November 16, 2016

SALEH ALLY 'JEMBE', AKIWA NA KOCHA MPYA WA YANGA, GEORGE LWANDAMINA BAADA YA KUFANYA NAYE MAHOJIANO IKIWA NI MARA KWANZA ANAFANYA HIVYO NA CHOMBO CHA HABARI NCHINI BAADA YA UONGOZI WA YANGA KUMFICHA KWA TAKRIBANI WIKI MOJA BILA YA YEYOTE KUJUA ALIPO. MAHOJIANO YAKE KWA MARA YA KWANZA YAMETOKA LEO KATIKA GAZETI NAMBA MOJA LA MICHEZO NCHINI LA CHAMPIONI.


Na Saleh Ally
HAYA ni mahojiano ya kwanza ya ana kwa ana kati ya kocha mpya wa Yanga, George Lwandamina tangu ametua nchini na kujiunga na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Ingawa Yanga haijamtangaza rasmi, Lwandamina ndiye kocha mpya wa Yanga, anachukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm.

Yanga iliamua kumchukua Lwandamina kutoka katika Klabu ya Zesco, uongozi ukiwa umelenga kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri zaidi kimataifa.

Msimu uliopita, Yanga iliishia katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Safari hii wanataka kufika mbali lakini wanajua Ligi ya Mabingwa si kitu kidogo na Lwandamina mchezaji kiraka wa zamani wa Mfulila Wonderers anaonekana kuwa chaguo sahihi baada ya kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu uliopita.

Kwa kipindi kirefu Yanga ilikuwa imemficha Lwandamina katika moja ya hoteli maarufu na kongwe za kitalii na kuwapa waandishi wa habari kazi ngumu ya kumpata, hadi Championi lilipofanikiwa baada ya uchunguzi wa takribani siku tano za kumtafuta bila ya mafanikio katika hoteli mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Baada ya kumpata, Lwandamina alionekana ni mtulivu, mzoefu na asiye na haraka na alitoa ushirikiano katika mambo kadhaa ambayo aliweza kuyazungumza.


SALEHJEMBE: Umekaa mafichoni, nini hofu yako?
Lwandamina: Sina hofu, wenyeji wangu ni Yanga wanaweza kulijibu hilo.

SALEHJEMBE: Lini hasa unaanza kazi rasmi?
Lwandamina: Pia hilo wanaweza kujibu wao Yanga.

SALEHJEMBE:Kuna taarifa kwamba umeanza kuleta wachezaji na wengine umewatema baada ya kuwaona?
Lwandamina: Nimezisikia hizi taarifa, lakini si kweli. Siwezi kuleta au kumtema mchezaji wakati sijawaona vizuri wachezaji nilionao.

SALEHJEMBE: Uliwashuhudia kwenye runinga mechi ya mwisho ya ligi, haitoshi?
Lwandamina: Mechi moja haitoshi, nahitaji kuona tena na tena. Ingawa kuna baadhi unaweza kuwatupia jicho na kujua ubora wao.

SALEHJEMBE: Kama yupi alikuvutia?
Lwandamina: Yanga ina wachezaji wengi wazuri, niliwaona wengi na ninaweza kuona tena na kuwafanyia kazi .

SALEHJEMBE: Utawaonaje sasa, wakati wa mazoezi?
Lwandamina: Nafikiri kabla, nitajua namna ya kufanya, au ninaweza kuangalia mechi zao zilizopita.

SALEHJEMBE:Hujaona hata mmoja kuwa anastahili kuondoka na ikiwezekana uongeze wawili, watatu kutoka Zesco?
Lwandamina: Nitafikia huko au la. Kuwa kocha si lazima uache tu wachezaji, unaweza kuwakuta na baadaye kuwatumia na mambo yakawa mazuri. Ndiyo maana nahitaji kuona tena na tena.


SALEHJEMBE: Unawajua Simba?
Lwandamina: Ndiyo, kwa maana ya kuwasikia lakini nimewahi kuwaona na kucheza nao.

SALEHJEMBE: Unawazungumziaje?
Lwandamina: Najua ni timu kubwa, wapinzani wa Yanga. Najua ina mashabiki wengi pia, maana tulipocheza nao na kuwafunga mabao 3-0, niliona mashabiki wao walivyojisikia vibaya.

SALEHJEMBE: Nakumbuka ilikuwa ni mechi ya kirafiki kwenye Simba Day?
Lwandamina: Ndiyo, nakumbuka baada ya kuwafunga, walimfukuza yule kocha wao Mzungu (Zdravko Logarusic).

SALEHJEMBE: Timu kama Yanga, presha ni kubwa ukilinganisha na Zesco ambayo kwa hapa ninaweza kuifananisha na Azam FC, utaiweza?
Lwandamina: Kazi ya ukocha ni presha kila sehemu. Najua nitaweza kwa kuwa nimecheza kipindi kirefu nikiwa na Mfululila Wonderers, kuichezea pia ni presha. Kucheza Ligi ya Mabingwa au mechi kubwa ni presha pia.

SALEHJEMBE: Huyu kiungo, Meshack Chaila ambaye anaelezwa kuwa kipenzi chako, hata kama sasa hujaamua kuja, unafikiri hapo baadaye ana nafasi ya kujiunga na Yanga ambayo imeonekana kuwa na tatizo la kiungo mkabaji.
Lwandamina: Yote hayo yatategemea nimeona vipi baada ya kuwaangalia na kufanya nao mazoezi ikiwezekana sawa.

SALEHJEMBE:Ungependa wakati unaanza kazi na kikosi chako, mazoezi yawe katika mazingira yapi.
Lwandamina: Napenda mazingira tulivu, lakini ni suala la kuzungumza kwanza na uongozi.

SALEHJEMBE:Una mshambuliaji kama Jesse Were raia wa Kenya, vipi usimuunganishe Yanga, Januari hii ili akusaidie kwenye michuano hasa ya kimataifa.
Lwandamina: Yote yanawezekana, ingawa yeye ana mkataba na Zesco na tunapaswa kuuheshimu. Sijafanya lolote hadi sasa, ila ninachoweza ni kupendekeza.

Nitafanya chochote baada ya kuwaona zaidi wachezaji wa Yanga, siwezi kuamua kabla. Pia mimi napenda kuwaamini ninaowakuta.

SALEHJEMBE: Wewe ni kocha wa aina gani?
Lwandamina: Sijaelewa vizuri.

SALEHJEMBE: Mkali sana, jeuri, kiboko ya wachezaji au?
Lwandamina: (tabasamu), ni mtu ninayependa wachapakazi bila ya kuchoka. Napenda wachezaji wanaopenda kushinda, pia ninapenda kuwaamini wachezaji wangu. Pia napenda kuwa na kikosi cha watu wanaopendana kama ndugu.

SALEHJEMBE: Wachezaji wa Yanga wamepumzika, wamepewa wiki mbili. Kimpira hii ni sawa?
Lwandamina: Si sawa, kwa mfumo wa sasa wa ufundishaji. Mchezaji hata kama amepumzika lazima ashiriki michezo mingine tena kujiweka fiti.


SALEHJEMBE: Umesaini mkataba wa miaka mingapi na Yanga?
Lwandamina: Hili suala ni siri kati ya mimi na Yanga.

SALEHJEMBE: Michezo mingine kivipi?
Lwandamina: Mfano mpira wa kikapu na kadhalika. Unajua mchezaji akikaa wiki mbili bila kucheza, kitaalamu ni tatizo. Kiwango chake hushuka chini kabisa. Unapoanza, unaanzia chini kabisa, si jambo zuri.

SALEHJEMBE: Kwa kuwa una mgeni unamtegemea tukupe nafasi.
Shukrani kwa muda wako. Tukuahidi ushirikiano utakapokuwa hapa kwa kuwa kazi yetu ni moja, kusaidia mchezo wa soka kubadilika na kukua kama ilivyo kwa mingine.

Lwandamina: Karibuni sana.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic