July 2, 2016

MALINZI

Na Jackson Lyase
JUMANNE iliyopita, uongozi wa Yanga ulichukua uamuzi mgumu wa kutaka mashabiki waingie bure wakati wa mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na timu kubwa na maarufu Afrika ya TP Mazembe kutoka nchini DR Congo.

Zoezi hilo lilifanyika na kweli mashabiki wakajitokeza kwa wingi na kuujaza Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku wengine wakibaki nje na kulazimisha kuingia.

Lilikuwa ni jambo la kushtua kidogo hasa kama utafikiria vipi Yanga wanaotaka mapato ya mlangoni halafu wanaamua kuingiza watu bure katika mechi ambayo wanategemea kuingiza watu wengi na wapate fedha.

Mjadala ulikuwa mkubwa kwa rafiki zangu na hasa mtaani, siku ya mechi nilisafiri kutoka Mbozi hadi Mbeya ambako pia nilikuta mjadala mkubwa unaohusiana na hilo na kila mmoja alikuwa na mtazamo wake.

Wapo waliofika mbali zaidi na kujadili kishabiki, suala la Usimba na Uyanga likatawala. Kitu ambacho sikuona kama kilikuwa kizuri au kilikuwa ni hoja ya kujadili hasa kwa watu waliotaka kujifunza.

Maswali yangu mimi yalibaki kwenye kwa nini Yanga waingize watu bure? Lakini majibu yalikuwa mengi na mwisho nikaishia kuyapata mengi ambayo ninaweza kuchangia nanyi, ndiyo maana nikaomba kuandika katika gazeti hili la Championi kwa kuwa ninaamini linawafikia watu wengi, wanipe nafasi hii.

Unaweza vipi kuwalaumu Yanga kuingiza watu bure wakati hata kama wangeruhusu huenda mapato ambayo wangechukua siku ile baada ya makato yote, yasingezidi hata Sh milioni 30.

Kumbuka faida kubwa ingekwenda kwa TFF, TRA na wengine wanaohusika na makato. Yanga ambayo inaongozwa na Mwenyekiti Yusuf Manji, ingepata kiduchu kabisa na hii ingechangiwa na mechi kuonyeshwa moja kwa moja kwenye luninga.

Lakini kuingiza mashabiki wengi, moja ni kuwa karibu na mashabiki hao na kuwaonyesha utamu wa kuona moja kwa moja wakiwa uwanjani kuliko kupitia luninga.

MANJI
Pia ni kuipa nguvu timu yao na hicho kilifanyika uwanjani siku hiyo ambayo ni jambo jema na huenda wakati mwingine mashabiki nao waonyeshe uungwana na kujitokeza kwa wingi kwa kulipa kiingilio.

Tofauti na majibu hayo, niliona hivi; TFF wanatakiwa kuiga mfano huo wa Yanga. Inawezekana Yanga wakapata hasara kwa kuwa wana wadhamini wachache sana. Lakini vipi TFF nao wasiweke kiingilio cha chini au kuacha mashabiki waingie bure katika baadhi ya mechi za Taifa Stars?

Tumeona nchi kadhaa wamefanya hivyo. TFF hawawezi kupata hasara hata kidogo, nitaeleza kwa nini ninaamini hivyo.

TFF inaingiza zaidi ya Sh milioni 500 kwa mwaka kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), una udhamini zaidi ya Sh bilioni moja kwa mwaka kutoka TBL, inaingiza fedha lundo kutoka Vodacom, Azam Media na kadhalika.

Inalipwa kwa ajili ya uendeshaji wa ligi, timu ya taifa na mambo mengine. Fedha za uendeshaji masuala ya ofisi pia nyingi zinapitia humo katika mikataba.

Sasa kama wana fedha hizo, vipi wasiamue kubadili mambo ili Taifa Stars isionekane ni mtaji au chanzo cha fedha na kwa kuwa timu yenyewe inasua, basi mashabiki waingie kwa wingi na kuiunga mkono.

Mtazamo wangu, naona walichofanya Yanga, inawezekana walitakiwa kufanya TFF wakati wa mechi ya Taifa Stars ikiwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika na Kombe la Dunia.

Gharama karibu zote zinakuwa chini ya wadhamini. Kiasi kidogo inachopata kwa ajili ya maendeleo kutoka Fifa, hatuoni maendeleo yenyewe, vizuri basi zikatumika katika uhamasishaji wa mapenzi ya Taifa Stars.

Najua kila mmoja atakuwa na mtazamo wake, lakini niwashauri TFF kujifunza kupitia hili jambo la Yanga. Wasifanye uadui na kuwachukia, badala yake wajifunze na watagundua jambo kwa faida yao.

Kama kweli Yanga wamekosea, wajifunze na kuwasaidia. Kama wanaona walikuwa sawa, basi waache hasira za hofu ya kukosa mapato (kama wanazo) basi washirikiane pamoja.
Yanga inatokea Tanzania na TFF ipo Tanzania. Kuanza kugombea fito ni kupoteza muda mwingi wa maendeleo ya mchezo wa soka.


Jackson Lyase ni msomaji mkubwa wa Gazeti la Championi anayeishi mjini Mbozi na anapatikana kwa barua pepe  jlyase06@yahoo.com

SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. Hizi tuwe nazo makini haiwezekani mashabiki walipie kuiona Ndanda na isiwe hasara but kulipia kuiona Mazembe kusilete faida. Kuweka bure hakuwezi kuwa suluhu ya kujaza watu viwanjani.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic