August 18, 2017




NA SALEH ALLY
MSIMU uliopita, kikosi cha Ndanda FC kilinusurika kuteremka daraja hadi la kwanza “kimkandamkanda” kwa kuwa mambo yalikuwa mabaya kupita kiasi.

Licha ya kuwa kati ya timu zinazoonekana zinakwenda kuteremka daraja. Ndanda FC ndiyo ilikuwa timu ambayo imepoteza mwelekeo zaidi baada ya uongozi wake kuonekana umepotea njia.

Kibaya zaidi, wachezaji wake wengi nao walionekana wamepotea na wamekata tamaa na hata kufikia kulalamika kwenye vyombo vya habari.

Baadhi ya mambo waliyolalamika ni kukosa hata fedha kwa ajili ya mlo. Yaani walikuwa kambini na walikuwa wakishinda njaa, kitu ambacho ni kibaya zaidi cha mwisho unapozungumzia kundi la wanadamu.

Mnaweza kukosa jambo jingine lakini si chakula ambayo ni huduma namba moja kwa mwanadamu. Lakini wachezaji hao walisema nafuu yao ilikuwa ni mlo mmoja kwa siku, jambo ambalo si zuri hata kulisikia na sikuwahi kusikia kiongozi wa Ndanda FC akilikanusha.

 Waliokuwa wakilalamika ni kati ya wachezaji wakongwe kabisa wa Ndanda FC na hata watu wa benchi la ufundi. Hili halikuwa jambo zuri lakini hongera kwao kwa kuwa walijitutumua na mwisho Ndanda FC ikabaki Ligi Kuu Bara.

Baada ya hapo, nilitegemea kuona wanajipanga. Ingawa jambo hilo halikufanyika mapema sana kwa kuwa inaonyesha hata usajili wa Ndanda FC haukuwa ule unaoonyesha kuna mabadiliko makubwa.

Huenda uongozi haukuwa na fedha na mipango haikuwa bora kuhakikisha fedha nyingi zinapatikana. Lakini baada ya dirisha la usajili kufungwa, nimeona kuna Kampuni Motsun Group Ltd kupitia ya bidhaa yake ya mabati ya Kiboko imejitokeza kuidhamini Ndanda FC.

Ndanda FC wamepata udhamini wa mwaka mmoja kuitangaza Kiboko. Hawakusema kiasi gani lakini tayari wameongeza kitu mfukoni mwao ambacho kitawasaidia kuwa tofauti na awali.

Lakini lazima ukumbuke kuwa Ndanda FC wanaingiza fedha kupitia wadhamini wa Ligi Kuu Bara, Vodacom pia Azam TV ambazo zinaweza zisiwe nyingi sana lakini zinasaidia gharama kadhaa za uendeshaji tofauti na zamani.

Msimu uliopita pia walipokea fedha kutoka Vodacom na Azam TV lakini wakashindwa kusimama na kufanya vizuri. Ujio wa Kiboko ni jambo jingine bora wanalopaswa kulitumia kama chachu ya mabadiliko.

Ninaamini Kiboko wangeweza kutodhamini katika soka na kwenda kwingine kujitangaza. Uamuzi wao kuingia kwenye soka lazima wapate faida na mafanikio yao na ikiwezekana wanaongeza mkataba ni kuona Ndanda FC inafanya vizuri.

Ndanda FC wasifurahie fedha tu wanazopata, badala yake wanapaswa kujua kwamba wadhamini wao pia kuna jambo wanategemea kutoka kwao na wakifurahia zaidi basi wataweza kuendelea na udhamini na ikiwezekana kuongeza zaidi, hili ninaamini linaweza kutokea.

Lakini anayeweza kulifanya litokee, ni Ndanda wenyewe ukianza na viongozi na wachezaji pia. Wanaposaidia lazima wajue wana deni la kumtangaza mdhamini wakiwa na mafanikio na ikiwezekana suala la nidhamu linapaswa kuwa juu zaidi ukilinganisha na msimu uliopita.

Kesho kama Ndanda FC itateremka daraja, maana yake watakuwa pia wamemshusha mdhamini wao kwa maana ya kwamba hatakuwa na nafasi ya kuongeza mkataba tena. Lakini wakifanya vema na ikiwezekana kufikia angalau ule uwezo waliouonyesha Mbao FC ya Mwanza msimu uliopita, huenda hata wadhamini wenye donge nono wanaweza kujitokeza zaidi.

Ndanda FC mna deni kubwa la kuonyesha tofauti kwa kuwa mwanadamu bora ni yule anayejifunza kupitia makosa yake. Kama msimu unaoanza wiki chache zijazo utaendelea kuwa wa shida kwenu, basi lawama zibaki kwenu na mtaonyesha ni watu wa kubahatisha mambo.


Fanyeni vizuri ili muwe sehemu ya kuwashawishi wadhamini wengine kwamba hata timu ndogo zinaweza kudhaminiwa na kuwatangaza vizuri wadhamini.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic