September 2, 2016


Na Saleh Ally
NIKISEMA niendelee kuhadithia kila ambacho nilikiona katika safari yangu ya La Liga Tour, huenda nitachukua mwezi mzima nikijaribu ‘kushea’ na wasomaji wa gazeti hili ili tujifunze au kujua namna tulivyo nyuma, tumelala huku tukiamini tuko mbali sana.


Nimeamua kufupisha na kuchambua mambo kadhaa ambayo ninaamini kila mpenda soka hasa anayependa kuona inaendelea, nijumuike naye kwa kile ambacho nilikiona, huenda ni kigeni au kipya kwangu.

Wakati nikiwa katika Jiji la Barcelona nchini Hispania, nilitembelea Uwanja wa Camp Nou unaomilikiwa na FC Barcelona ambako nilipata nafasi pia ya kushuhudia mechi ya ufunguzi wa La Liga kati ya wenyeji Barcelona dhidi ya Real Betis ambao walitandikwa mabao 6-2 huku mshambuliaji Luis Suarez akianza ligi kwa kupiga hat-trick.


Katika tembeatembea, nilipita katika duka la Barcelona ambalo huuza bidhaa mbalimbali zenye nembo ya klabu hiyo maarufu duniani.

Unaweza kusema jamaa wanauza karibu kila kitu ambacho kinaonekana kinaweza kuwekewa nembo ya klabu yao na ikawa ni biashara nzuri tu.

Hapo awali, nilibahatika kutembelea maduka ya klabu mbalimbali duniani kama Bayern Munich, Borussia Dortmund nchini Ujerumani, Galatasaray na Fenerbahce nchini Uturuki, pia nilitembelea nchi mbalimbali, lakini hawa Barcelona hawataki utani.

Kwani hata pamoja na Real Madrid kuwa matajiri zaidi yao ambako pia nilifika, lakini bado kwenye suala la uuzaji bidhaa, wanaonekana Barcelona wako makini zaidi.


Kuna vibeba ufunguo, vikombe, ‘kompasi’ za wanafunzi, miwani, saa, kofia, jezi, lakini hata kandambili.

Kuna kandambili zenye jina au nembo ya klabu. Pia wana zile zenye majina ya wachezaji na hasa Lionel Messi ndiyo zinaonekana kuwa nyingi na zinanunuliwa na watu wengi sana. Hakika niseme Barcelona wanaingiza fedha nyingi sana kwa siku kupitia biashara hiyo.

Pamoja na wanunuzi kutoka hapo Barcelona au nchini Hispania, lakini wako watu wengi hasa barani Ulaya na Asia wanakwenda kutembelea na kununua bidhaa hizo, pia wachache kutoka Afrika.

Pamoja na Barcelona kuwa maarufu na kubwa ambayo ingewezekana kabisa kupapatikiwa na mashabiki wake, eti yenyewe inafanya hadi biashara ndogo ya kandambili ambayo unaweza kuona ni ya mchuuzaji na si klabu kubwa kama hiyo.

Barcelona wanaonekana wako tofauti, kwamba wao wanajua mafanikio pia hupatikana kwa fedha kidogokidogo ambazo zikiingia kwa wingi huwa nyingi na kuongeza kipato.

Yanga na Simba, ni klabu kubwa hapa nyumbani. Hakika zina mashabiki wengi kuliko timu nyingine katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kamwe hazijawahi kuutumia vema mtaji huo.


Simba na Yanga hazifaidiki na mashabiki wake zaidi ya ‘ujiko’ wa viongozi kujiona wao ni bora kwa maneno mengi, niseme hivi, zimejaa watu wengi wasio wabunifu na wanaoamini majungu ni bora sana.

Watu wangapi ndani ya Yanga mmekuwa na maneno mengi, huku nafasi zenu zikijua wazi kwamba hamkuwahi kuushauri uongozi jambo lolote la maana?

Wangapi ndani ya Simba wanajua wamebaki kulaumu tu, hakuna ambacho wamesaidia kama kufikisha kitu wanachoamini ni bora au kukataa kununua bidhaa feki kuisaidia klabu yao au kufanya jambo linaloweza kuitwa msaada ndani ya klabu.

Barcelona wangeweza kusema wao ni maarufu sana. Kandambili huenda isingekuwa biashara ya wao kuifanya kwa kuwa ni wakubwa na wangekuwa na uwezo wa kuingiza fedha kupitia bidhaa nyingine. Wangeachana na kandambili, vikombe, vibeba ufunguo na kadhalika.

Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua umuhimu wake. Sasa kama Yanga na Simba zina mtaji wa mashabiki ambao ndiyo wanunuzi, vipi haziwatumii. Chuki na majungu baina yao ndiyo kitu bora na rahisi kukifanya unapokuwa ndani ya klabu hizo. Kweli zinashindwa hata kuuza kandambili au vibeba ufunguo tu?


Waungwana, lazima tukubali kuwa kuna shida na klabu hizo kongwe hazijawa mfano wa mafanikio, ukubwa wake hauna faida kwa klabu hizo na wanachama na mashabiki wake. Ni tatizo kubwa kwa kuwa ndiyo wanaochangia kuziangusha na wengi wao wakiwa ni maslahi binafsi au fuata mkumbo.


Muda unakwenda, tujipime, tutafakari na kuangalia ulipo ukweli halisi. Yanga na Simba, zinauchezea sana mtaji zilionao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic