March 18, 2016



Na Saleh Ally
SHOMARI Kapombe ni kati ya wachezaji wanaoweza kuwa mfano zaidi ya ule wa kawaida unapozungumzia mpira wa soka hapa nyumbani.
Mara nyingi ninapowazungumzia washambuliaji, zaidi ananivutia Amissi Tambwe kutokana na mambo mengi sana, maana huwa ninakwenda hadi nje ya uwanja.

Tambwe ni mtaratibu, asiyependa makuu lakini ni mtu anayependa kufanya kazi yake kwa ubora wa juu na mafanikio. Tumeona, hata hajamaliza misimu mitatu tayari ana mabao 50 kwenye Ligi Kuu Bara.

Kati ya mabao hayo, 30 amefunga akiwa na Yanga ambayo alijiunga nayo baada ya kutemwa na Simba baada ya kuwafungia msimu wa kwanza mabao 19, msimu uliofuata akacheza mechi tatu na kufunga moja. Jumla 50.

Kapombe ni Mtanzania, lakini ni mchezaji mwenye dalili zote za kufika mbali zaidi. Kwa kuwa anataka kufanikiwa na anatambua soka kwake ni nini.


Ukibahatika kuzungumza naye, utagundua kuna kitu anataka na aina ya utafutaji wake inaingia kwenye kundi la wanaotaka kufanikiwa kwa dhati.

Angalia wachezaji wa Azam FC au Taifa Stars wanapokuwa mazoezi. Kuwa makini na taswira zao, utagundua ni mtu aliye makini na anataka kitu fulani.

Wakati fulani niliwahi kuandika kuhusiana na upungufu niliouona kwenye kambi ya Taifa Stars nchini Afrika Kusini. Nikasema sikufurahishwa na wachezaji wa Azam FC kuchelewa basi, kuchelewa ndege. Hakika hadi leo nasisitiza halikuwa jambo zuri hata kidogo na Kapombe alikuwa mmoja wao.


Huenda ni moja ya kasoro chache anazopaswa kurekebisha, huenda anatakiwa kuepukana na “nguvu ya kundi” awe tayari kuwaambia wenzake kama anaona wanakosea, hata kama wako wengi.

Ukiachana na tofauti kama hiyo, lakini Kapombe amekuwa mchezaji anayepanda kwa kasi. Utaona katika kipindi hiki kuna kipimo bora kabisa katika ushindani wa namna katika nafasi ya beki wa kulia.

Juma Abdul wa Yanga yuko vizuri. Hassan Kessy wa Simba pia yuko vizuri na msaada mkubwa kwa timu yake. Lakini Taifa Stars akicheza Kapombe, hakuna hata mtu mmoja anaweza kupinga au kulalamika.

Kapombe akicheza katika namba hiyo hakuna anayeweza kusema hapana kwa kuwa anaona ni sahihi. Anashambulia, anakaba na anachezesha, anapiga krosi safi na anafunga.

Kwa sasa ndiye beki mwenye mabao mengi zaidi kuliko wote nchini. Katika Ligi Kuu Bara amefunga mabao nane, sawa na mshambuliaji tegemeo wa Azam FC, John Bocco.

Si mchezo, maana Bocco ni kati ya washambuliaji wakali nchini. Kapombe sasa yuko naye sawa katika upachikaji wa mabao, haliwezi kuwa jambo dogo au rahisi.

Kama hiyo haitoshi ana bao moja tena katika Michuano ya Kombe la Shirikisho. Jumla ana mabao tisa msimu huu akiwa na Azam FC katika mechi za mashindano, huyu si mtu wa kumbeza na badala yake linapofikia suala la utaifa, basi tumuunge mkono.

Kapombe ni aina ya watu wenye tabia ya juhudi, mwenye tabia ya kuweka msukumo wa kutaka kufikia malengo na mfano mzuri namna anavyopambana uwanjani.

Kwa watu kama yeye mafanikio wala si jambo gumu sana. Lakini anachotakiwa kuwa makini nacho kuharibiwa na mafanikio kama yakipatikana haraka zaidi kuliko yeye alivyotarajia.

Najua soka litakuwa limebadili maisha ya Kapombe ambaye alianza kuonyesha juhudi kubwa akiwa Simba. Lakini bado halijampa mafanikio sahihi anayoyataka ili kutimiza ndoto zake. Ndiyo maana nikapanga kumuambia navutiwa na kazi yake, ninaamini ana uwezo wa kujitahidi zaidi na kufika mbali zaidi ya Azam FC na Tanzania.


Vijana wengine, pia wanaweza kupitia kujifunza kwake. Kwani si lazima kujifunza kupitia wageni pekee. Kila la kheri.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic