September 12, 2016

Na Saleh Ally, Barcelona
Kabla ya mechi kati ya Deportivo Alaves dhidi ya Barcelona, juzi kulikuwa na gumzo kubwa katika Jiji la Barcelona kama kweli timu hiyo iliyopanda daraja ingeweza kuwa ya kwanza kushinda kwenye Uwanja wa Camp Nou, msimu huu.

Alaves ilikuwa imeanza ligi kwa sare dhidi ya Atletico Madrid ambayo niliishuhudia nikiwa uwanjani Vicente Calderon jijini Madrid. Mjadala ni kwamba, vipi wao Alaves wanaweza kujigamba na kuwa na uhakika wa ushindi?


Katika sehemu mbalimbali ambako kamari huchezwa, wale wahusika waliweka bei ya juu kabisa kwa wale watakaosema Alaves inaweza kushinda mechi hiyo na kuwa ya kwanza kushinda kwenye Uwanja wa Camp Nou katika msimu huu wa 2016-17 wa La Liga.

Kwa mtu ambaye angeweka euro 100 (Sh 240,000) akisema Alaves kweli itashinda, basi kama ingetokea hivyo angeweza kuibuka hadi na euro 15,420 (Sh milioni 37.1).
   






Huando Julio ni mkazi wa eneo la Santi Station jijini Barcelona ambaye aliamini Alaves itashinda na akatabiri mambo mawili ambayo yalijitokeza baadaye. Kwanza alifikiri kisaikolojia, Barcelona wangeidharau timu hiyo.

Lakini akasema kuwa sare dhidi ya Atletico Madrid, ilikuwa inaifanya Alaves kujiamini zaidi kwa kuwa mfumo wake wa safu ya ulinzi umeonekana imara sana wakati Barcelona ya Luis Enrique, tokea msimu uliopita imeonekana kutokuwa imara kuivunja ngome iliyopaki basi.

Mwisho wa mechi ilikuwa Barcelona 1-2 Alaves ambao walikuwa wageni na Julio akaibuka na kitita hicho cha fedha na mwisho kwenye mahojiano jana, amewashangaza wapenda mpira baada ya kuhadithia bibi yake mzaa baba ndiye alimshauri kuichunguza Alaves kwamba lazima itaifunga Barcelona kwa kuwa bibi huyo ni shabiki wa Atletico Madrid na aliiona timu hiyo ikicheza mechi ya kwanza ya La Liga dhidi ya timu yake na kuisumbua vilivyo.

“Baada ya maneno ya bibi, nikaona ni vema kuchunguza. Nikafuatilia kwa karibu sana mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuiangalia mechi dhidi ya Atletico ilivyokuwa.

 “Niligundua mambo mengi sana, ingawa kidogo sikuwa nakubaliana na mimi kwa asilimia mia. Mimi zaidi niliona ni sare, lakini niliamua kuweka kwamba Alaves watashinda na ukweli sikuangalia mechi kuepuka kuwehuka. Nilikuwa nikifuatilia live score kwenye simu yangu,” anasema Julio shabiki wa Espanyol alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa, jana.

Espanyol ndiyo wapinzani namba moja wa Barcelona kwenye jiji hili. Lakini bado Julio hakuamini Alaves wana ubavu wa kuwasimamisha wababe wao hao.

Alaves tayari imekuwa gumzo katika mechi tatu tu za La Liga. Kwani wakati ratiba ya La Liga ilipotoka, ilionekana ni mauaji kwenye timu hiyo, kwa vile ndani ya mechi tatu ilikuwa inatakiwa kucheza na vigogo wa La Liga.

Mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Atletico Madrid ambao ni moja ya vigogo watatu wa La Liga, ilipangwa kucheza nao nyumbani kwao Madrid. Mechi ya pili dhidi ya Athletic Bilbao, moja ya timu tatu ambazo hazijawahi kushuka daraja La Liga. Imebeba makombe kadhaa ya Ulaya na ni moja ya timu zenye mafanikio ya juu La Liga.

Mechi ya tatu, dhidi ya Barcelona. Tena Camp Nou, hakuna ambaye angeamini kwamba wanaweza kushinda, hata ingekuwa vipi. Mwisho wachezaji na kocha wa Alaves wameonekana ni mashujaa wa mechi tatu za mauaji ambayo wameyageuza kutoka kwao kwenda kwa vigogo.

Mechi ya kwanza wakiwa ugenini, ndiyo ile sare ya bao 1-1. Mechi ya pili wakiwa nyumbani, wakawakamata Bilbao kwa sare ya 0-0. Mechi ya tatu, wameitwanga Barcelona kwa mabao 2-1 ikiwa nyumbani kwake Camp Nou.

Ndani ya mechi tatu, wamekusanya ponti tano na sasa ni kati ya timu nane za La Liga ambazo zimecheza mechi tatu bila ya kupoteza hata moja, ikiwemo Real Madrid, Sevilla, Atletico Madrid na nyingine.

 Sababu hizi tatu…
Mafanikio makubwa ya Alaves ni mwaka 2001 walipofanikiwa kufika hadi fainali ya Kombe la Uefa na kufungwa kwa mabao 5-4  la mwisho likiwa ni bao la dhahabu ambalo liliwamaliza.

Maisha yake kwenye La Liga imekuwa ni kwenda na kurudi, pia si timu tajiri kwani hata uwanja wake wa Menduzirritza unachukua watazamaji 19,800 tu.

 Kocha wake mkuu, Mauricio Pellegrino si kocha mkubwa pia, lakini anasifika kwa jina la moyo wa chuma anayeongoza kikosi cha chuma kwa kuwa mfumo wa kwanza wa kikosi chake bila ya kujali una uwezo au la ni kujituma.

 Hii ni mara ya 12 inarejea kwenye La Liga tokea mwaka 1921 ilipoanzishwa lakini daraja la kwanza maarufu kama Segunda Division ndiyo nyumbani, kwani imecheza misimu 37 na kubeba ubingwa mara nne, ikiwemo msimu uliopita.

Mabingwa hao wa Segunda Division, ndiyo timu mpya na gumzo kwenye La Liga mara baada ya mechi tatu tu. Tayari timu zimeanza kuingia hofu dhidi yao.






 Lakini kocha wao anasisitiza, kamwe hawatabadilika kwa kuwa hadi wanachukua ubingwa wa Segunda Division na kupanda La Liga, walitegemea zaidi kujituma na umoja na ndiyo silaha watakayoitumia kwenye La Liga na ikiwezekana kuwapangua vigogo katika nafasi za juu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic