August 21, 2017



NA SALEH ALLY
WANACHAMA 1216 wa Klabu ya Simba, kwa pamoja wameamua kufanya mabadiliko ya katiba katika suala la uendeshaji wa klabu yao. Kumbuka Simba imezaliwa mwaka 1936.

Hakuna ubishi, Simba pia ilihitaji mabadiliko kupitia katika maisha mapya ya ushindani kwa kuwa hata baada ya kuzaliwa, ilipitia mabadiliko kadhaa kufikia hapa ilipo leo hii.

Mabadiliko yaliyofikiwa ni jambo la mpito wa maisha na wanachama waliofanya mabadiliko wanapaswa kujipongeza lakini wakiamini kuwa kuna hatua nyingi za kupitia kufikia kwenye mafanikio na ikiwezekana siku za usoni, mabadiliko mengine.

Mfumo wao unasema hivi; mabadiliko yaliyopitishwa na wanachama wa Simba yako hivi, wanachama watamiliki klabu yao kwa 50% huku 50% zikibaki kuwa za wawekezaji.

Wawekezaji watakuwa mmoja, wawili au watatu watatakiwa kutoa Sh bilioni 20 katika uwekezaji huo sawa na wanachama.

Kwa wanachama, kwa kuwa wanaonekana si wenye uwezo wa kutosha kifedha, wao watatakiwa kuchangia Sh bilioni 4 tu ambazo nia silimia 10 huku 40 ambayo ni bilioni 16 zitawekwa kando kwa kuangalia uwezo wao.



Suala la nani atakuwa mwekezaji itaundwa kamati baada ya watu kujitokeza, nayo itaandaa mkutano kuwaita wanachama kuwaeleza waliojitokeza katika uwekezaji ni akina nani.

Wawekezaji wanaweza kuwa wawili, watatu au vinginevyo na mgawanyo wa hisa kwa maana ya thamani na asilimia ndiyo utakaohusika.

Kitu kizuri zaidi ni kwamba wanachama wataendelea kuwa wamiliki wa klabu kwa asilimia 50 na ninachotaka kuwakumbusha kwamba hakuna kitu ambacho hakina matatizo.

Hii ni safari mpya, wameingia katika mabadiliko na kikubwa wanachopaswa ni kuendelea kujielimisha zaidi kuhusiana na mfumo huo ili kuweza kuutendea haki kwa ajili ya kujipatia maendeleo.

Nasisitiza waendelee kujifunza zaidi kwa kuwa wanapaswa kuhoji kuhusiana na mfumo huo, wanapaswa kuwapa wawekezaji changamoto zenye mlengo wa kujenga ili kufanikisha.

Wanachama wa Simba hawapaswi kuamini kwamba kwa kuwa wamefanya mabadiliko, basi wanapaswa kukaa kimya na kuacha mfumo ufanye kazi. Kuna mambo mengi ya kujifunza na kuyafanyia kazi ili mabadiliko yawe na maana.

Wawekezaji wanaokuja ni kina nani, kwa nini wanataka kuwekeza Simba, uwezo wao ni upi, wanaweza kusaidia nini. Historia yao kibiashara ilikuwaje na ikiwezekana ni vizuri kuhoji kuhusiana na nia yao ili kupata uhakika zaidi.

Kuingia katika mabadiliko ni kuingia katika changamoto mpya, kukabiliana nayo ni lazima kujielimisha zaidi kwa lengo la kutaka kujua mambo zaidi ili unapohoji unakuwa na uelewa zaidi wa jambo husika.

Ninaamini wako ambao wameshiriki katika mabadiliko hayo lakini hawakuelewa zaidi au hawakuelewa kwa asilimia 100. Huenda walifurahishwa na kusikia mabadiliko yataisaidia Simba kuwa imara zaidi.

Wako walioamini Simba ikiingia katika mfumo mpya, basi kazi yake itakuwa ni kushinda kila mechi, kuifunga Yanga kila siku na hakuna atakayeifunga tena Simba.

Ninaamini wako wamefanya hivyo kwa kuwa wanaitafuta furaha ya ushindi na kufanya vizuri wakitaka kuyakwepa maumivu ya kufungwa au kupoteza na kuzomewa na watani wao Yanga na wengine.

Haya yote yanaweza kuwa sawa lakini kwa kila mwanachama aliyehusika kupitisha mabadiliko hayo jana, namuasa kukumbuka kujifuza zaidi au kuhoji zaidi kuhusiana na mfumo huo ili awe sehemu ya mabadiliko kwa sehemu ya kuyapitisha lakini kuyasaidia yafanye kazi akiwa anaelewa kwa nini alifanya mabadiliko.

Kwa upande wa viongozi, wasiwe na jazba, wawape nafasi wenye hamu ya kuhoji wafanye hivyo. Wajibiwe kwa mlengo wa kujenga, si jazba au kuwadhalilisha kwa kuwa wengi walitaka.


Mtu mmoja amekataa katika mkutano wa jana ana haki, hivyo bado wako watakaopenda kuhoji nao wasaidiwe kujua ingawa nao walenge mafanikio badala ya vurugu. Kila la kheri.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic