January 21, 2017



Na Saleh Ally
MCHEZO wa soka nchini umekuwa ukitoa ajira kubwa licha ya kwamba kuna wengi sana ambao wamekuwa wakijaribu kutaka kupingana nao au kushindwa kuuonyesha heshima kwa maana ya kutaka kufanya kila inavyowezekana ufanikiwe zaidi.


Siwezi kuzungumzia ajira ya wanachama wa klabu za Yanga na Simba wenye tabia za kubabaisha mambo ambao tumewapa jina la makomandoo. Hawa wana ajira zao ambazo wanazipata huku wakitaka kuonyesha kwamba wanazipenda sana klabu hizo huku wakijua ni sehemu ya kuendesha maisha yao.


Ajira ya mishahara, utakubaliana nami kwamba hata Ulaya. Wachezaji wengi wasio na elimu ya juu, wanaweza kuwa matajiri wakubwa kutokana na kipato cha juu wanacholipwa.


Hata nyumbani, kuna wachezaji wenye mishahara mikubwa kuliko mameneja wa matawi ya benki mbalimbali. Wana mishahara ya juu kuliko madaktari na kadhalika na hii yote ni kutokana na mchezo wa soka.


Wakati tunaona mchezo wa soka unatoa ajira, basi mimi bila ya woga niwe wazi kuwa ningependa kuona ajira zinakwenda kwa wazawa au kwa Watanzania kuliko wageni.
Nasema hivyo kwa kuwa kila nchi duniani utaona namna inavyohakikisha wananchi wake wanafaidika na kila kinachopatikana ndani ya nchi yao.


Najua siwezi kuzuia kwa wageni kupata ajira. Kama watakuwa bora katika utoaji wa huduma katika jambo fulani basi nao wanastahili kupata hizo fedha ingawa bado siwezi kuona wanaweza kuwa na upendeleo namba moja.
Sheria za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zinaruhusu kila timu kuajiri wachezaji saba kutoka nje ya Tanzania. Au timu inaweza kuajiri makocha kutoka nje ya Tanzania na hapa tunakubaliana kwamba mchezo wa soka nchini unatoa ajira.


Wakati hilo linatokea, basi wageni ambao wanapata nafasi ya kucheza hapa nyumbani wanapaswa kuheshimu ajira wanayopewa kutoka hapa nyumbani kama wanashindwa kuonyesha hilo basi inastahili suala hilo la ajira libaki na kuwa faida kwa Watanzania.


Hivi karibuni, kumekuwa na taarifa kwamba wachezaji wawili wa Yanga ambao wanasema ni majeruhi, Donald Ngoma na Obrey Chirwa, ‘wamejivunja’.


Msemo ‘wamejivunja’, unatumiwa na wapenda soka kwa maana ya wamedanganya kuwa wameumia. Tayari Ngoma raia wa Zimbabwe ameshalitolea ufafanuzi hilo kwamba yeye ni mgonjwa kweli. Baada ya hapo aliondoka, imeelezwa kwamba ana msiba kwao Zimbabwe.



Mwenzake Chirwa, amekuwa kimya na hajawahi kuamua kueleza jambo hilo. Kama ni jambo zuri, basi si vibaya kuamini kuwa ni wagonjwa. Lakini taarifa kutoka ndani ya Yanga zimekuwa zikieleza mambo mengi sana.


Taarifa hizo zinaeleza kuwa wachezaji hao wana jambo, huenda hawafurahishwi na kitu kutoka kwa Kocha mpya, George Lwandamina. Hivyo wamekuwa wakijiondoa katika ushiriki ili kupunguza kasi ya Yanga. Huenda wanataka kupunguza kasi kwa kukaa kando.


Inawezekana hakuna ukweli lakini vizuri pia kukumbuka, “Lisemwalo lipo, kama halipo basi laja.” Jiulize mara ngapi Ngoma au Chirwa waliumia na haukusikia taarifa kama ambazo zimekuwa zikizagaa sasa.


Maana yake kuna jambo halijakaa sawa au kuna mtu anajua jambo. Kuna kitu ambacho kimefichika katika hili na kama kitakuwa kweli, basi kitakuwa kibaya zaidi.

Yanga haipaswi kuwa klabu ya kufanyiwa mchezo hivi. Chirwa aliyesajiliwa kwa zaidi ya Sh milioni 200, amefunga mabao matano tu.

Unamuona wakati wa michuano ya Mapinduzi wakati Yanga ikisumbuka, yuko jukwaani. Ngoma pia alifanya vizuri msimu uliopita, akafunga mabao 17 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Hamisi Kiiza aliyekuwa na 19 na mfungaji bora Amissi Tambwe aliyekuwa na 21.

Sasa anategemewa, lakini Yanga inapambana Mapinduzi yuko jukwaani. Yanga inapambana katika ligi yuko jukwaani. Anaumwa, lakini kuna hofu ya kutokuwa na ukweli!

Narejea, naweza kuwaamini Ngoma na Chirwa lakini bado nitabaki na hofu kutokana na kinachozungumzwa kwa kuwa mambo ya soka, yanajulikana na yanavyokwenda mimi si mgeni.

Kama ni kweli wao ni wagonjwa, niwaombee wapone haraka. Lakini kama linalozungumzwa ni kweli, basi litakuwa ni jambo baya linaloweza kufananishwa na wizi wa hali ya juu ambao haupaswi kuendekezwa.

Nataka niwe wazi, Yanga inatokea Tanzania. Mimi ni Mtanzania na bila ya woga hata kidogo niwaeleze wachezaji wanaotokea nje ya nchi yetu waache mchezo au mbwembwe. Pia waonyeshe thamani yao na kilichowaleta, la sivyo wanaweza kufunga safari na kurejea kwao.


Najua mashabiki wa soka ni watu wa kusahau. Mfano mauzi ya kila namna yanaweza kutokea lakini mchezaji akiifunga Simba, watamsamehe milele, Lakini kiuongozi haliwezi kuwa jambo sahihi.


Pia anayelipwa na klabu, aliyetengeneza ajira kutoka nje ya Tanzania anapaswa kutoa heshima kwa aliyempa ajira. Anapaswa kumpa mafanikio anayempa hiyo ajira badala ya kuendekeza hisia binafsi kutoka katika mawazo ya kutaka kutekeleza la moyoni kwa faida yake.


Naweka msisitizo, napinga wachezaji wote wanaopata ajira Tanzania na kutaka kuleta mchezomchezo. Nakataa kuona nchi yetu inageuzwa shamba la bibi huku watu wakiangalia matakwa yao binafsi au furaha za mioyo yao.

Mwisho niwakumbushe wachezaji wazawa, kwamba nyie ndiyo chanzo cha Tanzania kugeuzwa shamba la bibi. Hamtaki kujituma zaidi, hamna malengo ya kuwa tegemeo ili kuzuia wachezaji wa kawaida kabisa kulipwa mamilioni ambayo yangekuwa faida kwenu.


Viongozi wengi wa soka, pia hamtoi thamani kwa wachezaji wa nyumbani. Wengine mnafanya hivyo kwa kuwa wakati wa kusajiliwa kwa wageni mnafaidika kwa kuingiza dola mfukoni. Nyie pia ni chanzo cha matatizo mengi kwa kuwa mnaendekeza njaa bila ya kujua huwa haimalizwi na fedha zilizojaa ubinafsi. Kumbukeni, nchi yetu tunaweza kuibadilisha sisi na kila mgeni anayetaka kuajiriwa hapa akajipima.

SOURCE: CHAMPIONI


2 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic