September 19, 2016

Zikiwa bado siku chache miamba ya soka hapa nchini, Simba Yanga ikutane uwanjani kuwania pointi tatu za ligi kuu, hofu kubwa imeibuka ndani ya Klabu ya Yanga.

Hofu hiyo imesababishwa na kiwango cha juu alichoonyesha uwanjani mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib wakati alipokuwa akiitumikia klabu hiyo dhidi ya Azam FC juzi Jumamosi katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.


Katika mchezo huo uliomalizika kwa Simba kushinda bao 1-0, Ajib alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Azam kwani kila wakati alikuwa akiwapindua mabeki hao kama alivyotaka na kuingia ndani ya eneo la hatari kwa kasi ya ajabu lakini kipa wa timu hiyo, Aishi Manula alikuwa makini kupangua mashuti yake.
Hali hiyo, iliwatiwa hofu kubwa baadhi ya viongozi wa Yanga waliokuwa uwanjani hapo wakishuhudia mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.


Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga alizungumza na Championi Jumatatu uwanjani hapo lakini kwa masharti ya kutotajwa jina lake gazetini kwa madai kuwa akionekana anamsifia Ajib, wenzake wanaweza kumuona msaliti.


Alisema endapo benchi la ufundi la Yanga ambalo linaongozwa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm lisipokuwa makini na kumuandalia mikakati thabiti mchezaji huyo, basi ataisumbua sana safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Oktoba Mosi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


“Tuache unafiki Simba ya msimu huu ipo vizuri, tusipokuwa makini safari hii mambo yanaweza kuwa mabaya kwa upande wetu  siku hiyo tutakapokutana uwanjani Oktoba Mosi, kwani ina kikosi kipana sana chenye wachezaji wazuri.


“Lakini pia siku hiyo tunatakiwa kumchunga sana Ajib, kwani Ajib wa sasa siyo yule wa msimu uliopita, kiwango chake kimeongezeka sana, anapambana uwanjani, akishika mpira analitafuta eneo la hatari kwa kasi ya ajabu bila kuhofia mabeki.


“Kama kocha siku hiyo atawapanga mabeki wetu ambao hawana kasi, mtoto huyo atatuumiza, kama itawezekana siku hiyo waanze Kelvin Yondani na Andrew Vincent ‘Dante’ ambao kwa pamoja wana kasi na ni wazuri kwa kukaba,” alisema kiongozi huyo na kusisitiza kutotajwa jina lake.


Hata hivyo, alipotafutwa Pluijm ili aweze kuzungumzia suala hilo alisema: “Siwezi kusema chochote juu ya jambo hilo ila ninachoweza kuzungumzia ni kuhusiana na mikakati yetu ya kuhakikisha tunaondoka na pointi zote huku Kanda ya Ziwa.”


Kwa upande wake Ajib alisema: “Ni kweli nimebadilika ila na hiyo yote ni kwa sababu msimu huu nataka kuisaidia timu yangu ili iweze kuwa bingwa wa ligi kuu, hivyo nitapambana kila mechi kama nitapata nafasi ya kucheza.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic