October 10, 2016

MAVUGO
Mshambuliaji Laudit  Mavugo amepewa mechi nane tu kuhakikisha anaongeza ubora wake wa kushirikiana vizuri na Ibrahim Ajibu na washambuliaji wengine wa Simba.

Licha ya timu hiyo kucheza mechi saba mpaka sasa bila ya kufungwa na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara lakini benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mcameroon, Joseph Omog limeeleza kinagaubaga kuwa baada ya mechi hizo wanaamini safu yao ya ushambuliaji itatisha zaidi.

Kocha msaidizi wa Wekundu hao, Mganda, Jackson Mayanja amesema kuwa kila mchezaji sasa ameingia kwenye mfumo na kutengeneza maelewano mazuri isipokuwa wachezaji watatu; Mavugo, Muivorycoast, Fredric Blagnon na Ibrahim Ajibu.

“Kila kitu kimekaa sawa kwenye timu isipokuwa hawa watatu, yaani kama ‘combination’ yao ingeelewana mapema basi kazi ya msimu huu ingekuwa rahisi. Kinachokwamisha ni kuelewana kwa safu ya ushambuliaji kati ya Ajibu, Mavugo na Blagnon.

“Si lazima wote watatu waanze pamoja lakini tunachokilenga hapa kwamba wakianza wawili kati yao wafanye vizuri na akitoka mwingine akiingia mwingine iwe hivyohivyo, hili linamlenga mpaka Ame Ali siyo kina Mavugo pekee.

“Utendaji wao unahitaji kuboreshwa zaidi na hili ndiyo tunalolifanyia kila siku kwa sasa, tunataka mpaka mwisho wa mzunguko wa kwanza uliobakisha mechi nane hili suala liwe limekwisha, tukianza mzunguko wa pili, tuwe fiti kila mahali, tunajaribu kuwaelekeza lakini na wao pia lazima wafanye juhudi,” alisema Mayanja.

Kuhusiana na utendaji kazi wa Shiza Kichuya kikosini hapo, Mayanja alisema: “Kichuya anafanya vizuri, anafunga na anapambana, yeye amezoea mazingira mapema kwa kuwa yupo kwenye hii ligi tangu msimu uliopita lakini Mavugo na Blagnon ni wageni na wanahitaji kuongeza bidii kuzoea mazingira mapema sana.

“Bado tunahitaji mabao mengi ya kufunga, kwa hiyo ukichanganya haya ya Kichuya na yatakayopatikana kutoka kwa kina Mavugo, tutakuwa mbali.”

Simba imefunga mabao 13, katika hayo safu ya kina Mavugo imefunga sita tu; Mavugo matatu, Ajibu mawili na Blagnon moja. Yaliyobaki matano yamefungwa na Kichuya na mawili yamefungwa na Jamal Mnyate.

Hata hivyo, kwa muda sasa Mavugo amekuwa gumzo kutokana na kushindwa kutumia nafasi au kuelewana vyema na wenzake wanapopata nafasi za kufunga, licha ya kufunga katika mechi tatu mfululizo za awali, sasa ana rekodi mpya ya kutofunga mechi nne mfululizo za mwisho za Simba.

Katika michezo hiyo minne, Mavugo alifanyiwa mabadiliko katika michezo mitatu mfululizo, mechi waliyocheza na Azam, alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Blagnon, akafanyiwa mabadiliko pia walipovaana na Majimaji na kuingia Mohammed Ibrahim ‘Cabaye’, mechi ya mwisho ilikuwa dhidi ya Yanga alipompisha tena Blagnon.

SOURCE: CHAMPIONI 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic