January 21, 2017






Uongozi wa Majimaji FC ya Songea, ulitenga Sh milioni 40 za motisha kuwapa wachezaji wao endapo wangeifunga Yanga, bahati mbaya wakafungwa bao 1-0, sasa fedha hizo zimetengewa kuwapa wachezaji wao kama wakifanikiwa kuifunga Simba Februari 4, mwaka huu.

Majimaji inayoshika nafasi ya 15 katika msimamo wa timu 16 katika Ligi Kuu Bara, ipo katika hatari ya kushuka daraja na itacheza na Simba Februari 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Katika mchezo wa ligi kuu Jumanne ya wiki hii kwenye Uwanja wa Majimaji, Yanga iliifunga Majimaji bao 1-0 lililofungwa na Deus Kaseke.

Mkurugenzi wa klabu hiyo, Mahmoud Milandu ambaye ni maarufu kama Mudy Sebene, alisema: “Ni kweli tulikuwa tumewaahidi wachezaji wetu fedha hizo, na kwamba haikuwa ahadi ya kusubiria watoke uwanjani bali fedha hizo zilizokuwa mkononi muda wote wa mchezo na wangezichukua kama wangeshinda.

“Tunajua wachezaji wetu walipambana japo bahati ya ushindi haikuwa kwetu, kwa kuwa ilikuwa makubaliano hadi washinde ndiyo wagawane, hivyo wamezikosa baada ya kupoteza mchezo.

“Kwa kuonyesha tumejipanga kusaka ushindi, fedha hizi tunazipeleka kwenye mchezo dhidi ya Simba na kama wakishinda tutawapa fedha zote hizi wala hakuna tatizo, tunatumia njia hii kuwapa morali wachezaji.

“Tunataka wapambane ili washinde kwani timu haipo kwenye nafasi nzuri, nia yetu hasa ni kuhakikisha hatushuki daraja,” alisema Sebene.

SOURCE: CHAMPIONI



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic