December 16, 2017




Na Saleh Ally
UNAWEZA kuidharau Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, kwa kuwa si maarufu sana nchini, huenda kutokana na lugha yao.

Wapo wanaoamini timu pekee ni Bayern Munich katika Bundesliga jambo ambalo si sahihi kwa kuwa tumeona timu za Bundesliga ambavyo zimekuwa zikifanya vizuri.


Wahusika wakuu katika Bundesliga wanalijua tatizo lao, wanasema kwamba kuna wakati takriban miaka 10 iliyopita ligi yao haikuonyeshwa kwenye runinga barani Afrika.

Wakati huo ndiyo walitoa nafasi kubwa kwa Premier League ya England pia Bundesliga kupaa na kuwa maarufu sana licha ya kwamba ligi yao ina mpangilio bora wa kiushindani na kadhalika.

Bado wanaamini huu ni wakati mwafaka wa kuirejesha Bundesliga katika chati ya juu kwa kuwaeleza watu kilichopo na zaidi watatoa nafasi kubwa kwa Bara la Afrika watu waishuhudie.


Kwa Tanzania, mashabiki wa soka wanafuatilia ligi hiyo kupitia ving’amuzi vya StarTimes ambavyo hurusha mechi za Bundesliga moja kwa moja kupitia chaneli zake.

Ukiangalia msimamo unavyokwenda, huenda wale wanaofikiri Bayern ni pekee unaweza ukawa unatoa jibu hilo. Lakini kwa maana ya burudani, Bundesliga ina burudani nyingi, mpangilio mzuri na ustaarabu kwa mashabiki wanaokwenda uwanjani kwa kuwa wanajua wanafuata burudani tofauti na nchi nyingi za Ulaya.

Bayern Munich inaongoza msimamo wa Bundesliga ikiwa na pointi 38 baada ya kucheza mechi 16 na kufuatiwa na Schalke 04 yenye pointi 29 na RB Liepzig ina 28.

Msimamo unaonyesha bado kuna ushindani kwa kuwa tofauti ya pointi tisa haina tofauti na ile ya Premier League ambayo Man City wanaongoza kwa tofauti ya pointi 11.

Burudani kubwa ya Ujerumani, pia kuna tofauti sana na kwingine. Mfano, utaona Premier League washindani zinabaki timu tano au sita tu na lazima nafasi ya kwanza hadi ya tatu ziingie timu zilezile.

Mfano, Manchester United, Arsenal, Chelsea, Man City, Liverpool na Totteham. Ujerumani timu nyingi zisizotegemewa hupata nafasi ya kuingia nne au tano bora na zikafanya vizuri. Karibu kila mwaka kuna timu zinazofikia katika sehemu ambayo haikutarajiwa tofauti na Hispania katika La Liga.

Kilichowafanya Wajerumani wajisahau ni ubora wa ligi yao wakiangalia na kwingine kama mpangilio, ukubwa wa viwanja, umiliki wa timu, viwanja vya kisasa zaidi na kadhalika.



Utaona Bundesliga ndiyo inaongoza kwa kuingiza watu wengi na Borussia Dortmund imekuwa ni timu kinara kuliko nyingine zote.

Lakini sapoti kubwa ya mashabiki wengi sana ndani ya Ujerumani, pia waliona ni kama inatosha ingawa sasa kibiashara wanaona kuwa kweli wanaihitaji Afrika, Asia, Amerika Kusini na kwingineko.

Hivyo, lazima Wajerumani waufanye mtihani huo pamoja na ubora wao uweze kusambaa na kutanua soko lao kwa kuwa hawawezi kubaki na soko la Ujerumani au Ulaya pekee.
Soko pia hutegemea idadi kubwa ya watu na utaona Afrika, Asia na Amerika Kusini ni sehemu zenye watu wengi sana, tena wanaopenda mpira.

Tayari mkakati wa makusudi wameuanzisha Bundesliga, wameanza kufanya kila linalowezekana kuona wanafikia katika sehemu ambayo watakuwa na ushindani wa juu.
Katika mahojiano na gazeti hili mjini Koln, Ujerumani, baadhi ya maofisa wa Bundesliga wailiambia SALEHJEMBE kuwa pamoja na kuanza mkakati huo, wanajua haitakuwa safari ya muda mfupi.



Wanasema, wanajua itachukua muda mrefu kidogo kufikia malengo yao kwa kuwa Premier League na La Liga zimejiwekeza vizuri na mizizi yao imefika mbali.
Hivyo ni suala la kuendelea kuelekeza kwa muda tena na tena hadi hapo mambo yatakapokuwa mazuri na wao kuanza kujulikana kwa hali inayotakiwa.


Bundesliga wanataka kutoa pia nafasi ya kuona ligi yao inaonekana sana katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania, lakini wanataka kutoa nafasi kwa watu kwenda na kushuhudia Bundesliga kwa kuwa kama wakiipata nafasi hiyo watatambua ubora wa ligi hiyo.


Kwa yeyote ambaye amewahi kupata nafasi ya kushuhudia Bundesliga moja kwa moja uwanjani, kamwe hawezi kupinga kuhusiana na ubora wao kwamba ni moja ya ligi bora na si kitakwimu tu uwanjani kama ilivyo.


Lakini hata ushangiliaji, idadi ya watu inayokwenda uwanjani kwa wastani pia ushindani wa timu na timu na wakati mwingine upinzani wa mashabiki ambao ni mkubwa lakini uliojaa ustaarabu.



Kushituka kwa wahusika wa Bundesliga ambao walikaa na ubora wao na kuuacha katika wigo finyu, ni funzo kwa ligi nyingine ambazo huenda zinaweza kujisahau na kuona zilipo, hakuna anayeweza kufikia.

Wajerumani wana “pumzi” ya mambo yao wanapokuwa wanahitaji mafanikio ya jambo fulani kwa kuwa wao ni watu wenye tabia ya kuhakikisha wanatimiza kiu ya malengo yao. Hivyo hili linaweza kuchukua siku nyingi, lakini uhakika siku itafika na Bundesliga itakuwa gumzo na maarufu zaidi ya leo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic