March 19, 2016


Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Burundi na baadaye Kenya, Adel Amrouche amesema amekuwa akivutiwa na mashambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib.

Lakini akatoa mambo mawili makubwa ambayo Ajib anapaswa kuyafanya ili kuwa mshambuliaji bora kabisa.

Amrouche raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria, amesema Ajib anatakiwa kufanya zaidi mazoezi ya kuongeza nguvu na ikiwezekana kidogo ukubwa wa mwili.

"Kwanza nguvu, bado hana nguvu ya kupambana na mabeki imara. Pia anaweza kuongeza kidogo mwili lakini isiwe sana kwa kuwa itaua kasi yake," alisema Amrouche alipozungumza na SALEHJEMBE kutoka Ubelgiji huku akisema amekuwa akishuhudia mechi kadhaa za Ligi Kuu Bara kupitia mtandao maalum.

"Nafuatilia sana soka ya Tanzania, pili inabidi awe ni mtu anayelenga nini anachotaka kufanya. Kwa mchezaji anaweza kuwa anakwenda mbele huku akiwa na uamuzi wa mambo mawili. Naona kama anafanya hivyo mara kadhaa, utaona anapoteza mipira.

"Lazima awe amelenga kitu fulani kwanza, kikishindikana atahamia kwenye plani ya kitu cha pili. Hii itamsaidia kuwa bora lakini mazoezi ya kutosha akiwa fiti, hilo ni jambo la lazima," alisisitiza Amrouche.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV