January 18, 2017




Na Saleh Ally 
HAKUNA ubishi kuwa hapa nyumbani mchezo maarufu zaidi ni soka. Lakini duniani kote, soka ndiyo mchezo wenye mashabiki wengi zaidi tena kwa kiwango kikubwa cha asilimia nyingi.


Wafanyabiashara watatu wakubwa ndiyo wameamua kuwekeza katika soka na mabadiliko yamekuwa yakionekana hata kama si sehemu zote.


Said Bakhresa, yeye ameamua kuanzisha timu yake ya Azam FC. Imekuwa na mafanikio makubwa kwa muda mfupi ingawa haijaweza kuwashawishi mashabiki sana kama ilivyo kwa wakongwe, Yanga na Simba.


Yusuf Manji, bilionea ambaye amekuwa hataki kuonekana au kujitangaza sana kwa maana ya utajiri, yeye alikuwa tayari kuwekeza Yanga kwa njia ya kukodisha lakini inaonekana kumekuwa na figisu, jambo linaloonekana kuikwamisha Yanga na kuifanya iingie katika mwendo wa kusuasua.


Wakati Yanga bado hawajajua kipi ndiyo au hapana, Simba wapo kwenye mchakato wa kukubali Sh bilioni 20, ofa kutoka kwa bilionea kijana zaidi barani Afrika Mohammed Dewji ambaye utajiri wake unafikia dola bilioni 1.4 (zaidi ya Sh trilioni tatu).


Mo Dewji anataka kununua hisa za Simba kwa asilimia 51 ili kuanza kuiendesha kwa nafasi na kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko.


Wakati mabilionea hao wa Tanzania wameingia katika soka, upande wa Angola, mwanamama tajiri zaidi nchini humo na tajiri zaidi kuliko wanawake wote barani Afrika, Isabela dos Santos, yeye amechaguliwa kuwa rais wa klabu kongwe ya Petro Luanda, hali ambayo inaonyesha wazi sasa ameamua kuingia kwenye soka.


Utajiri wa Isabela ni dola bilioni 3.3 (zaidi ya Sh trilioni 7). Kumbuka mwanamama huyu mwenye watoto watatu ni mtoto wa Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola.
Lakini ni mke wa Sindika Dokolo, bilionea kutoka DR Congo, pia ni mtoto wa bilionea wa miaka nenda rudi wa nchini humo. Wawili hao walikutana wakiwa shule barani Ulaya ambako walianzisha uhusiano wa kimapenzi.



Klabu ya Petro de Luanda ilianzishwa mwaka 1980 na kupata mafanikio makubwa baadaye. Lakini miaka ya kuanzia 2000, ilianza kudorora na sasa Isabela anakuwa kama mkombozi. Ushindi wake wa cheo cha rais, bila shaka ni kama ukombozi kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwa wanajua Isabela ni mwanamama wa chuma ambaye hatakubali kuendesha kitu kinachodorora.


Isabela ni injinia kitaalamu. Lakini amekuwa mfanyabiashara aliyejijenga katika mafuta, madini hasa almasi lakini barani Ulaya hasa Ureno na Hispania amewekeza katika makampuni makubwa ya simu ambako anaingiza kiwango kikubwa cha fedha.


Lakini hivi karibuni kajiingiza kwenye biashara ya saruji na ameanza umiliki wa mabenki, hasa nchini Ureno.
Baadhi ya wananchi au wanasiasa wapinzani wamekuwa wakipinga kwamba anapendelewa sana kwa kuwa ni binti wa kwanza wa rais dos Santos, akiwa ni mtoto wa kwanza wa mkewe wa kwanza.


Mwanamama huyo ambaye pia ni Rais wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Angola, anasifika kwa kuwa na tabia ya kutaka ushindi au mafanikio makubwa kwa kila anachokiongoza.


Kabla aliwahi kuwekeza nchini Marekani katika mpira wa magongo. Lakini baada ya kushinda katika uchaguzi na kuwa Rais wa Petro de Luanda, alisisitiza anataka kuona timu hiyo inakuwa kubwa zaidi barani Afrika.


Isabela anasema fedha ni suala linalotokana na ubunifu na uwezo wa uamuzi hasa katika uchapaji kazi.
Amesisitiza, kama Waangola na hasa watu wa Klabu ya Petro de Luanda wanaamua kwa kushirikiana naye bega kwa bega, basi hakuna anayeweza kuizuia klabu hiyo kurudisha sifa yake na kuwa kubwa sana.


Kwa mashabiki wa Petro de Luanda ni faraja upya, lakini hofu kubwa ni kwa mashabiki wa timu nyingine. Kwamba fedha za Isabela na kwa kuwa ndiye binti kipenzi wa Rais wa Angola ambaye amekaa madarakani tokea mwishoni mwa miaka ya 1980, huenda upendeleo unaweza kuwa wazi.
Wengi wanaamini hata waamuzi, viongozi wa Shirikisho la Soka la Angola, watakuwa waoga na kuipa nafasi Petro de Luanda kufanya vizuri hata isipostahili.


Utaona, kuingia kwa bilionea huyo namba moja kwa upande wa wanawake Angola na Afrika nzima, kumewagawanya wengi. Wapo walio na faraja kuu na wengine hofu hasa ya haki, imetawala.


Isabela kasisitiza kwamba mafanikio ndani ya Angola ni namba moja lakini anachotaka yeye ni Petro de Luanda kuwa klabu kubwa zaidi Afrika na angependa kuona inazipa shida kubwa timu kubwa kutoka Afrika Kaskazini, Magharibi na ikiwezekana zile za Afrika Kusini huku akiitaja Mamelodi Sundowns ambayo pia iliwahi kuwa na rais mwanamama.


Isabela anaishi kwenye nyumba ya kifahari ambayo inaaminika ni ghali zaidi kuliko Ikulu ya Angola ambayo inaongozwa na baba yake mzazi. Lakini si rahisi kuipiga picha kutokana na ulinzi mkali.


Anamiliki boti ya kisasa, ndege mbili kwa ajili yake na magari zaidi ya 12 ya kifahari likiwemo aina ya Maybach Exelero lenye thamani ya dola 250,000 (zaidi ya Sh milioni 544) ambalo wengi waliamini ni la kisela na si kwa mtu kama yeye.

Kwa kuwa ana umri wa miaka 43, Isabela amekuwa haoni shida ‘kujiachia’ na msisitizo wake ni kwamba yeye ni mama kijana anayehitaji kuishi anavyoamini anataka.
Lakini amekuwa akisisitiza kuwa, sasa furaha yake ni soka na anaamini uwekezaji wake katika mchezo huo utakuwa sawa na ilivyo kuwekeza katika madini au zaidi.


Hakuna aliyepinga kuingia kwake katika uwekezaji. Wengi wanajua si mpenzi sana wa soka au haujui vizuri. Lakini wanaamini kwa kuwa ni mfanyabiashara, atasaidia kupatikana kwa mabadiliko kwa kuwa anajua ili kufanya biashara vizuri katika soka, basi lazima timu inayotaka kufanya vizuri ishinde na kupata makombe.



Isabela anataka makombe yamsaidie kupata biashara. Hivyo lazima atahakikisha Petro de Luanda inaamka na kuwa bora zaidi ya sasa na kumsaidia kupata na kufanya biashara ya uhakika.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic