July 9, 2016


Na Saleh Ally
KULIKUWA kuna kampeni za chinichini kutaka kubadili mwendo, kwamba mchezo wa soka usiwe ule unaopendwa zaidi kuliko mingine duniani.

Huenda walioamua kufanya hivyo walichoshwa tu kwa hisia zao, wakataka kuona mabadiliko. Huenda hilo halitawezekana milele.

Mchezo wa soka ni ule unaofurahisha wengi pia unawaudhi na kuwaumiza wengi, lakini siku zote umekuwa ukiacha mgawo wa furaha na maumivu utambae kila sehemu na si kubaki upande mmoja.

Hata Tanzania licha ya kukosa viongozi bora kuna siku timu zake husherehekea jambo fulani ambalo maana yake ni ushindi.

Lakini mpira uko ‘fea’ kweli. Unaweza kujichagulia adhabu kutokana na unavyojipanga. Ubora unaweza kukusaidia lakini pia unaweza usiwe msaada kama utakuwa umekosea hesabu.


Vizuri kuitumia mechi ya nusu fainali ya michuano ya Euro kati ya Ufaransa dhidi ya Ujerumani ambayo ni timu bora sasa kati ya zile za taifa, duniani kote.

Ujerumani ambao ni mabingwa wa dunia, walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kufika fainali ya Kombe la Euro linalomalizika nchini Ufaransa, kesho na ikiwezekana kwenda nalo Ujerumani, hasa baada ya mabingwa Hispania, kuvuliwa, wakarejea kwao na kuliacha.

Mechi dhidi ya wenyeji Ufaransa, ambao pia wanapewa nafasi ya kulibeba, ilionekana wazi wenyeji wamekwisha maana walikuwa wanakutana na watu wa kazi kweli. Lakini bado soka likazidi kuonyesha kila kitu kinawezekana na usichokitarajia ndicho hutokea.

Katika soka hakuna miujiza, kila kitu kipo wazi na mchezo wenyewe unachezwa hadharani tena kwenye uwazi mkubwa sana. Ninaamini mashabiki, makocha na wachezaji wa Ujerumani hawakuwa na usingizi.

Ujerumani ilitawala katika mchezo huo kwa kila kitu, maana ukiangalia takwimu ilizidiwa kitu kimoja tu na Wafaransa nacho ni rafu. Hadi mwisho wa dakika 90, Ujerumani walikuwa na faulo 8 na Ufaransa 12. Vitu vilivyobaki, wao walikuwa bora zaidi.


Wajerumani walimiliki mpira kwa 65% dhidi ya 35% ya wenyeji, walishambulia mara 17 dhidi ya 15 lakini ubora ukapungua katika mashambulizi yaliyokuwa na tija, kwani Ujerumani walikuwa na 6 wakati Ufaransa walikuwa na 7.

Ujerumani walipiga pasi 574 na zilifika kwa 90% wakati Ufaransa walipiga 247 na zilifika kwa 82%.

Unaweza kuigeuza mechi hii kama somo kubwa na ujuzi wa makocha wanaoweza kuutumia. Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps aliukubali ubora wa Ujerumani na alichofanya ni kusoma ubora na upungufu wao na akautumia.

Kwanza alijiimarisha kuhakikisha ubora wa wapinzani haufanyi kazi, utaona hakukuwa na makosa ya ‘kijinga’ katika safu ya ulinzi kama yale ya katika mechi ya robo fainali dhidi ya Iceland ambayo walishinda kwa mabao 5-2.


Akaangalia, nini Ujerumani wanakosa. Pamoja na wapinzani wao kumiliki sana mpira, walichofanya ni kupata mabao ambayo yanaamua matokeo ya mchezo. Bao la kwanza ni kosa kutoka kwa mchezaji mkongwe, Bastian Schweinsteiger lakini unaona kosa la pili ni la kijinga zaidi ambalo anafanya beki kinda aliyetaka kupiga chenga ndani ya 18.

Ufaransa walijua mabeki wa kati wa Ujerumani hasa wanapomkosa, Mats Hummels wanakuwa hawana kasi. Wamemtumia Antoine Griezmann kukimbia kwa kasi kwenda langoni kila alipopata mpira.

Hapa ishu haikuwa chenga au kwenda kupiga krosi, badala yake kupita katikati kwa nguvu maana Chris Boateng na hata kiungo namba sita, Schweinsteiger wote hawana kasi. Hivyo ni rahisi mtu kama Griezmann kupata nafasi ya kupiga au faulo.

Ujerumani bado ni bora, lakini kwa mechi hiyo Ufaransa walikuwa bora zaidi katika kuamua matokeo na kujilinda kwa ubora wa juu kabisa kwa kuwa walijua wanakutana na timu ya namna gani.

Maana ya kocha, inaonekana katika mechi kama hiyo na utasema kweli aliusoma mchezo na ubora wa Ujerumani. Ubora wa wachezaji unaonekana hapo pia, kwamba walielezwa cha kufanya, wakatimiza sahihi, huo ndiyo weledi bora katika utendaji.


Soka, unaamua mwenyewe, matokeo unapanga mwenyewe na hata furaha au majonzi unachagua mwenyewe. Mechi hiyo ya nusu fainali ambayo kila mmoja anaweza kujifunza, hata Ujerumani na Ufaransa, kila upande walichagua wanachotaka.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic