October 19, 2016



Na Saleh Ally
SOKA ni mchezo wa kiume hasa, ingawa unaweza kuchezwa na wanawake pia. Ni mchezo ambao kama hauna nguvu, hauwezi kuwa mchezaji wa ushindani.

Akili ni muongozo kwenye mchezo wa soka, lakini lazima kuwe na nguvu na ndiyo maana mazoezi ya nguvu ni mengi kuliko yale yanayohusiana na akili.

Mazoezi ya akili ni ujuzi wa kocha, anapofikiria kuwajenga wachezaji kiufundi zaidi halafu wakafanya mazoezi ya vitendo ili kuhifadhi mbinu au maelekezo wanayotakiwa kufanya.

Lakini asilimia 70 hadi 85, mwili utatakiwa kuwa fiti, halafu nyongeza inayofuatia ni ufiti wa kichwani kwa maana ya akili.

Kama utakuwa na akili asilimia 85 kwa maana ya ubora na nguvu 15, hakika hautakuwa na nafasi kubwa ya kuitwa mwanasoka bora. Bado nguvu ni jambo muhimu sana.

Pamoja na hivyo, kucheza kwa nguvu hakuwezi kuwa dhambi lakini katika soka kutimiza suala la soka ni burudani, kazi na kadhalika huku mwisho ukiishia si uadui, lazima kwa kila mchezaji kuhakikisha anahitimisha na tahadhari.
Kama utasikia kuna mchezaji anajiandaa au kucheza huku akiwa amelenga kuwaumiza wenzake, huyu si muungwana na inawezekana pia si anayejiamini kwa uhakika.

Wengi wasio na uwezo wa jambo, mfano ukimuona bosi wako ni mkali tu kila siku, ujue kuna kitu anaficha na huenda uwezo wake ni mdogo na ukali anatumia kama kichaka cha kuficha udhaifu wake.

Siwezi kusema beki Aggrey Morris wa Azam FC ana uwezo mdogo na sasa vile vitendo vya kuwaumiza wenzake kwa makusudi au ‘bahati mbaya’ kama inavyoelezwa vinaweza kuepukika.

Ukiangalia vizuri, vitendo kadhaa alivyofanya havionyeshi kama kuna asilimia kubwa ya bahati mbaya, badala yake unaweza kuona kuna asilimia kubwa ya kukusudia.

Morris anaweza kuwa na nafasi kubwa ya kujitetea, kwamba yeye ni beki, lazima acheze kwa nguvu na unapokuwa mlinzi wa katikati, basi lazima ucheze kwa nguvu kweli. Lakini bado hiyo haitaidhinisha kuumiza wenzako na haiwezekani ikawa wewe tu.

Beki huyo, aliwahi kumuumiza Emmanuel Okwi, alimpiga kwa makusudi na picha za runinga zikaonyesha wazi akimpiga. Okwi akapelekwa hospitali akitolewa uwanjani moja kwa moja. Alizimia wakati anatolewa na wapo waliolaani hilo.

Morris alikuwa majeruhi, baada ya kurudi kama wiki moja iliyopita, hivi karibuni amemuumiza Abasrim Chidiebere kwa kumvunja taya. Tunaweza kuamini na hiyo nayo ilikuwa ni bahati mbaya. Tena tumpongeze Morris na wachezaji na viongozi wengine wa Azam FC kufika kumjulia hali Mnigeria huyo. Lakini msisitizo unabaki palepale, kwamba Morris anaweza kuwa mchezaji anayeepuka hiyo hali.

Wakati tunaondoka kwenye hilo, kama wewe unataka kujiridhisha, basi fuatilia mechi ya Azam FC dhidi ya Yanga, utaona namna Morris alivyofanikiwa kucheza rafu ambazo zinaashiria kuumiza.

Alifanya hivyo kwa Simon Msuva, alifanya hivyo kwa Obrey Chirwa ambaye alimkanyaga begani huku akijua wazi mpira aliokuwa akiufuata asingeweza kuufikia kwa mguu.

Hivi, katika suala la kuwaumiza wachezaji wa timu pinzani ni Morris tu ndiye anayekosea na kuwaumiza wenzake? Vipi awe mtu mwenye lengo la kuumiza badala ya kufanya kazi yake kwa ufanisi.
Unaweza kujiuliza ni maji ya jioni, yaani anakwisha kimpira, unaweza kujiuliza kwamba ana mawazo ya jambo fulani halimfurahishi, hivyo kawa na hasira ‘gunia’ ambazo anataka kuzimalizia kwa wengine?

Lakini unaweza kujiuliza, vipi Morris hana huruma kwa wachezaji wenzake kama anajua ubaya wa kukaa nje kwa mchezaji aliye majeruhi.

Lazima anajua, soka kwa wachezaji ni kazi na wengine wanautegemea kujiendesha na kuendesha familia zao. Sasa kama naye Morris anaishi hivyo, vipi hajifikirii kwamba anachofanya si sahihi.

Beki bora, anaweza kuwa ni yule anayezuia zaidi au kuisaidia timu yake kutofungwa kwa ubora wa kuokoa au kuvuruga mipango ya wapinzani lakini si kwa sifa nyingi za kuwaumiza wengine.

Niliona hata Erasto Nyoni alifanya hivyo, alicheza faulo nyingi za kijinga ambazo zinalenga zaidi kuumiza kuliko kuzuia. Hakika haiwezi kuwa sawa na hii si sahihi.

Tunaweza kuona aibu, au haya kuwaeleza ukweli kwa kuwaacha wajifiche kwenye kichaka cha wao ni mabeki au walinzi wanaotakiwa kufanya kazi yao. Lakini ni vigumu kwa mtu mwenye akili timamu kuona wanavyocheza halafu useme, mfano Morris ana lengo la kulinda.

Kama atakuwa na lengo la kutisha zaidi ili alinde, basi kuna shida kubwa ambayo inaweza kuniaminisha kwamba ameshuka kiwango au umri unamfanya ashuke na yeye hataki kuamini, hivyo anatumia njia ya kutisha kama yule bosi asiye na uwezo.

Ninaamini baada ya mechi, watu hurudi na kuzungumza kama kawaida kwa kuwa hakuna tena presha. Lakini hakuna anayeweza kukubali kuondoa presha huku akiwa na jeraha la kuumizwa kwa makusudi aseme anaondoa presha au kurudisha urafiki.


Ninaamini Morris anaweza kubadilika. Lakini kama ataendelea hivi; siku si nyingi ataingia kwenye majuto ya nafsi na haya niliyoyaandika, yatabaki kama kisu kwenye kumbukumbu yake ya baadaye.

1 COMMENTS:

  1. Halafu utakuta wale commentators wao pale wanamtetea...ukiwafatilia vizuri utagundua wanatangaza mechi kwa mahaba ya AZAM FC.
    AZAM TV nao WABADILIKE

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic