August 8, 2016


Kocha wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm, ameshindwa kujizuia na kuanza kuwamwagia sifa wachezaji wake waliotua klabuni hapo hivi karibuni; Mzambia, Obrey Chirwa na Andrew Vincent ‘Dante’ akidai kuwa ni chaguo sahihi kuelekea kwenye msimu ujao unaotarajiwa kuwa mgumu zaidi.

Pluijm ambaye si mwepesi wa kuzungumzia mchezaji mmojammoja, alilazimika kuwazungumzia wachezaji hao kutokana na uwezo wa juu waliouonyesha katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar juzi Jumamosi na kumalizika kwa suluhu.

Kuhusu Dante, Pluijm alisema si mchezaji wa kukaa benchi na kwa uwezo anaouonyesha hajajua itakuwaje kuelekea msimu ujao, kutokana na ushindani ulioongezeka katika nafasi ya beki wa kati tangu alipotua katika kikosi hicho akitokea Mtibwa.

“Umemuona alivyokuwa anacheza leo (juzi), mipira yote ya juu alikuwa anaimudu, pasi zake zote alizopiga zilifika sehemu husika, kasoro moja tu. Amedhihirisha si mchezaji wa kuja kukaa benchi, maana kiwango chake kinashabihiana na mabeki wengine aliowakuta hapa (Kelvin Yondani, Vincent Bossou na Nadir Haroub ‘Cannavaro’). Tusubiri kuona msimu ukianza itakuwaje, maana ni mchezaji mwenye kiwango cha juu.

“Umeona hata Chirwa amecheza vizuri sana, amekuwa akipambana kila mechi, mfano leo alikuwa akitengeneza nafasi nyingi, amejaribu kupenya kufunga kila wakati lakini alikosa msaada kidogo tu, ni dalili nzuri kuelekea msimu ujao,” alisema Pluijm.

Dante, Chirwa ni kati ya wachezaji waliosajiliwa Yanga hivi karibuni kwa ajili ya kuiongezea nguvu timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na ligi kuu msimu ujao. Wengine ni kipa Beno Kakolanya aliyetokea Prisons, Hassan Kessy (Simba) na Juma Mahadhi (Coastal Union).



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic