November 23, 2016



Na Saleh Ally
Kama utazungumzia mitandao, naamini unakumbuka Blog ya SALEHJEMBE ndiyo pekee iliyofanya mahojiano na Kocha mpya wa Yanga, George Lwandamina tokea ametua nchini na kuwekwa mafichoni na uongozi wa Yanga ambao juzi uliamua kufunguka na kuweka mambo hadharani.

Katika mahojiano hayo, moja ya mambo ambayo Lwandamina anaonekana ameyatupia macho mapema ni kuhusiana na suala la kiungo mkabaji ambalo Yanga wamekuwa wakilifuatilia kwa muda sasa.

Lwandamina ambaye alisema anahitaji kuangalia DVD za wachezaji wake wakiwa kazini ili kupata uamuzi sasa na si zile hadithi kwamba anaachwa au anasajiliwa huyu, alisema Thabani Kamusoko anaweza kuwa kiungo bora mkabaji.

 Kama atakuwa ameshindwa kulifanyia kazi, mfano kukosa mchezaji kwa wakati husika anaamini Kamusoko atafaa.

Lakini Hans van Der Pluijm ambaye anabaki tena Yanga, yeye mara kadhaa alipenda kumpanga Kamusoko kama kiungo wa ushambulizi kwa kuwa uchezaji wake ni ‘direct football’, si ‘hold’. Yaani anayecheza kwa kusukuma zaidi kuliko yule ambaye anaweza kukaa na mpira kwa kipindi fulani, mfano wa Haruna Niyonzima.

Utaona kwa hali ilivyo kwamba kweli ndani ya Yanga kuna tatizo la namba sita. Wanahitaji mtu imara hasa na ikiwezekana ambaye ameshaanza kupata au mzoefu hasa wa michuano ya kimataifa.

Hisia ya kila kitu kizuri kinapatikana nje, huenda ndiyo inayowafanya Yanga kutoangalia karibu na kuwavuka wachezaji wengi wanaoweza kumaliza tatizo lao hilo na mambo yakaenda vizuri.


Inawezekana kwa mchezaji kama Misheck Chaila wa Zesco ambaye ili wamlete Tanzania lazima watakuwa wamelipa si chini ya dola 50,000 hadi 70,000 au zaidi. Hii ni zaidi ya Sh milioni 120 hadi 140 na ushee.

Fedha hizo zingeweza kutumika kumsajili Himid Mao Mkami wa Azam FC, ninaamini Yanga wangekuwa wamemaliza tatizo lao la kiungo mkabaji.

Himid, mtoto wa kiungo bora wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Mao Mkami aliyekuwa maarufu kama Ball Dancer, kwa sasa ndiye kiungo bora zaidi mkabaji hapa nchini. Hii ni bila ya kujali anachezea timu ipi.

Tumeona mechi nyingi za Azam FC ikicheza na timu ndogo, kubwa, mechi za kimataifa na hata anapokuwa akiichezea Taifa Stars. Ameonyesha ni bora, mpambanaji na ana sifa nyingi za viungo wakabaji.

Lakini faida ya kumpata Himid ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza namba nyingi. Kwa Yanga wanakuwa kama wanamsajili Mbuyu Twite mwingine, lakini kwa Himid kunakuwa na faida nyingine kwa kuwa ni kijana na sasa ndiyo amekomaa.

Inawezekana kabisa, Yanga wakawa wanaona hawana shida ya kusajili mchezaji kutoka Azam FC tena ikiwezekana kwa kutoa fedha nyingi, kisa watakuwa wanaangalia suala la upinzani wao na Azam FC.


Au wataona mchezaji kutoka Tanzania hata kama uwezo wake uko juu kuliko wageni, basi hapaswi kupewa au kununuliwa kwa fedha nyingi. Na wanaweza kumpata anayetokea nje, hata kama uwezo wake ni wa kawaida, basi anunuliwe tu kwa fedha ya juu.

Kwa tatizo wanalopambana nalo Yanga kwa kipindi hiki, wanahitaji mtu mwenye mapafu ya ‘mbwa’ kama Himid. Ambaye anapokuwa anacheza namba sita, basi ana uwezo wa kubadilika kuwa namba nne au tano kulingana na mazingira na kinachotokea uwanjani kutokana na wakati husika.



Kuna haja pia ya kuangalia ubora wa wachezaji wa nyumbani na kukubali bora wanachokifanya. Pia kuachana na utamaduni wa kuamini kila kitu kinachotolewa nje ndiyo bora zaidi.

Huenda Yanga wamesahau kuangalia ndani kwa kuwa wanaamini kila cha nje ni bora zaidi. Lakini ukweli usio na kipingamizi, dawa ya tatizo lao, ipo hapa Tanzania na dozi bora, Himid anayejulikana kama Ninja, angekuwa tiba.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic