March 19, 2016

AL SIYABI AKIWANOA MAKIPA WA SIMBA MWAKA JANA ALIPOKUJA NCHININa Saleh Ally
WIKI chache zilizopita, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alimueleza Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa kwamba shirikisho hilo linapambana, baada ya miaka 10 ijayo, Tanzania ishiriki Kombe la Dunia.

Mmoja wa wadau wakubwa wa soka nchini ni Haroon Amur Al Siyabi. Huyu ni kocha wa makipa wa timu za taifa za Oman na asili yake ni Tanzania.

Al Siyabi, mkufunzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambaye ni mwajiriwa wa Shirikisho la Soka la Oman (Ofa), amekuwa akija nchini kusaidia kuinua viwango vya makipa wa Simba na wengine. Anasema miaka 10 ni michache na mambo mengi hayajafanyiwa kazi.

 Katika mahojiano yake na SALEHJEMBE, Al Siyabi ameliambia gazeti hili kutoka Oman. TFF haitaweza kutekeleza ahadi hiyo waliyomueleza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuwa hawajafanya mambo muhimu ya msingi.

1. Soka mashuleni:
“TFF wamesema ni programu ya miaka 10 ili waweze kucheza Kombe la Dunia. Lakini hakuna mafanikio hayo bila ya kuwa na michezo mashuleni tena katika shule nyingi kwa wigo wa kutosha ili kutengeneza vijana wakiwa makinda ambao watakuwa katika malezi ya soka,” anasema Al Siyabi.

“Hili ni muhimu sana, kwa kuwa soka ya Tanzania haiko katika shepu nzuri. Watoto mashuleni wangekuwa chachu kubwa”.


2. Hakuna makocha Bora:
“Hakuna anayeweza kukataa kwamba Tanzania hakuna makocha bora. Timu zote kubwa zilizo nafasi ya kwanza hadi za chini zinafundishwa na makocha wa kigeni.

“Angalia hata kocha wa timu ya taifa sasa anatokea Yanga lakini alikuwa kocha msaidizi. Tanzania haiwezi kuwa na ndoto ya kucheza Kombe la Dunia wakati haina makocha wazalendo watakaoendeleza soka nyumbani. Wageni wanaweza kuchangia lakini wenyeji kwanza. Ziko wapi kozi bora za makocha wa nyumbani?” Anahoji Al Siyabi.

3. Klabu na vijana:
“Vijana wanakuzwa kwenye klabu, si timu ya taifa. Klabu ngapi zina timu bora kabisa za vijana ambazo zina uhakika wa kutoa nyota wa soka wenye malezi sahihi?

“TFF haikuzi vijana, lakini tayari ingekuwa na programu sahihi na kusimamia hilo. Vijana wanahitaji muda na ndiyo maana nasema miaka 10 ni michache.”

4. Ligi ya Vijana:
“Ligi ya vijana itasaidia kuwapa uzoefu, kujiamini na mwisho itakuwa rahisi kuvumbua vipaji vyao.  Kama huna ligi bora ya vijana, usitegemee kuwa na kikosi bora cha timu ya taifa.

“Suala la ligi ya vijana ni la TFF na kama kweli ina ndoto ya kucheza Kombe la Dunia. Ni lazima kuisimamia, la sivyo itakuwa ni kupiga hadithi tu.”

5. Wachezaji 7 wa kigeni:
“Kwangu naona ni ndoto itakayoishia hapo ilipo. TFF inawaza kuboresha ligi na viwango vya wachezaji wakati imeruhusu wachezaji saba wa kigeni. Hili si sahihi hasa kwa maendeleo ya soka.

“Ligi ya Tanzania sasa inatumika kuboresha ligi za wengine. Lazima TFF ipunguze idadi ya wachezaji wa kigeni. Unataka kwenda Kombe la Dunia ukiwa na wafungaji karibu wote wa kutoka nje ya Tanzania. Mabeki wengi bora kutoka nje ya Tanzania. Hili haliwezekani hasa kwa nchi ambayo inachipukia kisoka.”

6. Wangapi wanacheza nje?
“Tanzania ina wachezaji wangapi wanaocheza nje ya nchi. Ambao watakuwa msaada kwenye timu ya taifa?

“TFF pia inapaswa kushirikiana na klabu kuhakikisha wachezaji wanakwenda nje. Ifanye hivyo ikijua haohao watakuwa msaada kwa timu ya taifa.

“Kusaidia kwake inaweza kualika mawakala, inaweza kushirikiana na mashirikisho ya nchi zilizoendelea kisoka na kuomba kama kuna nafasi wachezaji wa klabu kwenda kujifunza. Lakini kuwa karibu na klabu kwa kushirikiana na kuangalia hilo litatatuliwa vipi kwa kuwa ni faida kwa taifa likifanikiwa.”


7. Programu ya maendeleo ya wachezaji na makocha:
“Iko wapi programu ya maendeleo kwa wachezaji na makocha wa klabu za Tanzania?

“Inahitajika kwa kuwa itakuwa na nafasi ya kuwabadilisha kiufundi, kuwajenga kisaikolojia na hali ya kujiamini zaidi.

“Kazi ya TFF pia ni kuziinua klabu zake zikiwemo zile zinazoshiriki michuano ya kimataifa. Lakini kualika wataalamu kutoka katika klabu mbalimbali kubwa ambao watatoa mafunzo kwa wachezaji na makocha. Lini limefanyika hilo, lipo?


“Kabla ya kufikia ndoto hizo za Kombe la Dunia, hakika TFF inahitaji wataalamu kwa upande wa wachezaji, makocha na hata madaktari wa michezo. Hii si safari ya kuota tu, badala yake inatakiwa kufanyiwa kazi kwa upana,” anasema Al Siyabi.

1 COMMENTS:

  1. Wewe saleh na wenzako wote ni hovyo,toka lini Oman ilishacheza kombe la dunia hadi hicho kikufunzi kianze kuwabeza makocha wa TZ?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV