October 18, 2017

SINGIDA UNITED

Na Saleh Ally
IKITOKEA Simba imepata sare na timu yoyote ile ya Ligi Kuu Bara, gumzo kubwa linakuwa ni kuhusiana na thamani ya kikosi chake.

Imeelezwa kuwa kikosi cha Simba kilifanya usajili wenye thamani ya Sh bilioni 1.3. Kama unakumbuka, msimu huu Simba walifanya mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kusajili zaidi ya wachezaji 10 ikiwa wamepania kurekebisha kikosi chao.

Gumzo la kikosi limekuwa ni jambo kubwa zaidi kuliko hali halisi kwamba timu zinazokutana na Simba zinaonyesha soka la kuvutia au la uhakika na kutoa upinzani sahihi.

Hakuna hata mmoja anayejaribu kufikiria kwamba, kuanza kujitokeza kwa wadhamini wengi katika Ligi Kuu Bara na klabu zenyewe, kumechangia ushindani mkubwa ingawa bado linakosekana suala la weledi kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa kuwashawishi zaidi wadhamini na kuwafanya waamini kile wanachotoa kitawapa kile wanachohitaji.

Unaona msimamo wa ligi ulivyo sasa unaweza ukawa unakupa majibu ya kitaalamu zaidi. Kuwa ligi hii hadi sasa ina kiwango cha juu kutokana na pointi na tofauti ya timu na timu.

Wanaoongoza ligi ni Simba, wana pointi 12, wanaowafuatia hadi timu ya nne ukianza na Mtibwa Sugar, Yanga na Azam FC kila timu ina pointi 12 kama za Simba na tofauti ni GD, yaani tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa pekee.

Maana yake timu nne zilizo juu katika msimamo wa ligi pointi zote ni sawa. Timu ya tano ambayo ni Singida United ina pointi 11 na Prisons iliyo nafasi ya sita ina pointi 10. Maana yake tofauti kati ya timu iliyo katika nafasi ya sita na inayoongoza ligi ni pointi mbili tu.

Hii ni baada ya kila timu kucheza mechi sita, takribani robo ya ligi na hii inatengeneza mwendo kwamba ligi hii si rahisi tena na inakuwa vigumu kutabiri nani atakuwa wapi kwa kipindi gani.

Lakini unaona kabisa ugumu umejengwa na ubora unaoongezeka na haya ni majibu kwamba pamoja na kuwa wachezaji wanajituma lakini wapo wanaolipwa mishahara kwa wakati, wapo walioongezewa na kuna timu zimejipanga kutokana na kuwa na wadhamini wa kutosha mfano wa Singida United.

Kuongezeka kwa Singida United kunatoa jibu sasa, kwani unaiona ni kati ya timu tano zilizo juu ya msimamo na unaona baada ya timu tano kuna ushindani mkubwa unakuja kutoka kwa timu nyingine kama Prisons, Mbeya City, Ndanda na Mbao FC.

Hii inafanya kuwa moja ya ligi bora kama ushindani wa namna hii utaendelea kuwa hivi na ushindani usibaki kati ya Yanga na Simba pekee. Au timu zisiwe bora inapofikia zinacheza na Yanga au Simba pekee.

Kuwa na ligi bora hata kama utaangalia mechi kati ya Ndanda dhidi ya Majimaji au Stand United dhidi ya Kagera Sugar upate ladha ya ushindani inayozalishwa na ubora sahihi.

Soka ni mchezo wa hesabu, mwisho majibu yake hutengenezwa na hesabu baada ya mechi kuchezwa kwa hesabu. Mwisho msimamo pia huwa na hesabu, maana yake tutapata bingwa, nafasi ya pili, ya tatu lakini tutajua waliosalimika na walioteremka.

Lakini pamoja na yote hayo, tukubaliane jambo moja, kwamba marekebisho kutoka kwa waamuzi kuanza kupunguza mambo yao ya kutokuwa makini yamechangia mabadiliko na ushindani ambao tunaupata sasa kwa kuwa timu zinalazimika kushinda kwa ushindani wa haki badala ya upendeleo, ushabiki au kuangalia ukubwa wao.

Lakini imepunguza uonevu ambao baadhi ya timu za mikoani zilikuwa zinafanya kwamba timu yoyote inapokwenda kucheza dhidi yao hasa zile ambazo si kubwa basi lazima ziache pointi bila ya kujali uwezo wa wenyeji.

Kama wenyeji wanazidiwa, basi waamuzi wanakuwa upande na sehemu ya kikosi kama ambavyo tunaona katika Ligi Daraja la Kwanza ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza.

TFF wanatakiwa kulifanyia kazi kwa kuwa walichokifanya katika Ligi Kuu Bara, haya ndiyo majibu na wanatakiwa kuendelea kushikilia kwa kuwa ligi kama hii ndiyo tunayoitaka na itasaidia kwa kiasi kikubwa mabadiliko na maendeleo ya wachezaji na wanamichezo wenyewe na itaendelea kuwashawishi zaidi na zaidi watu kuingiza fedha zao katika soka na si kwa timu chache, badala yake karibu kwa kila timu inayoshiriki ligi hiyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic