November 22, 2016

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limeendelea kutoa adhabu na onyo kwa timu za ligi kuu baada ya kukamilika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo msimu wa 2016/17. Yanga na Simba ni baadhi ya timu zilizoguswa na adhabu za shirikisho hilo. 

Yanga Vs Ruvu Shooting
Timu ya Ruvu Shooting imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 12, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.

Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amepigwa faini ya Sh 500,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya wakati wa mapumziko kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Pia baada ya mechi kumalizika alikwenda kwenye chumba cha waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 40(1).

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya Sh 500,000 baada ya washabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa walipokuwa wakiingia vyumbani wakati wa mapumziko. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).

Tanzania Prisons Vs Simba
Klabu ya Simba imepigwa faini ya Sh 500,000 kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) na kufika wakati taratibu zote za msingi zikiwa zimemalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.

Klabu zote (Tanzania Prisons na Simba) zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa milango isiyo rasmi. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 14(14), na adhabu imezingatia Kanuni ya 14(48).

Pia Tanzania Prisons imepigwa faini ya Sh 500,000 baada ya gari la Jeshi la Magereza namba MT 0084 aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up likiwa na watu 15 kuingia uwanjani kwa nguvu, na kusababisha kupigwa na kuumizwa kwa mlinzi wa getini. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).

Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kutoka Morogoro amepewa onyo kali kwa kutoripoti baadhi ya matukio ya wazi yaliyotokea kabla ya mechi hiyo kuanza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic