October 7, 2016


Nahodha na kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude, amepongeza maamuzi ya Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kutengua adhabu yake ya kadi nyekundu aliyoipata katika mechi dhidi ya Yanga, Jumamosi iliyopita.

Mkude amesema kadi hiyo aliyopewa na Martin Saanya ilikuwa ikimtesa na kumnyima raha kwa kuwa hakufanya kitendo kilichodaiwa kuwa alikifanya na kudai kuwa kilichotokea ni kumfedhehesha kwa kiwango cha juu kwa kumsingizia kosa ambalo hakufanya.

Kadi ya Mkude ilidaiwa kuwa ilitokana na kumsukuma mwamuzi huyo wakati akilalamikia bao lililofungwa na Amissi Tambwe.

“Ile kadi ilinifedhehesha sana na kuniweka katika wakati mgumu na kunitesa, nilikuwa nawaza kila siku juu ya mashabiki kuwa wananifikiriaje, ilionekana nimesababisha timu ikacheza pungufu, nilijua sijafanya kosa hilo kwa kuwa sikumgusa mwamuzi hata kidogo na ndiyo maana nikawa na hasira.

“Ifike hatua pindi itakapofika mechi kubwa kama hizi waletwe waamuzi kutoka nje ya Tanzania ili kuweza kuchezesha kwa kuondoa utata kama huu kwani kadi niliyopewa mimi ni wazi nimeonekana kuigharimu timu katika mchezo ule kwa kucheza pungufu.


“Nilitamani nipate mkanda wa tukio lile siku ileile baada ya mchezo kwisha niwaonyeshe Watanzania ili waone juu ya kile kilichotokea, lakini nimefurahishwa na maamuzi ambayo yananitia faraja sana ambayo yamefanya ukweli ujulikane na mashabiki wa Simba wafahamu ukweli juu ya hilo,” alisema Mkude.

SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. Kweli saanya akuwa makini na maamuzi na pia akumudu mzecho

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic