March 18, 2016



MURO

Na Saleh Ally
Juzi Jumatano, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Simba, Haji Manara, alielezea masuala mengi yanayohusiana na kuonyesha Simba ndiyo klabu pekee iliyofanya vizuri zaidi kimataifa.

Manara alieleza mengi kuhusiana na Simba ilivyokuwa ya kwanza kuvaa viatu, kununua basi, kuvaa suti na kupanda ndege na pia yenye mafanikio zaidi kimataifa.

Lakini Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga na msemaji wa klabu hiyo, Jerry Muro, anasisitiza kwamba Simba ni “Wa matopeni tu”.

Amesema anaamini hata data zilizozagaa mitandaoni zinazoonyesha Simba ndiyo timu bora zaidi unapozungumzia kimataifa, huenda zimepikwa kwa kuwa Yanga ndiyo klabu bora zaidi kwa sasa hapa nchini.

SALEHJEMBE: Kwa nini unaona Simba ni wa matopeni na jina hilo huoni kama ni kashfa kwa watani?
Muro: Kashfa kivipi, wao ni wa matopeni kwa kuwa wapo tu. Wanacheza hapahapa, hawachezi kimataifa na sasa zaidi ya misimu mitatu na harufu inanukia hata msimu huu watabaki hapahapa.

SALEHJEMBE: Hujaona rekodi zinaonyesha Simba ndiyo timu bora zaidi unapozungumzia kimataifa?
Muro: Data zimetolewa na nani, uhakika uko wapi na Simba haijacheza mechi za kimataifa sasa ni msimu wa tatu, huo ubora wanautoa wapi hadi iwe timu ya kujisifia na kusema ni bora?

MANARA
SALEHJEMBE: Takwimu zinaonyesha ni za kipindi chote kabisa, inajumlisha muda wote. Hapo ndipo Simba inaizidi Yanga, hivyo huoni unapaswa kuwapa heshima yao Muro?
Muro: Siwezi kutoa heshima kwa wa matopeni, tena nisikilize nina hoja hii hapa. Kama Yanga imechukua ubingwa mara 25 kati ya mara 50, vipi Simba iwe imeshiriki mara nyingi wakati bingwa anakwenda katika michuano ya kimataifa?

SALEHJEMBE: Umesahau kidogo, bingwa na mshindi wa pili ndiyo wanashiriki. Sasa Simba inaweza kuwa imeshika nafasi ya pili mara nyingi. Ikashiriki michuano ya Klabu Bingwa wakati huo, pia kulikuwa na Kombe la Washindi baadaye Kombe la Caf ambalo walifika fainali. Tena inaonyesha wao walikuwa wanafika mbali kidogo, Yanga ni hatua za awali tu nje. Umeelewa?

Muro: Hakuna lolote, pale klabu tumeingia kwenye mtandao wa Caf kupitia akaunti maalum. Inaonyesha hata wao Caf wameweka timu 10 Bora. Hakuna hata moja ya Afrika Mashariki, Simba wanabaki kuwa wa matopeni tu, Manara pia analijua hilo.

SALEHJEMBE: Vipi wewe kila kitu Manara, hivi katika hali ya kawaida, una ugomvi na Manara?
Muro: Hata kidogo, haijawahi kutokea lakini kila mtu yupo kazini kwake.

SALEHJEMBE: Lakini amekuwa akilalamika unamtukana, unatukana viongozi wake, nafikiri hilo si sahihi, unaonaje ukirekebisha?
Muro: Nijirekebishe nini, sijawahi kumtukana na yeye anajua. BMT walitaka kutusuluhisha, lakini nao walipomuuliza Haji kasema eti nimewatukana kwa kuwaambia wa mchangani.

SALEHJEMBE: Nasikia mna ugomvi binafsi, mlikopana mwisho mkasigana?
Muro: Hilo lilitokea kule Zanzibar, ingawa nisingependa kulizungumzia, lakini kabla, Haji tulikuwa tunazungumza vizuri sana. Hadi nilimkopesha shilingi laki moja. Hili ni jambo la kawaida kabisa ila kulipa ikawa matanga.

SALEHJEMBE: Sasa ugomvi ukatokea wapi sasa, ulidai kwa nguvu?
Muro: Mambo yalizidi kuwa magumu, ilifikia hadi (Geoffrey Nyange – Makamu wa Rais Simba) Kaburu akaingilia, ni mimi ndiye nilimwambia baada ya kuona mambo hayaeleweki.

SALEHJEMBE: Ok, sasa ikawaje?
Muro: Nikamueleza Kaburu, naye akamuita Haji pale, basi Kaburu akatoa fedha “tap tap tap”, akahesabu laki akamlipia Haji.
 

KABURU kamlipia Manara. Je, Manara mwenyewe analizungumziaje hilo? Muro kama alilipwa, nini sasa kinasababisha wasielewane na msemaji mwenzake? USIKOSE KATIKA MAKALA YA KESHO AMBAYO ITAELEZA KILA KITU HUKU HAJI NAYE AKIWEKA MAMBO HADHARANI.

SOURCE: CHAMPIONI

3 COMMENTS:

  1. JAMANI MSIWACHONGANISHE HAO WATOTO BADO WANAHITAJI MSAADA WA WAKUBWA WAO KATIKA KUFIKIA MALENGO.WAACHENI WATATULIA WAKIKUA HAO

    ReplyDelete
  2. Nijuavyo mimi,Hajji manara ni mgumu kulipa deni,kumbuka hadi alifikishwa polisi kwa kosa la wizi wa kuaminiwa alipoazimwa gari na rafiki yake,ndivyo alivyo huyo kama ana katabia cha utapeli fulani na ukizingatia rangi ya ngozi yake wengi wanaogopa kumfata na kudai madeni yao kwa kuchelea kuambiwa vinginevyo!

    ReplyDelete
  3. Inaonekana Muro hana analojua juu ya soka na hata juu ya Simba na Yanga, huenda huyu jamaa anaijua Yanga ya Manji tu, hajui hata kama kulikuwa na kombe la Muungano, mara nyingi majibu yake si ya mtu mweredi wa mambo. Ubora wa Simba kwa rekodi za jumla Kimataifa ziko wazi ukilinganisha na Yanga, hata mzee Akilimali anajua vizuri. Pili, atambue kuna rekodi za kushiriki mashindano na rekodi za mafanikio katika mashindano husika. Arejee rekodi za Simba na Yanga pale CAF nadhan zitamjengea weledi zaidi.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV