September 30, 2016



Huku kikosi cha Yanga, kesho Jumamosi kikitarajia kushuka uwanjani kupambana na Simba katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, matajiri wa timu hiyo jana waliivamia kambi ya kikosi hicho iliyopo kisiwani Pemba.

Matajiri hao ambao inadaiwa kuwa walikuwa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mhandisi Paul Malume, walitinga kisiwani humo kwa ndege ya kukodi na kisha kufanya kikao na wachezaji wa timu hiyo.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa lengo kubwa la matajiri hao kuwafuata wachezaji wa timu hiyo kisiwani Pemba wakati bado siku moja tu washuke uwanjani kupambana na Simba, ni kuwajenga kisaikolojia ili waweze kuibuka na ushindi hiyo kesho.

“Ukiachana na hilo, pia wachezaji hao wameahidiwa kupewa shilingi milioni 20 na matajiri hao kama wataibuka na ushindi siku hiyo.

“Lakini pia baada ya wachezaji wetu kurejea Dar es Salaam kesho (leo), watakutana na mwenyekiti wetu, Yusuf Manji katika kikao maalumu ambacho bado sijajua kitafanyika wapi kwani naye atakuwa na machache ya kuzungumza nao kwa ajili ya mchezo huo.

“Kutokana na hali hiyo napenda kusema kuwa mambo sasa yamekaa sawa, Simba wajiandae kwa kipigo siku hiyo,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Alipotafutwa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, ambaye yupo na kikosi hicho kisiwani Pemba ili kuthibitisha juu ya ugeni huo kutua kambini hapo, hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.

Tulupozungumza na mmoja wa wachezaji wa timu hiyo ambaye aliomba kutotajwa jina lake kutokana na uongozi wao kuwazuia kuzungumza na waandishi wa habari, alisema:

“Ni kweli kabisa leo tuna wageni walikuja kututembelea na tumefanya nao kikao na wametuahidi zawadi nzuri kama tutaifunga Simba, ila siwezi kukwambia ni shilingi ngapi.”



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic