October 8, 2016



Na Saleh Ally
UNAWEZA kuona namna mchezaji kama Cristiano Ronaldo ambaye anapambana kila inavyowezekana anavyochanganyikiwa akiwa na hamu kubwa ya kutaka kufanya vizuri.

Mambo si mazuri kwa Ronaldo ambaye ndiye mchezaji bora zaidi kwa kipindi hiki kutokana na mafanikio makubwa anayopata, ukijumlisha yale ya kuisaidia Ureno kubeba ubingwa wa Ulaya.

Ingawa aliumia katika mechi ya mwisho na kutolewa, lakini Ronaldo akabaki kuwa shujaa wa Ureno katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Ufaransa mwaka huu.

Baada ya hapo, akapewa mapumziko nje ya kikosi cha Real Madrid kwa kuwa alitakiwa pia kujiuguza kwa kuwa alikuwa majeruhi. Baada ya hapo alirejea kikosini Madrid na kufanikiwa kuanza vizuri kwa kufunga katika mechi ya kwanza tu.


Ikaonekana kama amerejea baada ya maandalizi ya kutosha katika eneo la Ciudad Madrid ambako kuna viwanja vya mazoezi vya klabu hiyo.

Mechi ya kwanza dhidi ya Osasuna, alifunga bao lakini akatolewa katika dakika ya 65, Madrid ikiibuka na ushindi wa mabao 6-2. Mechi iliyofuatia dhidi ya Sporting Lisbon, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Madrid ikashinda 2-1 na yeye akifunga bao moja.

Baada ya mechi hiyo, Madrid ilicheza mechi nne mfululizo, zote zikiwa sare na Ronaldo akishindwa kuonyesha kiwango bora au kuwa msaada katika kikosi chake.

Sare ya bao 1-1 dhidi ya Manyambizi wa Villarreal, akicheza dakika 90. Ikafuatia sare ya 2-2 dhidi ya Las Palmas, Kocha Zinedine Zidane akamtoa katika dakika ya 71 akionekana wazi Ronaldo hakupenda kwa kuporomosha maneno rundo.

Wengi waliona kutolewa kwake, kulisababisha sare. Mechi mbili zilizofuata Ronaldo akacheza kwa dakika 90 zote na pia ikawa sare ya 2-2 dhidi ya Borussia Dortmund ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya na waliporudi kwenye La Liga wakatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Eibar.

Zidane akaamua kukubali kwamba kweli sasa hali ni mbaya, mwendo wao si sahihi na wanahitaji kubadilisha jambo. Huenda Ronaldo anatakiwa kukubali kama alivyosema Zidane kwamba mambo si safi.

Ukimuona Ronaldo anavyokwenda, huenda anaweza kuvurugikiwa kabisa kwa kuwa anashindwa kukubali kwamba hawako vizuri na wanatakiwa kutulia na kujipanga upya.

Yeye ni mtu aliyetoka kwenye majeruhi, lazima hawezi kurejea kwenye kiwango sahihi. Alitumika sana na muda wa kupumzika bado ulikuwa mchache kwa kuwa ‘fatiki’ ya ugumu wa michuano ya Euro inaweza kuendelea kumtafuna.


Kawaida, mchezaji nyota wa Reald Madrid ndiye anakuwa mfalme wa Jiji la Madrid ambalo ni kubwa na lenye watu wengi zaidi nchini Hispania. Lazima Ronaldo anachanganyikiwa na presha kubwa iliyojaa kichwani mwake.

Ahueni ni kidogo kwani Messi ameumia, lakini kumbuka msimu uliopita kumekuwa na presha ya watu wawili kutoka Barcelona, Neymar na Luis Suarez ambao wanaweza kuchukua utawala wake.

Ukiachana na hao, ndani ya Jiji la Madrid kuna timu ya Atletico Madrid. Hawa hawajalala na wako vizuri kabisa. Pia wana mtu anaitwa Antoine Griezmann. Wakati wowote anaweza kumpora Ronaldo ufalme wa Jiji la Madrid na hata La Liga ikiwezekana.

Bado ana ndoto za kumalizia miaka yake minne ijayo ya ubora. Februari 5, mwakani anafikisha umri wa miaka 32. Kawaida hadi miaka 35, kunakuwa hakuna ujanja tena. Lazima angependa kuongeza makombe zaidi na siku zijazo abaki katika historia kwa maana ya rekodi za juu za mafanikio.

Presha hiyo inaweza kumuangusha zaidi Ronaldo. Lazima afanye chini juu kuhakikisha anatuliza akili na ikiwezekana kusaidia kupandisha kiwango cha timu kwanza ambacho kitamsaidia yeye kupanda.

Kwa maumbile, Ronaldo anaonekana ni mtu rahisi sana kuchanganyikiwa ukimfananisha na Messi. Kutofanya vizuri kunaendelea kumchanganya zaidi na kinachotakiwa kwake ni kuhakikisha anatanguliza utulivu ili kuondoa presha ya kichwa.


Hakuna ubishi, wadhamini walioingia naye mikataba au wanaotakiwa kumlipa mamilioni, wangependa kuona ana mafanikio makubwa zaidi. Yeye analiona hilo na angependa liende kwa mafanikio zaidi ili kufikia kile wanachokitegemea wadhamini hao na uongozi na mashabiki wa Real Madrid.

Hakika kama binadamu, presha ya kichwa kwake iko juu, lakini dawa pekee ni kwake kukituliza hicho kichwa ili aweze kurudi kwenye kiwango chake huku akikumbuka, umri nao unamtupa mkono.

Takwimu za Cristiano Ronaldo:

2016/2017
Mechi: 4
Mabao: 3
La Liga: 1
Copa del Rey: 0
Ligi ya Mabingwa: 2


2015/16
Mechi: 48
mabao: 51
La Liga: 35
Copa del Rey: 0
Ligi ya Mabingwa:  16



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic