September 16, 2016

Na Seleman Matola
Wakati naanza kuichezea Simba mwaka 2,000, niliikuta hali ya timu hiyo haikuwa nzuri kiuwezo, ilikuwa imepita miaka minne haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Simba ilitwaa ubingwa wa Bara mwaka 1995, baada ya hapo ufalme ukawa ni wa Yanga iliyotwaa ubingwa mara tatu mfululizo, lilikuwa pigo kubwa kwa Wanasimba.

Kila tulipokatiza kicheko kilikuwa ni kwa Wanayanga tu, ilituuma sana, wanaofuatilia soka kwa ukaribu hasa upinzani wa Simba na Yanga wanaweza kunielewa vizuri.

Mwaka 2001 uongozi wa Simba ukamwajiri kocha kutoka Kenya, James Aggrey Siang’a ambaye hakuwa na jina kubwa hapa nchini.

Siang’a alikuta Wanasimba wamekata tamaa kwa kuwa baada ya Yanga kutwaa taji mara tatu kilichofuata ni Mtibwa Sugar kutwaa mara mbili mfululizo, hivyo ikawa imepita miaka mitano Simba haijatwaa ubingwa.

Taratibu Siang’a akaanza kazi na kupewa ushirikiano na viongozi wa Simba. Katika msimu wake wa kwanza tu akaipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ilionekana kama maajabu kwa jinsi ambavyo Simba walivyokuwa wakiusubiri ubingwa huo.

Kikosi cha Simba kilichoiondoa Zamalek mwaka 2003 chini ya Siang’a, picha hii ilikuwa kati ya mechi iliyowaondoa Waarabu hao, kutoka kushoto waliosimama ni Emmanuel Gabriel, Said Sued, Yusuph Macho, Alex Massawe, Victor Costa, Selemani Matola. Kutoka kushoto walioinama; Ramadhani Wasso, Ulimboka Mwakingwe, Juma Kaseja, Athuman Machupa na Boniface Pawasa.

Kabla ya mechi ya Zamalek vs Simba kuanza jijini Cairo mwaka 2003.

Huo ulikuwa mwanzo tu, Siang’a akaendela kufanya vizuri zaidi na zaidi, sikumbuki mataji mangapi aliipa Simba lakini yalikuwa ni mengi na kwa ufupi heshima ya Simba ikarejea na kuwa juu zaidi ya ilivyokuwa awali.

Kizuri zaidi Siang’a aliiwezesha Simba kufuzu hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2003 kwa kuiondoa Zamalek ya Misri ambao ndiyo waliokuwa mabingwa watetezi.

Siang’a ambaye alifariki Ijumaa iliyopita Septemba 9, 2016 akiwa Bungoma nchini Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu, ameacha historia kubwa na kuna mengi ya kumzungumza.

Nimeamua kushea na wewe msomaji mambo kadhaa ya kukumbukwa kuhusu marehemu Siang’a.


James Siang'a

Wasifu wa Siang'a kwa ufupi
Aliwahi kucheza katika timu za Gor Mahia, Luo Union na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars akiwa kipa, mbali na kuifundisha Simba, pia aliwahi kuwa mwalimu wa Moro United, Express ya Uganda na Gor Mahia ya Kenya.

Siang’a aliidakia Kenya katika Kombe la Mataifa ya Afrika 1972, alikuwa kocha wa Harambee Stars mwaka 1999 na 2000.

Alitengeneza timu kuwa familia
Akiwa Simba alikuwa ni zaidi ya kocha kwa wachezaji, alikuwa kama baba yetu, alitulea vizuri na hakutaka makundi ndani ya timu, uwepo wake ulisababisha vijana wengi kuwa na kiwango bora na kutengeneza timu ambayo baadaye ilikuwa tishio.

Nakumbuka katika kikosi chake baadhi ya wachezaji ni mimi Matola, Victor Costa, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Gabriel, Lubigisa Madata, Primus Kasonzo, Christopher Alex, Said Swedi, Ramadhani Wasso, Boniface Pawasa, Shekhan Rashid na Athumani Machuppa.

Unajua tena mambo ya vijana, kuna wakati alikuwa akitatua matatizo ya wachezaji ambayo yapo ndani ya uwezo wake bila kuhusisha viongozi.

Mfano ilipotokea mchezaji amekiuka kanuni za klabu au kuonyesha utovu wa nidhamu, alimuita na kuzungumza naye kisha kuyamaliza yeye mwenyewe wakati angekuwa kocha mwingine lazima aripoti kwa viongozi na unavyowajua viongozi wa Bongo mambo yanakuwa makubwa kwa kitu kidogo tu.

Kuna wachezaji walikuwa wakitoroka kambini kwenda kustarehe, alipogundua aliwaita na kuwakanya pasipo kuhusisha viongozi.

Kikosi cha Simba kilichokuwa chini ya Siang’a, kutoka kushoto waliosimama ni Joseph Kaniki, Madaraka Suleiman, Geoffrey Mhando, Selemani Matola, Boniface Pawasa na Shekhan Rashid. Waliochuchumaa wa kwanza kushoto ni Nteze John ambaye amekatwa, Steven Mapunda ‘Garrincha’, Mwameja Mohammed, Qureish Ufunguo na Sekelo Barnabas

Avaa boksa tu baada ya kufungwa
Kuna tukio nalikumbuka mpaka leo, kuna mechi tulicheza dhidi ya Nkana FC ya Zambia, tulikuwa na kikosi kizuri sana na matumaini ya kushinda yalikuwa makubwa, lakini katika mchezo huo tukafungwa mabao 3-0.

Siang’a hakuamini kilichotokea, wakati akitoka uwanjani alikuwa na hasira sana, hakupenda kufungwa kabisa, waandishi wakamfuata wakiwa wamemzunguka, hakutaka kuzungumza, wao wakaendelea kumfuata, alipoona wanamsumbua zaidi, akaipiga kamera moja kwa hasira na akataka kumvaa yule mpigapicha, watu wakamuwahi wakamzuia.

Tulipofika kambini akaingia chumbani kwake na kujifungia, baadaye akaniita mimi kwa kuwa nilikuwa nahodha, nikaenda chumbani kwake, nilipoingia nikamkuta amelala kitandani akiwa na boksa tu, akaanza kuniuliza sababu za kufungwa 3-0.

Tukazungumza lakini akili yake haikuwa sawa, tulikaa siku mbili kule Zambia, alishindwa kula vizuri kabisa mpaka tulipoondoka na kurejea Dar, hiyo ilikuwa ni katika Klabu Bingwa Afrika.






ITAENDELEA...

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic