September 17, 2016

Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema kwa ratiba waliyonayo katika Ligi Kuu Bara, inawapa urahisi wa kutetea ubingwa wao kwani ni rafiki kwao.

Pluijm ametamba kupambana muda wote kuhakikisha timu yake inatetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na wala hana hofu na Simba na Azam FC.

Simba na Azam zote zina pointi 10 katika ligi hiyo na leo zinakutana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, lakini Pluijm raia wa Uholanzi, amesema: “Hao hawana jeuri ya kuchukua ubingwa.”

Kauli hiyo ya Pluijm ni kama ya kupiga mkwara kwani hadi sasa Simba na Azam zote zina pointi 10 katika mechi nne zilizocheza huku zikilingana mabao ya kufunga na kufungwa. Wote wana mabao saba na wamefungwa mabao mawili.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Yanga inaanza na mechi za ugenini saba wakati Simba inazo nne tu.

Katika mzunguko huu wa kwanza, Yanga ugenini inacheza na Ndanda FC (tayari wamesuluhu), Mwadui FC (leo), Stand United, Toto African, Kagera Sugar, Mbeya City na Prisons. Simba itacheza na Mbeya City, Prisons, Mwadui na Stand United.

Hii inamaana kwamba, mzunguko wa pili Simba itacheza mechi nyingi za ugenini kuliko Yanga ambayo itakuwa nyumbani jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Pluijm alisema: “Nafurahia ratiba ya ligi kuu ambayo naamini itanirahisishia kutetea taji la ligi kuu kwani tunaanza na mechi nyingi za ugenini tena zile za mikoani.
“Unajua changamoto kubwa ya mechi za mikoani ni ubovu wa viwanja, hivyo napata matumaini makubwa kwenye mzunguko wa pili nitapata matokeo mazuri na njia ya ubingwa itakuwa rahisi.”

Pluijm, raia wa Uholanzi, alisema anataka kuweka rekodi nzuri kwenye msimu huu wa ligi kuu kwa kutwaa ubingwa mara ya tatu mfululizo na anaamini hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chake.

“Ninapata ujasiri huo, kutokana na kuanza ligi kuu kwa kucheza mechi tatu mfululizo mikoani ambako huko ndiyo kugumu kwetu, hivyo tukifanya vizuri tutakuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

“Nina uzoefu mkubwa wa ligi kuu ya hapa nchini, mechi za mzunguko wa pili wa ligi kuu ni ngumu kutokana na kila timu kupania, nyingine zikipambana kubaki nyingine zikitaka ubingwa.

“Wapinzani wetu Simba na Azam wenyewe wameanza kwa kucheza mechi zao nyumbani na kupata matokeo mazuri, hivyo sina hofu nazo kabisa na wao watakuja huku mikoani, halafu tuone kama wataendelea kukaa kileleni,” alisema Pluijm kutoka Shinyanga.

Yanga ambayo leo inacheza na Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi tatu.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic