March 14, 2016

KERR
Aliyekuwa Kocha wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, bado anaifuatilia Ligi Kuu Bara na amesema kutokana na Yanga na Azam kushiriki michuano ya kimataifa, Simba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Kerr aliiacha Simba ikiwa nafasi tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, kwa sasa timu hiyo ndiyo inaongoza ligi.

Yanga na Azam juzi Jumamosi zilishinda mechi zao za kimataifa, Yanga iliifunga APR ya Rwanda mabao 2-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam ikiichapa Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 3-0 katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kerr anaamini Yanga na Azam zitakuwa zikitolea macho zaidi michuano ya kimataifa huku wachezaji wake wakitumika sana na hiyo ndiyo itawafanya Simba kufanya vizuri na hatimaye kuwa mabingwa.

“Unapokuwa unashiriki michuano mingi, mara chache sana unaweza kufanikiwa kufanya vizuri kote, lakini timu nyingi hushindwa kumudu na kujikuta zikipoteza kote.

“Hali hiyo kwa sasa ndiyo wanayo Yanga na Azam ambazo zinawania ubingwa wa ligi na Simba, zenyewe zinashiriki michuano zaidi ya miwili wakati Simba yenyewe inashiriki miwili tu (ligi na Kombe la FA), kwa maana hiyo naona kabisa Simba ndiyo ina nafasi kubwa ya kuwa bingwa wa ligi msimu huu kuliko hizo nyingine,” alisema Kerr.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV