January 21, 2017Beki wa kushoto wa Mtibwa Sugar, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ amemchambua winga wa Simba, Shiza Kichuya kwa kusema ni mchezaji wa kawaida na ni rahisi kumzuia tofauti na wengi wanavyofikiria.

Kauli hiyo ya Baba Ubaya imekuja baada ya Jumatano wiki hii, Mtibwa Sugar kutoka suluhu na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Baba Ubaya amesema kwa beki yeyote anayetumia akili nyingi uwanjani hawezi kusumbuliwa na Kichuya kwa sababu atakuwa akitumia akili kumdhibiti na ndiyo maana katika mchezo huo alifanikiwa kumzua asisababishe madhara langoni kwao.

“Kichuya ni mchezaji mzuri lakini siyo sana kama wengi wanavyosema au wanavyodhani kuwa hakabiki, kwangu mimi namuona kuwa ni mchezaji anayekabika kirahisi sana kama mtu anayemkaba atakuwa anatumia akili na siyo nguvu kila wakati.

“Amekuwa akitumia sana mguu wa kushoto tofauti na ule wa kulia, hivyo ukifanikiwa kumdhibiti asipate nafasi ya kuutumia ipasavyo mguu wake wa kushoto basi unakuwa umemmaliza.


“Ndiyo maana amekuwa akipata shida sana kupita upande wangu kila ninapokutana naye uwanjani (naye anatumia mguu wa kushoto) hata wakati akiwa Mtibwa kabla ya kujiunga na Simba ilikuwa hivyohivyo,” alisema Baba Ubaya.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV