March 27, 2017



Wikiendi ijayo zitakuwa ni dakika 180 muhimu sana kwa timu za Simba na Yanga. Wekundu wa Msimbazi watategemea pigo moja tu itakalolipata Yanga, kisha wao wawe na uhakika wa asilimia nyingi wa kuutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 55, wakati wapinzani wao kwenye vita hiyo, Yanga, wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 53.

Simba ambayo mara ya mwisho kuutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa ni msimu wa 2011/12, enzi hizo ligi ikiwa na timu 14, inategemea Yanga ichinjwe na Azam FC katika mchezo wao wa Jumamosi ijayo, halafu wao wapambane kuifunga Kagera Sugar kesho yake Jumapili ili wawe wamewakimbia Yanga kwa tofauti ya pointi tano, kila timu ikiwa imebakiza mechi tano.

Kama ikiwa hivyo, basi Simba itakuwa na uhakika mkubwa wa kuutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Lakini inatakiwa pia ipate pointi nyingine sita dhidi ya Toto na Mbao kabla ya kurejea Dar.  

Hata hivyo, haitakuwa rahisi hata kwa upande wa Simba pia katika mchezo wao dhidi ya Kagera kwenye Uwanja wa Kaitaba, kwani wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu kupata matokeo kwenye uwanja huo.

Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilipata pointi nne dhidi ya Kagera Sugar, kwa maana ya kuwa ilitoka sare katika mchezo wa kwanza mjini Bukoba kabla ya kupata ushindi katika mchezo wa pili dhidi ya timu hiyo jijini Dar es Salaam. 

Tangu msimu huo ambao Simba ilipata ubingwa kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya washindi wa pili Azam FC, enzi hizo ligi ikiwa na timu 14 tu tofauti na sasa ambapo ina timu 16, Wekundu hao wamekuwa wakipata upinzani mkali kutoka kwa Kagera Sugar.

Tangu msimu ambao Simba ilipata ubingwa, wamekutana na Kagera mara 11, wameshinda mara 5, wametoka sare mara 4 na kufungwa mara mbili.

Katika uwanja wa nyumbani wa Kagera Sugar ambako wanakwenda kucheza wikiendi hii, Simba wamekutana na Kagera mara 5, wameshinda mara mbili, wametoa sare mara mbili na kufungwa mara moja.

Hata hivyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema: “Hakuna wa kutuzuia kupata pointi katika mechi hizo, kwanza hilo wanatakiwa walitambue hata wajiandae kwa namna gani kwa sababu tunataka kumaliza ligi kama ambavyo tulianza mwanzoni.

“Lakini kingine ambacho kinatupa jeuri ya kuona tuna kila sababu ya kutamba huko ni uimara wa kikosi tulichonacho tofauti kabisa na wao na sasa amebaki mchezaji mmoja pekee Method Mwanjale ambaye ndiye mgonjwa hivyo tukienda huko tunaenda tukiwa kamili."

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic