October 7, 2016

MKWASA

Licha ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kutangaza kulipa deni la mishahara wa Kocha wa Taifa, Boniface Mkwasa, mwezi huu, imeelezwa kuwa mshahara wa kocha huyo unalipasua kichwa shirikisho hilo kutokana na ukubwa wake ambao unagharimu zaidi ya nusu ya mishahara ya wafanyakazi wa TFF ambapo awali ulikuwa ukilipwa na serikali.

Inadaiwa Mkwasa anaidai TFF mshahara wa zaidi ya miezi miwili ambapo kwa mwezi anapokea kiasi cha shilingi milioni 28 mshahara aliourithi kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Martin Nooij ambaye naye aliurithi kutoka kwa Mbrazili, Marcio Maximo ambao walikuwa wakilipwa na serikali ya awamu ya nne, hivyo kulifanya sasa shirikisho hilo kuwa na mzigo mkubwa katika suala zima la kulipa mshahara huo.

Hivi karibuni Malinzi alikiri juu ya kudaiwa mshahara na Mkwasa ambapo aliahidi kutekeleza jukumu hilo ndani ya mwezi huu.

Taarifa kutoka ndani ya shirikisho hilo imeelezwa kuwa, mshahara wa Mkwasa umekuwa mzigo mkubwa TFF kutokana na ukubwa wake na kuwa uongozi wa juu unahaha kulipa.

“Hakukuwa na mazungumzo ya makubaliano tangu awali juu ya Mkwasa kurithi mshahara huo.

“Baada ya kuja Mkwasa kuna waziri aliamua kuuhamishia mshahara huo kwa kocha huyo bila ya kuwepo kwa mazungumzo ya makubaliano na TFF, hivyo kujikuta wakitakiwa kumlipa kiasi hichohicho jambo ambalo ni mzigo mkubwa kutokana na kiasi cha fedha kuwa kikubwa kwa kuwa serikali hailipi mshahara huo kama ilivyokuwa awali.

“Unajua mshahara anaolipwa Mkwasa unaweza kulipa nusu ya wafanyakazi wote waliopo TFF, hivyo unaona ni jinsi gani hali ilivyokuwa ngumu, hata sasa hajalipwa kwa miezi miwili iliyopita, huu tunaenda mwezi wa kumi, lakini kuna utaratibu unaoendelea ili aweze kulipwa fedha zake zote ndani ya mwezi huu.

“Mkwasa anatarajia kumaliza mkataba wake Machi, mwakani, naamini itabidi wamlipe tu hadi utakapofikia tamati na baada ya hapo haijajulikana kama ataongezewa mwingine ama la,” kilisema chanzo.

Aidha ilielezwa kuwa hata wafanyakazi wa TFF nao hawajalipwa kwa miezi miwili lakini wanatarajiwa kulipwa mwezi huu.


Alipotafutwa Msemaji wa TFF, Alfred Lucas kuhusu suala hilo alisema yupo kwenye kikao atafutwe baadaye, alipotafutwa baadaye hakupatikana hewani. Alipotafutwa Mkwasa kuzungumzia hilo, hakupokea simu.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic