August 19, 2016


SALEHJEMBE, AKIWA NJE YA UWANJA WA CAMP NOU JIJINI BARCELONA, JANA.


Na Saleh Ally, Barcelona
UWANJA wa Camp Nou ni mali ya Klabu ya Barcelona ambayo inamilikiwa na wanachama lakini una miongozo kadhaa yenye utamaduni wa aina yake.

Neno Camp Nou ni katika lugha ya wenyeji wa hapa, yaani Kihispania. Kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili, neno hilo maana yake ni Kambi Mpya.

Nakukumbusha tu kuwa ni uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 99,354 waliokaa vitini. Hii inaufanya kuwa wa pili kwa ukubwa kwa maana ya kuingiza watu wengi, duniani. Unaoongoza ni Uwanja wa Rangrado May Day wa Korea Kaskazini.

Idadi hiyo ya kuchukua watu 99,354 inaufanya Uwanja wa Camp Nou kuwa wa kwanza kwa ukubwa nchini Hispania na barani Ulaya kote ambako unafuatiwa na Wembley wa England unaochukua watu 90,000.

Kweli ni “Kambi Mpya”, lakini ni jina lililoanza mwaka 1957 tangu walipohamia. Umeendelea kuwa mpya kutokana na marekebisho kadhaa na kama hiyo haitoshi, uwanja huo ni mtaji mkubwa kwa Barcelona.


Wakati nikifanya ziara kadhaa maeneo ya karibu ya uwanja huo, ndani pia, kilichonivutia ni mpangilio na namna unavyotoa ajira kwa Wahispania zaidi ya 150.

Watu wanaofanya kazi hapo ni wale wanaohusika na matengenezo kwa maana ya mafundi, wanaoutunza uwanja, watunza majani ya uwanja na wale ambao wanakuwa katika baadhi ya ofisi za Barcelona.

Hawa wote wanalipwa na uwanja huo kwa kuwa umeendelea kufanya kazi hata siku ambazo si za mechi kwa kuwa watu mbalimbali wanafika kuutembelea, hivyo kuufanya kuingiza zaidi ya euro milioni 1.5 (zaidi ya Sh bilioni 3.6) kwa mwezi kwa shughuli za kawaida tu, nje ya mechi ambazo hutumiwa na Barcelona.


Kwa Barcelona, Camp Nou ni mtaji mkubwa ambao huenda Yanga na Simba wanaweza wakajifunza mengi na kujiona wamechelewa kujenga viwanja vyao kwa kuwa bado tunaweza kuona uwanja hauna maana ya sehemu ya kuchezea pekee, badala yake, uwanja ni mtaji au biashara kubwa.

Klabu ya Barcelona inautegemea kwa asilimia 61 uwanja huo ili kujipatia matangazo zaidi, asilimia 39 iliyobaki inaweza kuwekwa sehemu nyingine, ikiwemo kwenye jezi za klabu hiyo.

Wakati nafika hapa, nilikuta ule mjadala wa uwekezaji wa uwanja huo umefumuka upya, Barcelona wakiamini unaweza kuwaingizia fedha nyingi zaidi kama watafanya kama ilivyokuwa kwa Arsenal na jina la Emirates au Man City na Etihad kwa kuwa klabu hulipwa fedha nyingi mwekezaji kuwekeza jina lake kwenye uwanja ambao tayari ulikuwa maarufu.

Uwekezaji huo unaonekana kupingwa na wengi, kamwe hawataki kuona jina Camp Nou linapotea. Wanaona ni utamaduni, sifa au kitu cha kujivunia na wanapenda kubaki jina hilo ili wajisikie raha kufika hapo na wanachama wengi ambao ni wamiliki wa klabu wanaona bora kuendelea kubaki na jina hilo.


Wameelezwa, kwamba maisha yanabadilika na utaona Barcelona ilikuwa ikilipa euro milioni 1.5 kwa Unicef ili itumie jina lake kwenye jezi zake. Ilikuwa klabu pekee inayomlipa mdhamini halafu inamtangaza lakini baadaye mambo yakawa magumu ikalazimika kuchukua mamilioni ya Qatar Airways ambayo ni Shirika la Ndege la Qatar.

Sasa suala la fedha linahitajika, mtaji mkubwa Barcelona kibiashara ni wachezaji watatu, Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar ambao Barcelona inaona angalau ni vizuri kukaa nao kwa miaka mitano mingine ijayo, lakini bila fedha ndoto zao hazitatimia.

Barcelona wanajua wapinzani wao wakubwa Real Madrid katika suala la fedha, wamewahi kuwanunua wachezaji kadhaa nyota kama Ronaldo di Lima, Luis Figo na wengine. Kwa sasa kumuuza mmoja kati ya Suarez, Neymar au Messi kwenda Madrid itakuwa ni faida ya muda mfupi lakini kibiashara, itachukua muda mrefu.

Hivyo, Barcelona inahitaji uwekezaji na mwekezaji akaribishwe Camp Nou na hakuna ubishi, atakayewekeza lazima atakuwa anahitaji kujitangaza na lazima atataka kubadili jina.


 Hili linaonekana kuwakera wengi, mmoja wa manahodha waliokuwa na mafanikio ndani ya Barcelona, Cares Puyol naye ameamua kufungua mdomo na kusema, kuvunja jina la Camp Nou, ni kuiondoa Barcelona kwenye ramani ya soka duniani kwa kuwa inaonekana ndiyo maarufu zaidi kwa klabu za Bara la Ulaya.

Anaamini na kukubali klabu inahitaji fedha ili kujilinda na mawimbi ya kifedha yanayotarajiwa japokuwa anaona kuna mbinu zaidi za kuweza kuikomboa Barcelona na soka la vijana ndiyo njia pekee.

Puyol amesema kupitia kituo cha kukuza vijana cha La Masia, au kushikilia suala la vijana, itakuwa ni msaada mkubwa sana.

Kibiashara, Barcelona imebadilika kwa kuwa ilitaka kupambana na masoko. Neymar alichukuliwa kwa ajili ya Brazil maana ilionekana wengi kutoka katika nchi hiyo kama wanataka kuiweka kando Barcelona na kuonekana ni kama ya watu wa Argentina anakotokea Messi, jambo ambalo halikuwa zuri kwao.


Suarez alichukuliwa kwa biashara ya Uruguay lakini kuongeza ushindi kwa kuwa anaaminika bora katika ufungaji mabao. Kawaida biashara hukua au kupaa timu inapofunga mabao mengi au kushinda mechi nyingi. Hivyo biashara yote ya soka, inategemea zaidi ya kufanya vizuri kwa timu.

Jina la Camp Nou linaendelea kuwa utatanishi wa kipi sahihi cha kufanya kulingana na muda. Tayari Barcelona wameonekana kuingia hofu kwamba kuna hatari inakuja mbele na wanaweza kujikutana wanawauza kati ya nyota wao hao watatu, jambo ambalo linaonekana halikubaliki kuanzia utosini mwa Barcelona hadi kwenye unyayo wake.

Nitakuwa zaidi Barcelona kwa siku moja, ninaamini nitapata nafasi nyingine ya kukuletea taarifa kuhusiana na Barcelona inavyokwenda kiuchumi na inavyoweza kuwatumia wachezaji kama mtaji wake, jambo ambalo klabu za nyumbani zinapaswa kujifunza hili, kwani ni jambo muhimu na katika soka, suala la furaha pekee, limepitwa na wakati.

 SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic