September 30, 2016



Na Saleh Ally
KWA kuwa mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba ni kesho Jumamosi, kwa wapenda soka nchini hakuna anayeweza kukataa kwamba joto limepanda kwa kuwa presha ni kubwa.

Kila sehemu wanaamini wana nafasi ya kushinda. Simba wanajiamini sana lakini Yanga wanajua wana kikosi kizuri, nao wanaamini watashinda.

Mjadala mkubwa ni zaidi kwa mashabiki ambao huchagiza mchezo unapokuwa umekaribia. Kawaida mashabiki huwa na mawazo au mwonekano wa kujiamini zaidi kuliko hata makocha au wachezaji wenyewe.

Mechi ya watani ni mechi kubwa kwa maana ya soka nchini. Inawakutanisha vigogo ambao ndiyo wenye mashabiki wengi kuliko mwingine. Si vibaya kusema, itakuwa ni siku ya wakubwa.

Wakati ndani ya Simba na Yanga kila upande ukiamini una nafasi ya kushinda, ukweli ni kwamba mashabiki watakaokwenda uwanjani watakuwa wanataka kuona burudani ya mchezo wa soka.

Wanataka kuona pasi bora, pasi zinazofika, pasi za vipimo. Mashabiki hao watalipa kwa kuwa wangependa kuona mabao bora na mipango ya uhakika. Kila mmoja akiiombea timu yake iibuke na ushindi.

Hata kama kutakuwa na ushindi, soka lisiwe na kuvutia. Bado huwa ushindi wa maswali au ushangiliaji wake unakuwa ni wenye maswali au usiokuwa na furaha ya asilimia mia kutokana na walichokiona.

Nimeamua kuandika kuhusiana na suala la umakini na wachezaji kujitambua zaidi kwamba kesho watakuwa wanafanya nini na wako wapi baada ya kujifunza mambo kadhaa kwenye mechi za watani.

Mechi ya Yanga na Simba imekuwa na presha kubwa, hali ambayo huwafanya wachezaji wengi kutojiamini na huenda kucheza chini ya kiwango au kuwa na mbinu nyingi ambazo si sahihi ili washinde.

Mbinu ambazo wamekuwa wakizitumia, mfano kupigana viwiko, kuumizana au kuzozana bila ya sababu za msingi, haitakuwa sawasawa hata kidogo, mashabiki wangependa zaidi kuona mpira.

Mchezaji anayemvizia mchezaji mwenzake amuumiza, hakika halitakuwa jambo ambalo mashabiki wamelipa kiwango kuingia uwanjani kwenda kushuhudia, badala yake iwe ni soka tu.

Kwa wachezaji ambao wamekuwa wakipoteza muda, mfano timu moja inakuwa imefanikiwa kupata bao, basi kuanzia hapo, hata kama ni dakika ya 36, yaani kipindi cha kwanza, eti inaanza kupoteza muda.

Kupoteza muda kuanzia dakika ya 36 ni kuwanyima haki mashabiki waliolipa fedha zao na kujigharimia usafiri hadi kufika hapo. Haki yao ni kufanya kila linalowezekana waone soka safi na lenye mvuto.

Wachezaji ni sehemu ya masoko katika mchezo wa soka. Wanaweza kuwa watu wazuri wa kuvuta watu wengi zaidi, kuwaridhisha na kuwafanya waendelee kuwa upande wa klabu zao kwa kuwa wataziamini zaidi lakini hii ni hadi wacheze mpira.

Kila mchezaji ajiamini kwamba anaweza kucheza vizuri na burudani ya soka ianze dakika ya kwanza hadi 90 kwa kuwa walio jukwaani wamelipa.

Kingine, suala la kujiangusha bila sababu za msingi, iwe kwa mchezaji kusingizia ameumia au kipa kupoteza muda kwa kujiangusha, si sahihi hata kidogo. Ili kuonyesha soka nchini limekua, lazima kuanzia nanyi ambao ndiyo timu kongwe.

Kama soka la kuvutia litachezwa katika mechi kati ya Stand United na Mwadui FC, halafu Yanga dhidi ya Simba ikawa madudu, basi itakuwa ni miujiza kusifia mabadiliko ya mchezo huo.

Hakuna ujanja, wachezaji wa Yanga na Simba, lazima Jumamosi waonyeshe ni watu wenye mabadiliko na kuachana na tabia za ‘mchangani’ kuzipeleka katika mechi kubwa kabisa.

Kila kocha angefurahia kuona kikosi chake kinashinda. Hivyo mwamuzi achezeshe ‘fea’ na wachezaji waonyeshe uwezo wao kwa kutoa burudani safi kwa Wanayanga na Simba watakaojitokeza kuwaunga mkono. Hakuna anayefunga safari kwenda uwanjani kuona wachezaji wanavyoanguka au wanavyopoteza muda!


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic