September 10, 2016

Licha ya Simba kuonekana kuwa ipo vizuri na ina mwenendo mzuri katika Ligi Kuu Bara msimu huu, kocha wa timu hiyo, Joseph Omog amesema kama wachezaji wake wasipokuwa makini basi Yanga itakuwa bingwa tena.

Omog, raia wa Cameroon, asiyependa sifa za kijinga, ameiongoza Simba katika mechi tatu za ligi hiyo ambapo ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC, ikatoka suluhu na JKT Ruvu kisha ikaifunga Ruvu Shooting mabao 2-1.


Simba ambayo kesho Jumapili itacheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba sawa na timu zilizo juu yake ambazo ni Azam FC na Mbeya City lakini imezidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.


Katika mahojiano maalum na Championi Jumamosi, Omog aliyeipa ubingwa Azam bila kufungwa msimu wa 2012/13, alisema kuna mambo makuu matatu ambayo yataifanya Simba ipotee na kuifanya Yanga itwae ubingwa msimu huu.


Omog aliyataja mambo hayo kuwa ni ubinafsi wa wachezaji, ukosefu wa umakini na uzalendo.
“Tunaonekana kama tupo vizuri na tumechanganya katika ligi, ukweli ni kwamba tusipokuwa makini katika mambo haya matatu ni lazima Yanga itwae ubingwa tena,” alisema Omog anayesaidiwa na Jackson Mayanja, raia wa Uganda.

UMAKINI
“Tazama katika mechi na Ruvu Shooting (iliyochezwa Jumatano wiki hii), tulikuwa tufunge hata mabao matano, lakini tatizo ni umakini mdogo.
“Karibu wachezaji wote, hasa safu ya mbele hawapo makini kwani tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi za mabao lakini tunaishia kutumia chache mno,” alisema Omog.

UBINAFSI
“Pia nimegundua kuna ubinafsi. Simba ni timu moja, tunapigania kitu kimoja, tukipata ushindi siyo wangu wala mchezaji fulani bali ni ushindi wa timu kwa ujumla, tukifeli pia tunakuwa tumefeli wote.
“Kuna baadhi ya wachezaji wao wanaangalia mafanikio yao binafsi, kila mmoja anataka afunge hata kama hayupo kwenye nafasi ya kufunga badala ya kumtengenezea mazingira mwenzake.
“Hili ni tatizo na ni lazima tulitatue mapema kabla halijawaathiri sana,” alisema Omog.


  UZALENDO
Hapa Omog anamtolea mfano beki wa kati Juuko Murshid ambaye hadi jana Ijumaa alikuwa hajarejea kikosini kutoka Uganda alipokwenda kuitumikia timu yake ya Taifa, The Cranes.
 “Mfano unaweza kujiuliza Juuko mpaka sasa anafanya nini kwao? Kama ni matatizo si angetoa taarifa lakini hakuna taarifa yoyote juu ya kuchelewa kwake. 


“Kwangu ni utovu wa nidhamu na akirejea lazima achukuliwe adhabu, huyu anakosa uzalendo kwa timu yake na kama unatafuta ubingwa halafu ukawa na watu wenye tabia kama hizi ni ngumu kufanikiwa,” alisema Omog. 


Omog alisema atajitahidi kurekebisha hali hiyo mapema kabla ya kukutana na Yanga Oktoba Mosi mwaka huu kwani anaamini wachezaji wake watabadilika na kupambana uwanjani.


“Nitajitahidi kurekebisha haya matatizo matatu ili tusitoe nafasi kwa Yanga na Azam kwani wanaweza kutwaa ubingwa,” alisisitiza Omog.


Katika mazoezi ya timu hiyo jana jioni kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam, Omog alionekana akiwaelekeza kwa kina washambuliaji wake Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib, Fredric Blagnon na Ame Ally ‘Zungu’ kuhusu umakini katika kufunga.


Akizungumzia mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa, Omog alisema: “Lengo letu ni lilelile, kuhakikisha tunapigana kila mechi japokuwa  najua haiwezi kuwa rahisi namna hiyo lakini tutapigana kadiri ya uwezo wetu ili tushinde.”


Naye Kocha Salum Mayanga wa Mtibwa alisema: “Mechi hii ni ngumu kwani kuna wachezaji wametoka Mtibwa na wanatujua lakini tutapambana kupata ushindi au pointi moja.”





SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic