October 12, 2016

MWINYI

Akiwa amebakiza miezi saba ili amalize mkataba wake na Yanga, beki wa pembeni wa Yanga, Haji Mwinyi, amesema yupo tayari kujiunga na Simba.

Beki huyo, alitua kuichezea timu hiyo msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara akitokea kwenye kikosi cha KMKM cha Zanzibar na sasa amekuwa ndiyo mhimili wa safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Mwinyi, kwenye mechi iliyopita ya watani wa jadi dhidi ya Simba, aliweza kumdhibiti kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya kutokana na aina yake ya uchezaji wa kasi, pamoja na kwamba mshambuliaji huyo aliifungia timu yake bao la kusawazisha kwa kona ya moja kwa moja kwenye matokeo ya 1-1.

Mwinyi amesema wakati mkataba wake ukielekea ukingoni, ametoa nafasi kwa timu itakayomhitaji kuanza kufanya naye mazungumzo wakiwemo wapinzani wao Simba.

Mwinyi alisema, pia anatoa nafasi kwa timu yake ya Yanga anayoitumikia kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kutumikia hapo ambapo alitwaa ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la FA msimu uliopita.

Aliongeza na kusisitiza kuwa, kikubwa anachokiangalia yeye ni maslahi pekee yatakayomshawishi kusaini mkataba wa kuichezea timu itakayoonyesha nia kubwa ya kumsajili.

“Mimi mkataba wangu unatarajiwa kumalizika rasmi Aprili, mwakani, hivyo kuanzia hapo ninaruhusiwa kusaini mkataba kwenye timu yoyote itakayonihitaji, ikiwemo timu yangu ya Yanga.

“Kama unavyojua, mimi ninaendesha maisha yangu kwa kupitia soka, hivyo ili niishi kwa mafanikio, ni vema nikalipwa mshahara mzuri na dau zuri la usajili na siyo kitu kingine.

“Mimi siogopi changamoto yoyote nitakayoikuta kwenye timu nitakayoenda, kwa mfano wakati ninakuja Yanga, nilipewa vitisho vingi, lakini nilipambana, hivyo basi hata kama ikitokea Simba wakazungumza nami na kuonyesha nia nitakwenda.


“Nikienda Simba nitapambana na kupata nafasi ya kucheza mbele ya Tshabalala (Mohammed Hussein) wala sina hofu,” alisema Mwinyi.

SOURCE; CHAMPIONI.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic