March 21, 2016


MECHI ya jana kati ya Yanga dhidi ya APR huenda itakuwa ni daraja lingine katika mpira hapa nyumbani. Kwanza kwa wale ambao ni waungwana na hawataki ushabiki kwenye ukweli, watakubaliana nami kuwa Yanga iliboronga.

Wale ambao wanaupenda mpira na wanaamini kuangalia ukweli ni sehemu ya njia ya kufanya vema, watakubaliana nami Yanga ilicheza kiwango cha chini kabisa na zile mbwembwe za “Kampa, kampa tena” hazikuwepo kabisa!

Yanga ilianza kwa kushinda mabao 2-1 ugenini dhidi ya “Watoto wa Shule” wa APR. Katika mechi hiyo jijini Kigali, Rwanda kila kitu kilikuwa wazi kabisa kwa sababu APR walionekana waoga kwa kuwa wanakutana na timu kubwa kwao.

Lakini katika mechi ya juzi, mambo yalibadilika. APR ambayo ina wachezaji wengi wanafunzi wa shule ya sekondari ndiyo walionekana wenyeji. Wakapata bao la mapema kabisa na wao ndiyo wakaonyesha soka la uhakika.

Hakuna ubishi kwamba mashabiki wa Yanga na mashabiki wazalendo wa Utanzania walikuwa na hofu kuu kuanzia dakika ya kwanza hadi 90. Lakini bahati nzuri Yanga imefuzu. Hapa ni vizuri kuelezana ukweli kwa kuwa Yanga sasa inakwenda kukutana na Al Ahly ya Misri.

APR wametoka lakini wamewaachia somo kubwa Yanga na Tanzania kwa ujumla, kwamba bado vijana wanapaswa kuaminiwa.

Kikosi cha APR kilikuwa na wachezaji wote Wanyarwanda, hakuna hata mgeni mmoja. Mkongwe ni kipa Jean Calude Ndoli na mshambuliaji aliyekuwa benchi. Waliobaki wote ni vijana waliokuwa kwenye akademi ya APR.

Akademi ya APR iko katika eneo la Kimihura ambayo kuna Shule ya Sekondari ya Ape Rugunga. Kumbuka hata aliyeifunga Yanga juzi, Fiston Nkinzingabo ni mwanafunzi wa sekondari hiyo. Kwa sasa APR wanakuza vijana ambao watakuwa msaada kwao na Rwanda kwa ujumla.

Kusema Yanga ianze kusajili sasa itakuwa uongo, lakini tunagundua kwamba vijana wakipewa nafasi na kulelewa vizuri basi wanakua na makuzi bora ya kisoka na watakuwa msaada baadaye.

Yanga au timu yoyote ya Tanzania haitakuwa na nafasi ya kuitoa APR katika michuano yoyote ya Caf miaka mitatu ijayo. Kwa kuwa watakuwa na timu kweli. Hivyo basi, tusiache mafunzo hayo yakapita kiulaini, tuyatumie na ikiwezekana yafanyiwe kazi mara moja, si maneno maneno tu.

Kitu kingine, tukirejea katika mechi hiyo unaweza kuona kama Yanga walikata tamaa kabisa baada ya APR “kushika nchi” licha ya kuwa ugenini.

Tena unarudi katika mechi ya Kigali, pamoja na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya APR ugenini, lakini mimi nasisitiza, bado Yanga haikuonyesha soka la kutikisa au kutisha. Awali nilifikiri wako ugenini na mambo mazuri yatakuwa nyumbani lakini nako wameshindwa kuonyesha cheche.

Hivyo wanachotakiwa kufanya Yanga kwa sasa ni kuamini mechi ya APR imepita kwa kuwa wamefuzu. Lakini lazima wakubali kwamba kwa kuwa ni hivyo, maandalizi ya kuwavaa Al Ahly lazima yawe na uzito kama uzito wa Waarabu hao.

Kama itajirekebisha, Yanga ina nafasi ya kucheza vizuri dhidi ya Al Ahly na kufanya vema, hili linawezekana. Lakini kama Yanga itazubaa, basi lazima ijue mzigo unaokuja utakuwa ni mzito zaidi kuliko ule wa APR.

Kuitoa APR kwa shida, hakuna maana hata kidogo Yanga haiwezi kufanya vizuri dhidi ya Al Ahly. Tena kwa wachezaji ndiyo hawapaswi kuliweka hilo kichwani maana litawafelisha.

Badala yake lazima wajue kila mechi ina mipango yake na inafanya kazi kwa njia zake. Wakiamini wanaweza, kweli itawezekana. Wakiona ni ngumu haitafanikiwa, basi itakuwa hivyo na ubabe wa Waarabu kwao, hautaisha milele.


4 COMMENTS:

 1. Salehe hata jean claude Iranz aliyeanza kuichezea APR mwaka 2012 naye pia ni wa academ?!Duh kama ni hivyo basi Academ ya APR ina wachezaji wazee!
  Acha ukanjanja fanya tafiti kabla ya kushika kalamu,ninachojua mimi Yanga haina uchezaji wa kupigania magoli na hilo wote mnalitambua kwani ilishindwa kuifunga Simba kwa magoli mengi licha ya kupata nafasi zaidi ya 8.

  ReplyDelete
 2. Yanga hawana timu ya kuwatoa waarabu hata kwa karne nzima ijayo,hilo linajulikana.Tatizo si kutumia vijana au Academi kwani pamoja na timu za Ulaya kuwa na maacademi kibao bado zinatumia mabilioni ya pesa kusajili wachezaji wazuri toka sehemu zingine.Nani angeweza kuamini kama Barcelona ingewasajili Suarez,Neima,Raktic nk wakati wana vijana wenye vipaji kibao?Hiyo yote ndio jitihada za makocha kutaka ushindi wakati uliopo na si kutegemea wakati ujao kama mzee Wenga ambaye naye sasa kabadilika kwa kuwasajili majembe akina Ozil,Sanchez,Salehe Metodo nk.
  Hata huyo Joseph anayetarajiwa kwenda O?Trafford atasajili wachezaji wakubwa kwanini hasiwaamini akina Rashid(Rashfod) anayewafungia magoli hivi sasa ambaye ni mwanafunzi?
  Fanya tafiti kaka si kukurupuka na kuanza kuandika tuu,hakuna kocha anayetaka matokeo mabovu ila huo ndio uwezo wa timu yao!

  ReplyDelete
 3. Mimi naamini kila game ina game plan Yake!! Tatizo waandishi wa tz mnaandika kwa matukio!! Yanga waliposhinda Amohoro kila mtu alisifia leo kutoa droo imekuwa kosa!! Yanga walikuwa wanabadilika kutokana na wakati kama mwl alivyosema!! Baada ya kufungwa goli walibadilika na kuanza kushambulia na baada ya kupata goli wakatulia ili kutoruhusu magoli ya kijinga!! Mpira magoli na sio kushambulia!! Yanga waligonga mwamba na kukaribia kufunga kwa faulo mara mbili lakini bado APR ndo wanaonekana walikaribia kushinda!!? APR ilifukuza wacjezaji wa kigeni miaka mitatu iliyopita baada ya kuona hipati mafanikio ambayo hadi sasa hawajawahi pata maana ni mara ya tatu wanatolewa round ya kwanza!! Leo unasrma miaka 3 baadae!? Sio wote ni watoto kama mnavyowachukulia,Hata akina mwaishuya na matteo wangekuwa shule leo si wangekuwa sekondari!?

  ReplyDelete
 4. Niseme ya kwamba wakati umefika tubadilikeni watanzania.Hata kama game ingelikwisha kwa penalties la maana ni umefanikiwa kwenda level ya juu zaidi.Mpira unamambo mengi jana c leo na leo c kesho hivyo tuwape hongera kwa kusonga mbele,kilichobaki ni kutoa mikakati ni kipi kifanyike kama washabiki wa soka ili uongozi uweze kufanyia kazi nasi kuanza kutuonesha wasiwasi ulionao to the coming next game.Sio siri hii yanga inatisha kuifunga APR kwao ni shida mpira hauna utoto na ukiwaangalia hao APR wako vyema Physic pamoja na intelligence ya mpira hivyo kusema ni wa shule sidhani kama inasound better kama football analyst.nimalize kwa kusema kwamba huu ndo wakati wa yanga kuionesha al ahly kwamba east africa football isn't as what they think about.YANGA,AZAM PAMOJA TUTASHINDA

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV