November 25, 2016




Na Saleh Ally
NILIWAHI kulizungumzia suala la Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kujichanganya katika taarifa yake ambayo imetolewa na katibu mkuu wake, Mohamed Kiganja.

Mara ya mwisho, Kiganja alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari akieleza kusimamisha michakato ya mabadiliko katika suala la ubinafsishaji au masuala ya hisa, pia ukodishwaji katika klabu za Yanga na Simba.

Wakati akisimamisha, Kiganja akasisitiza kuhakikisha klabu hizo zinafuata michakato sahihi ili kufikia kile ambacho wanakusudia, jambo ambalo lilionekana kwamba hawataki figisu.

Lakini mwisho wa barua, Kiganja sijui sasa ndiyo tumuite serikali au tunakosea; kuwa serikali imezuia masuala ya kukodisha na kuwekeza na anasema wanaotaka kuwekeza wanaweza kuanzisha klabu zao.

Nilieleza namna nilivyoshangazwa, lakini leo naongeza wasiwasi wangu kwamba wale wanaozuia uwekezaji ndani ya klabu za Yanga na Simba, watakuwa wana maslahi yao binafsi na wanakataa bila sababu za msingi. Unajua hata ukiwa una nguvu ya kuzuia, basi jenga hoja za msingi ambazo zitawaonyesha wanaokusikiliza hasa wale wanaokuamini kwamba ni mtu mwenye nia nzuri na upo kusaidia michezo na si kusaidia kile unachokiamini au kinachokufurahisha.

Inawezekana sikupata bahati ya kuona ushiriki wa Kiganja katika michezo kwa miaka yote niliyoshiriki. Sikujua alikuwa wapi ndiyo maana nashindwa kumuita mgeni, lakini si vibaya kumkumbusha tu ili twende sawa.

Kwanza si vibaya kusema Kiganja ni kati ya wanaochelewesha mabadiliko katika michezo lakini nimhakikishie hiki kinachotokea sasa ni cha muda tu, iwe mwaka, miaka miwili au mitano, siku itafika na mabadiliko yatafanyika tu.

Kinachofanyika sasa ni kujaribu kuzuia mvua za masika katika kipindi cha masika kwa kutumia mikono. Mwisho itakunyeshea na utalowa tu.
Serikali ya Rais John Magufuli imeishajipambanua wazi kuwa ni “Serikali ya Viwanda”. Maana yake suala la uwekezaji linapewa kipaumbeke kikubwa.

Ndiyo maana umeona watu kutoka nchi mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Mfalme wa Morocco walikuja hapa nchini na suala la uwekezaji likachukua nafasi kubwa kwelikweli.

Unajua watu wamewekeza kwenye viwanja mbalimbali vya serikali lakini hata mara moja hawakuwahi kuambiwa kuanzisha vya kwao. Wala hakujawahi kuwa na hofu wakiwekeza na kufanikiwa watakuwa na nguvu sana baadaye wawe tatizo.

Kama serikali inawekeza katika viwanda vyake ambavyo ilivianzisha miaka nenda rudi na haikuwataka wawekezaji waanzishe vyao, vipi leo inaweza kuinua mkono na kuwa kali huku ikisisitiza wanaotaka kuwekeza ndani ya Yanga na Simba wanapaswa kuanzisha klabu zao kama Azam FC.

Wafanyabiashara wana mawazo tofauti, Bakhresa aliona anaweza kuwekeza kwa kuanzisha yake. Wengine wanaona wanaweza kuwekeza kwenye timu ambazo zina majina na hii ndiyo biashara ya kisasa zaidi.

Wanaotaka kuwekeza Yanga na Simba wanajua tayari timu hizo zina mtaji wa watu. Wao wanaweka fedha zao ili maendeleo na mgawanyo uanzie hapo. Hivyo serikali ilipaswa kusimamia hilo na kuangalia mchakato kama ni halali, mgawanyo wanauonaje na kadhalika lakini si kuzuia na kutoa hoja laini ya kila mmoja aanzishe klabu yake.

Kwanza kusema maneno laini kama hayo si jambo jema. Kuanzisha timu leo, kupambana nayo ipande daraja ni miaka mingapi? Ukinunua pia bado muda unahitajika. Lakini kuwekeza Yanga au Simba baada ya muda mfupi faida itaanza kusoma, kila mfanyabiashara hili angelipenda zaidi.

Viongozi wenye dhamana, si wafanyabiashara. Mambo yao huyafanya bila kuangalia mengi kibiashara na huenda hupitisha maamuzi ambayo kamwe hayawagusi wala kuwaharibia kitu bila ya kujua wanasimama mbele kama kigingi kuzuia maendeleo ya wapenda michezo wengi bila sababu za msingi.




1 COMMENTS:

  1. Ninachokiona ni huyo kiganja kutumia mgongo wa serikali kutimiza matakwa ya hao wanaomtuma, infact haiingii akirini eti msimamizi wa kitu akawa na mandate 100% juu ya namna ambavyo jambo fulani linapaswa kuendeshwa while wenye mandate hao wapo na wanafuata taratibu! nilimsikia kwa masikio yangu siku ile akihojiwa na Azam TV kuhusu suala la Simba kuitisha mkutano ili kufanya mabadiliko ya vipengele katika katiba yao na Kijanga akatanabaisha bayana kuwa wao kama BMT hawaitaki hiyo michakato! nikajiuliza hivi ni kiasi gani BMT wanazipa Simba na Yanga ili ziweze kuendesha mambo yao? je wanachangia uendeshaji wa kila siku wa klabu ama wanachangia kwenye usajili wa klabu? binafsi naona BMT kupitia kwa kiganja wanavuruga mipango ya maendeleo ya mpira wa Tanzania. Namshauri kiganja asitafute kiki kupitia michakato ya Yanga na Simba, wao kama BMT wapaswa kustrategize namna ambavyo kama taifa tutapiga hatua kwenda mbele, kitendo cha kuzuia michakato hii ina athari kubwa sana kwa mustakabali wa soka la Tanzania na Naomba nimwambie Kiganja na hao wanaomtumia kuwa hawezi kupambana na Simba na Yanga maana kwa kufanya hivyo atakuwa anapambana na watanzania milioni 30+.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic