November 7, 2016



Na Saleh Ally
MARA ya kwanza nilianza kuona umahiri wa beki Nadir Haroub wakati akiichezea Zanzibar katika mechi ya michuano ya Kombe la Chalenji mjini Kigali, Rwanda.
Nakumbuka ni mwaka 2000, Zanzibar ilishinda katika mechi ya ufunguzi wa michuano hiyo kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Rwanda ambao waliona vizuri kuanza na Zanzibar ambayo waliiona haiwezi ikatibua sherehe yao, lakini ikawa tofauti.
Nadir ambaye baadaye alibandikwa jina la Cannavaro, beki nyota kutoka Italia, Fabio Cannavaro akifananishwa naye kwa kucheza kazikazi, alikuwa nyota wa mchezo katika mechi hiyo ya ufunguzi.
Baadaye alitua Yanga, miezi michache tu baada ya kuonyesha kiwango bora katika michuano ya Chalenji. Tangu ametua Yanga mwaka 2001, Cannavaro amekuwa mfano wa kuigwa kwa wachezaji wengi sana.

Aliondoka Yanga, akapelekwa Whitecaps Vancouver ya Canada kama sehemu ya mkopo, lakini hakufanikiwa kufanya vizuri, aliporejea alicheza Zanzibar nusu msimu kabla ya kujiunga na Yanga tena mwaka 2006 hadi sasa.
 Cannavaro ni gwiji la timu ya Yanga, mmoja wa wachezaji wachache ambao wamecheza katika kikosi hicho kwa uwezo wa juu na muda mrefu kabisa, tena akiendelea kucheza vema.
Amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga kutokana na aina yake ya uchezaji. Havutii kabisa, si mtu anayeweza kunyumbulika na mpira, hana mbwembwe. Lakini ni mtu makini kwa maana ya kuhakikisha ulinzi.


Kaongoza ulinzi wa Yanga katika mechi lukuki na mfumo wake yeye ni “kazikazi”, anachotaka kufanya ni kuiokoa timu yake isifungwe na kupata sare au kupoteza mchezo.
 Lakini sasa, Cannavaro si yule tena, hapewi sifa zile, haonekani na inawezekana wengine wameshamsahau kama ilivyo ada ya watu wengi wa soka. Hujali na kufurahia kilicho machoni mwao wakati husika.
Kabla ya mechi ya jana, Yanga ilikuwa imecheza mechi 13 za Ligi Kuu Bara, Cannavaro alikuwa amecheza mechi mbili au zisizozidi tatu. Moja akianza dhidi ya Ndanda, akaingia dhidi ya Azam FC. Katika hali ya kawaida, unaweza kujiuliza kweli huyu ni Cannavaro?


Kama kweli ingekuwa ni haki, basi tungeweza kuomba Cannavaro ‘asiishe’, kwa kuwa ni mtendaji bora wa kazi yake, anayeijali, si mlevi, si mpenda starehe na ana uwezo wa kuendelea kufanya vizuri hata hivi baada ya kufikisha umri wa miaka 34.
Kuporomoka ghafla kwa Cannavaro kumekuwa kukinishangaza, naona ameshuka kwa kasi sana. Jambo ambalo limenifanya nianze kuamini wakati umefika wa yeye kuchagua mambo haya matatu yafuatayo.

Kwanza:
Nimekuwa nikiamini kitendo cha Cannavaro kuvuliwa unahodha wa Taifa Stars kwa utaratibu usiofaa, imechangia kumporomosha kisaikolojia.
Kwa hali ilivyo, huenda ikawa ni vigumu kumrejesha tena alipokuwa. Hivyo huu ndiyo wakati mwafaka wa yeye kuondoka Yanga na kwenda timu nyingine, mfano nchini Kenya, Rwanda au kwingineko ambako anaweza kuinua morali yake tena na kuanza kufanya vizuri angalau kwa misimu miwili ambayo atamalizia soka yake.

Pili:
Atafute timu ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara, ikiwezekana isiwe Simba. Kama atajiunga na timu nyingine, itainua morali yake, atataka kuonyesha uwezo wake na kufanya vizuri.
Kama atakuwa akipambana kuitumikia timu mpya, akapata bahati asiandamwe na majeraha, basi ana nafasi ya kucheza vizuri kabisa.
Cannavaro ana nafasi ya kucheza vizuri kwa kuwa si mchezaji mwenye tabia ya mambo mengi ndani na nje ya uwanja. Hivyo bado anaweza kurejea akawa fiti na kucheza kwa mafanikio tu, tena hata katika timu zinazoonekana ni kubwa.
Cannavaro hapaswi kuona kuhamia Stand United, Mwadui FC, Mbeya City au Ndanda ni sawa na kujishusha. Hii ni kawaida kabisa katika soka lililopiga hatua.
Huu mfumo unaitwa dropping. Wachezaji ambao hujiona umri wao umepanda sana, hata kama uwezo unaonekana juu, huondoka na kwenda kumalizia soka katika klabu nyingine ndani au nje ya nchi zao kwa lengo la kumalizia mpira wao, halafu baadaye hurejea.
Angalia nyota wengi wa Real Madrid, Barcelona wamekuwa wakifanya hivyo na baada ya hapo, hurejea katika klabu zao na kufanya kazi nyingine. Mfano ukocha, au zile za uongozi kwa maana ya kuendeleza klabu walizozitumikia kwa muda mrefu.


Tatu:
Cannavaro anaweza kubakia Yanga, hapa anatakiwa kuwa mvumilivu huenda kama alivyofanya Shadrack Nsajigwa. Atabaki kama kiongozi katika kundi la wachezaji lakini si mwenye matarajio ya kucheza kwa muda mwingi.
Hawezi kufanya vizuri kwa kuwa ni kazi kuiinua morali akiwa Yanga. Kawaida mchezaji aliyekuwa tegemeo, akiona sasa hategemewi, hufa morali kisaikolojia na kuiinua huwa ni vigumu kwa kuwa kibinadamu kuichukulia kama anaonewa au hatendewi haki hata kama hatataka kuonyesha moja kwa moja.
 Lakini kama ataamua kubaki Yanga, ajue atakuwa na muda mchache zaidi wa kufikia kustaafu na jambo muhimu kabisa analotakiwa kulifanya katika kipindi hiki wakati amebaki Yanga, ni kusomea ukocha.
Cannavaro anatakiwa kusomea ukocha kwa kuwa akiwa Yanga watamuelewa na kumpa nafasi ya kufanya hivyo kuliko akihamia timu nyingine ambao watakuwa wakitaka huduma yake ‘full mziki’.
Wachezaji wengi unaowaona walibaki katika timu au klabu zao na wanataka kuendelea kuwa kwenye ulimwengu wa soka, waliingia kwenye kozi na wakimaliza ndiyo hao akina Zinedine Zidane, Pep Guardiola na wengine wengi ambao wanafanya vizuri.
 Waliowahi kuwa manahodha kama Cannavaro au kukaa muda mwingi kwenye timu, pia wana nafasi ya kuwa makocha wazuri hapo baadaye.
Cannavaro ni mfano wa kuigwa hasa katika mambo haya; jitihada, nidhamu ya uwanjani, nje pia. Lakini ni mtu aliyefanya kazi yake kwa weledi muda mrefu. Hivyo bado ni hazina ya soka nchini na hapaswi abezwe hata kidogo.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic