February 24, 2017




Na Saleh Ally
GUMZO la Simba dhidi ya Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kesho Jumamosi linazidi kupaa.


Gumzo hilo litahitimishwa kesho kwa majibu, kwamba nani ni mshindi na nini kimetokea. Baada ya hapo itakuwa mazungumzo mengine ya kilichotokea.


Mengi yanaweza yakazungumzwa, kila mmoja anaweza akapata anachotaka kwa kuwa ni mechi yenye burudani kubwa. Lakini kuna wachezaji wa nafasi ya kufanya vizuri licha ya kwamba wanaonekana hawakuwa tishio sana hapo awali.


Kila safu ya ushambulizi ina nafasi ya kufanya vizuri kwa kuwa kila upande umeonyesha una uwezo mkubwa wa kufunga mabao ingawa kuna tofauti ya mabao 10 kati yao.


Yanga imecheza mechi 21 na kufunga mabao 46 na Simba wamecheza 22 na kufunga 36. Lakini ndiyo safu kali zaidi ya ushambulizi katika ligi hiyo.


Zinakwenda katika mechi ambayo inaonekana itakuwa ya kuamua au kutoa nafasi kubwa zaidi kwa nani awe bingwa.


Kila mshambulizi kwa kila upande anaweza kufanya vema. Lakini kuna washambuliaji wawili ambao huenda ndiyo wakawa waamuzi wa mechi hiyo na mabeki wanapaswa kuwa makini sana.


Washambulizi hao wote ni wageni, Laudit Mavugo upande wa Simba na Obey Chirwa kwa Yanga. Hawa ni watu hatari sana lakini wamekuwa wakibezwa kwa muda mrefu.


Kasumba ya mashabiki wa Yanga na Simba, hali kadhalika baadhi ya viongozi wamekuwa ni watu wenye haraka sana na wasio na subira wakiamini kwamba soka si mchezo wa kukurupuka katika kila jambo.


Hivi karibuni, kidogo Chirwa na Mavugo wameanza kuonyesha cheche katika mechi walizocheza kwa kufunga lakini inaonekana kabisa kuna njia nyeupe kwa mmoja wao au wote kuibuka katika mechi hiyo na kuwa gumzo.


Kuwa gumzo kwa upande wa uzuri, lazima uwe bora. Tayari wao ni bora na wameanza kuizoea ligi ya Tanzania.


Hii inawapa nafasi ya kuanza kuonyesha walichonacho, kufanya wanachoweza na kuzitumia nafasi wanazoweza kuzitengeneza.


Tayari Chirwa ambaye alijiunga na Simba akitokea FC Platnums ya Zimbabwe amefunga mabao nane katika Ligi Kuu Bara huku akiwa hajapata bao kwenye mechi za michuano ya Kombe la Shirikisho.


Wao wawili watakuwa na nafasi ya kuchagua kwa kuwa wana kila kitu. Wakifanya vema, basi watakuwa gumzo. Wakiboronga, basi watapotea kabisa.


Mavugo ambaye amejiunga na Simba akitokea Vital’O ya kwao Burundi. Tayari katikisa mabao saba. Sita yakiwa ya Ligi Kuu Bara na moja la Kombe la Shirikisho.


Kinachofanya sura hizo mbili nizione kuwa zina nafasi ni mambo yafuatayo matatu ambayo yanafanana kabisa kutoka kwa kila upande.


Kasi:
Wote wawili wana kasi. Ni wachezaji wenye uwezo wa kukimbia kwa kasi na raha yao wanalenga katikati kwa maana ya kuelekea langoni.

Kawaida mchezaji hata kama si mzuri wa umiliki wa mpira, kama ana kasi anakuwa tatizo kwa mabeki kwa kuwa anasababisha kuzaliwa kwa hofu, kawaida ikizaliwa huondoa utulivu. Kukosekana kwa utulivu huzaa makosa na kusaidia kuzaliwa kwa nafasi kwa timu pinzani. Wakiitumia, mmekwisha.


Kujiamini:
Usitegemee kumuona Chirwa au Mavugo haladu akawa ana hofu. Suala la mabeki wawili au watatu wako mbele yao, si jambo la kusumbua vichwa vyao.

Hali ya kujiamini inawafanya kuwa hatari zaidi na kila mmoja anapenda kukimbilia ndani ya boksi kama ilivyo kwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Ben Mwalala.


Ndani ya boksi anakuwa na faida mbili. Ukimuacha atafunga, ukimgusa ataanguka. Umakini unatakiwa lakini kasi kubwa ya maamuzi ili kuwathibiti.


Lakini kingine walichonacho, ni ubora wa ujuzi. Mfano kuficha mpira au kupiga chenga na kila mmoja wao akipata nafasi ya kupiga shuti, basi kama atalenga ujue yamewakuta.


Kumalizia:
Hili ndiyo suala liliwasua wote. Lakini ukiangalia mabao mawili kati ya matatu ya mwisho aliyofunga Chirwa au Mavugo utagundua kuna utulivu mkubwa katika suala la kumalizia.


Umaliziaji ulikuwa tatizo kubwa kwa Mavugo, hata alipowachambua mabeki wawili, alikurupuka kupiga mashuti bila ya kutulia. Lakini angalia bao lake alilofunga dhidi ya Majimaji au lile dhidi ya Prisons.


Hali kadhalika Chirwa, bao zuri mechi dhidi ya Ngaya katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini utaona amekuwa akifunga mabao ya namna hiyo mfululizo. Hii ni silaha kubwa kwao na kama watapata utulivu kama huo, basi kuanzia Jumamosi jioni hadi Jumapili, gumzo litakuwa ni sura zao.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic