November 30, 2016



Mkurugenzi wa Kampuni ya Millen Magese Group (MMG), Millen Magese  ameishukuru Serikali kupitia kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, huku akifurahishwa na uwakilishi mzuri wa Miss Tanzania Julitha Kabete (19), aliyeingia kwenye tano bora katika mashindano ya Afrika. 



Kabete  alipeperusha vema Bendera ya Tanzania kwa kuingia hatua ya tano bora ya mashindano yaliyofanyika Jumamosi nchini Nigeria na  kuitoa Tanzania kimasomaso. 

Akizungumza na waandishi wa habari, Millen alisema ni faraja kubwa kwake na nchi yake kwa  Julitha kuingia hatua ya tano bora, lakini sababu kubwa ikiwa ni ushirikiano iliyoupata. 


"Napenda kuchukua fursa hii kwa heshima nyingi na taadhima kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa ushirikiano wa hali ya juu, kupitia Waziri Nape Nnauye kwa ushirikiano na mwongozo wa kipekee, wazazi na familia nzima ya Julitha kwa malezi yenu kwa binti , Kamati nzima ya Miss Tanzania chini ya Mkurugenzi Hashim Lundenga (Tunashukuru sana), kwenu wanahabari hatuna maneno sahihi ya shukrani, asanteni sana," alisema Magese. 


Naye mshindi huyo wa tano wa Miss Afrika, Julitha Kabete, alisema anashukuru kwa ushirikiano aliupata, lakini pia nchi yake kupata thamani ya kipekee katika shindano hilo kupata nafasi tano za juu. 

Kabete alisema kuwa licha kutopata nafasi ya kwanza, lakini ameweza kuiwakilisha vema nchi katika shindano hilo, kwa sababu ushindani ulikuwa mkali sana. 

"Kwangu ni faraja kubwa kwa kuwa balozi mzuri wa Tanzania na kuweza kuwashinda wenzangu wengi ikiwemo na mwenyeji wetu ambaye hakuingia katika hatua ya tano kama ambayo mimi nimeipata nina furaha kubwa sana,"alisema Kabete. 


Alisema kuna mkataba mpya ambao utaingiwa kati ya Tanzania na waandaaji wa shindano hilo la Miss Africa katika kutoa ushirikiano wa ushiriki wa shindano hilo. 

Katika shindano hilo lililofanyika Novemba 26, mwaka huu nchini Nigeria, taji la shindano hilo lilienda kwa mnyange Neurite Mendes (23) wa Angola, aliyenyakua kitita cha dola za Marekani 25,000 sawa na sh.milioni 52 ya Kitanzania na  gari jipya (brand new 2016 Ford Escape), safari maalum ya mafunzo nchini Uingereza na Ubalozi wa Mazingira– Afrika. 


Mshindi wa pili katika shindano hilo ni Refilwe Mthimunye wa Afrika Kusini alipata dola za Kimarekani 15, 000 ni sawa na zaidi ya sh. milioni 32, na Jencey Anwifoje kutoka nchini Cameroon, akiibuka wa tatu na kupata dola za kimarekani 10,000 sawa na zaidi ya  sh.milioni 20. 



Shindano la Miss Afrika 2016 lilichagizwa kwa heshima ya mji wa Calabar na jimbo la Cross River, chini ya Gavana wa Cross River Profesa Ben Ayade. 

Kampuni tanzu ya Millen Magese (MMG) imeanzishwa kwalengo la kuibua, kuinua, kutambua na kukuza vipaji katika Bara la Afrika na ngazi ya Kimataifa. 

MMG imeweza kufika nchi mbalimbali barani Afrika na mwaka 2012 iliweza kuendesha shindano la kwanza ya aina yake ambapo wanamitindo wawili kutoka Tanzania walipata nafasi ya kupata mikataba nchini Afrika Kusini. 


Wanamitindo kutoka mashindano hayo wameweza kuendelea kufanya vizuri maonesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Mwaka huo huo wa 2012 MMG kupitia mradi wa TIFEX iliwezesha wabunifu kutoka nchini kupata uzoefu na uelewa wa wiki za mitindo duniani. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic