November 4, 2016




Na Saleh Ally
SIMBA ndiyo vinara wa Ligi Kuu Bara, sasa wanaongoza msimamo wa timu 16 wakiwa na pointi 35 wakiwa wamefunga mabao 25 na kufungwa matatu tu.

Kikosi cha Simba chini ya Kocha Joseph Omog kimeshinda mechi 11 kati ya 13 kilizocheza, kimetoa sare mbili na kubaki kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo nyumbani wala ugenini.

Mwendo wa Simba, ndiyo bora zaidi kuliko mwingine wa timu nyingine yoyote kwenye Ligi Kuu Bara. Hivyo sahihi kusema hadi sasa kwenye ligi hii, Simba ndiyo timu au kikosi bora kabisa kuliko vingine.

Faida zaidi kwa Simba, pamoja na ugumu wa ligi hiyo, wao wanafanya vizuri zaidi na wapinzani wao Yanga na Azam FC wanaendelea kuwa na mwendo wa kusuasua ambao huenda mabadiliko yake yakachukua muda hasa kama hawatatulia.

Si sahihi hata kidogo kuanza kufikiria Simba bingwa kuanzia sasa, yanaweza yakawa ni mawazo ya kishabiki zaidi kuliko hesabu za kitaalamu na uaminifu wa mpira kuwa una mambo yake na yanatokea kila sehemu, si Tanzania pekee.

Simba itakuwa na nafasi ya kuwa bingwa kama itaanza vema mzunguko wa pili na kuumaliza sawasawa. Ila sasa, imejiweka kwenye nafasi ya kutajwa kuwa ina nafasi ya kuwa bingwa lakini si uhakika, Simba bingwa!

Lengo langu si kuzungumzia ubingwa sasa, lakini naweka hoja mezani ambayo inanishangaza kabisa. Inaonyesha kuna pande mbili ambazo hazijui biashara ya mpira na faida yake lakini pande hizo zipo ndani au nje ya mchezo wa mpira.

Hapa ninalenga suala la biashara, kwamba pamoja na kushinda, Simba inahitaji kufanya biashara. Kufanya biashara si kwa ajili ya kutwaa ubingwa pekee, badala yake kwa klabu maarufu na kubwa kama Simba, inapaswa kuitumia timu yake kuingiza fedha nyingi.

Angalia Simba sasa imecheza mechi 13 za Ligi Kuu Bara, kifuani kwa wachezaji wake hakujaingiza hata shilingi moja! Hii si habari njema kwa watu wanaojua kuyatumia matundu au nafasi za kuingiza kipato kupitia mchezo wa soka.

Timu inayofanya vizuri zaidi, maarufu sana, yenye mashabiki wengi katika nafasi ya kwanza au ya pili, kongwe, yenye historia kubwa. Haina mdhamini na kifua cha wachezaji wake, hakina faida hata kidogo katika klabu!

Simba vipi hawana kitengo cha watu makini wa masoko? Hawa wangehakikisha hata kama kuna mkataba mfupi wa msimu ili watumie vifua vya wachezaji kuingiza kipato. Huenda kitengo cha masoko kinaonekana ni jambo dogo kutokana na mambo kupelekwa kimazoea.

Inawezekana ndani ya klabu za Tanzania, mtengeneza fitna akapewa nafasi ya juu au umuhimu kuliko mtu wa masoko. Hii ni yale mawazo kwamba katika soka, ni ushindi tu na hata ukipatikana, hakuna anayejua unaifaidisha vipi klabu zaidi ya furaha ya mioyoni. Hakika, haya yamepitwa na wakati, furaha ndiyo, lakini soka ni biashara, tena biashara kubwa.

Upande wa pili ni wale walio nje ya soka. Wenye makampuni ya kuuza bidhaa mbalimbali zikiwemo ndogondogo au saizi ya kazi. Hata kama ingekuwa ni magodoro, matank ya maji, wauza gesi za kupikia majumbani, wauza simu, Tecno, Huawei na wengine. Hivi kweli hamuoni nafasi ya kujitangaza na Simba?

Najiuliza, hakika mna watu wazuri wa masoko ambao wanafikiri mbali na kuona sehemu ambako wanaweza kuongeza soko? Nani anaweza kusema Simba haiwezi kumuongezea soko?

Kama kampuni ndogo na zile za saizi ya kati zinaamini haiwezi kuongeza soko, angalia Yanga ambao ni kubwa kama Simba, wanapiga pesa na moja ya makampuni makubwa kabisa Tanzania ya Quality Group.

Tena hii inatoa funzo, si lazima kama kampuni ikidhamini Yanga, eti lazima idhamini na Simba ndiyo ifanye biashara. Haya mambo ya kizamani ya ‘kubalansi’ yamepitwa na wakati, vizuri kujiamini zaidi.

Viongozi wa Simba, sijui kama wanaliona hili na kama wanajua wanatengeneza hasara kila kukicha huku wakifurahia ushindi pekee. Hao wenye makampuni, soka ni sehemu inayolipa katika kufikisha matangazo ya bidhaa zenu, jifunzeni katika hili na wanaohusika na masoko katika makampuni yenu, wainue vichwa zaidi na kuwa wepesi katika ubunifu.


SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. Swala la kwamba mashabiki wa simba hawatakiwa kuwaza ubigwa kwa sasa huo utakua ni uoga kila shabiki Bia yake nintikubyake kuchukua ubigwa mlianza kwa kusema tusubiliae kwanza mechi za mikoani mikoani wameenda wanashinda mnaleta visingizio vingine vya round ya pili.ngoja tuone..
    Kuhusu swala la wadhamini tunatakiwa kujua kwamba simba ni timu kubwa kutangaza biashara za watu bila timu kupata masirahi ni bora timu ibaki na hasara kifuani kama ulivyosema.MF.tu ni ligi kuu ya uingeleza,walivyojitoa Barclay's na ligi kubaki bila udhamini haina maana kwamba ligi ya uingeleza aina maofisa masoka makini ama nini..mpira ni biashara sio kuchafua jezi kwa matangazo wali timu inabaki na madeni...asante.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic