kimya.

Nikasema hivi; mmekaa kimya lakini aliyezoa vya kunyonga, vya kuchinja hamviwezi. TFF wataendelea na hili ili kuwatisha wengine na wao wajitengenezee njia ya kupita tena waendelee kufanya wanavyotaka na kuudidimiza kabisa mpira nchini.

Sasa ni Jerry Muro, hakuna sababu ya msingi inayoainishwa inaweza kugonga kwenye masikio ya mtu mwenye akili timamu ili aamini kweli alikuwa na kosa la kufungiwa na kupigwa faini, mimi ninaona ni dhuluma ya uhuru wa kuongea na dhuluma ya wazi ya riziki ya mtu.

Mnayezuia asifanye kazi na kumpiga faini ya fedha ni ujinga wa hali ya juu. Muro hakutukana, alipambana akiwakilisha klabu yake katika suala la uamuzi wao wa kuingiza watu bure. Hakuwahi kusababisha jambo lolote baya wala kusema maneno ya kashfa kwa TFF, amefungiwa akiwa nje ya kikao, akiwa mapumzikoni na kama unakumbuka Dk Ndumbaro alifungiwa kwa kuwa siku aliyoitwa alikuwa safarini Marekani ambako alialikwa na moja ya vyuo vikuu kufundisha. 

Kumbuka yeye ni mwalimu wa Chuo Kikuu Huria (Out) na Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).
Muro amefungiwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF ambayo inaundwa na watu walioteuliwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Ambaye ndiyo mkuu wa shirikisho lililokuwa likiandamwa naye akipinga mambo kadhaa ambayo hayakuwa sahihi.

Hakuna anayesema, serikali haiwezi kuingilia. Yanga inaonekana haina njia ya kujitetea au kumtetea, lakini hadi sasa hukumu kuitoa pia imekuwa shida ili kuweka wazi makosa yake. Nimeambiwa hadi Yanga wameandika barua kuiomba, hii si sawa.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT), lipo kimya, hakuna linachokifanya na huenda wamekaa wakisubiri kukabidhiwa kwa bendera timu ikiwa inaondoka.

Ukimya, maana yake baada ya Muro ‘anayeuawa kitaaluma’, kikazi na kadhalika maana yake, TFF imdungue mwingine naye ‘afe’.  Kwa kuwa hakuna wa kuizuia, mwingine ajiandae, soon itaelekeza mtutu wake msipopajua. Hasa kwa wale wanaotaka kupunguza kasi yake ya kuingia madarakani.

Inaonekana kamati zake ndiyo mitutu ya kuwamaliza wasemakweli wote. Inawezekana Simba, watasherekea lakini siku atafungiwa Haji Manara na itakuwa rahisi kufanya hivyo kwa kuwa TFF itakuwa imeishazoea vya kunyonga, mwisho hakuna atakayesema tena.


Simameni, semeni ukweli na muache uoga usiokuwa na sababu. TFF haikuwa na sababu za msingi za kumfungia mwanahabari Muro. Acheni ushabiki, simamieni kwenye haki. Hatuhitaji TFF hodari ya kuziba watu midomo wasiseme ukweli, wakati imefeli kupita kiasi katika kuleta maendeleo.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic