January 14, 2017
Na Saleh Ally
MACHI mwaka huu, harakati za kuwania kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2019, itakayofanyika nchini Cameroon, zitaanza.

Wakati tunasubiri kuanza kwa harakati hizo, leo waliofanya vizuri katika harakati zilizopita, watakuwa wanaanza kupambana katika michuano ya Afcon inayoanza nchini Gabon, timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki michuano hiyo kwa mara ya mwisho mwaka 1980, haipo tena kwa mara nyingine.

Stars ina matumaini ya kushiriki michuano hiyo Cameroon na imepangwa Kundi L lenye timu za Lesotho, Cape Verde na Uganda. Ajabu, wako wanaosema ni kundi laini.

Ulaini wa kundi, unazibwa na vigezo vyote sahihi. Kwamba angalau Lesotho wanaweza kufanana nasi, lakini Uganda wako Afcon, Cape Verde walishiriki michuano iliyopita.

Hata kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) katika kundi hilo, sisi Tanzania ndiyo hovyo zaidi. Maana tuko katika nafasi ya 156, Lesotho wako namba 142, Cape Verde ni 79 na Uganda ndiyo vinara namba 73.

Kundi la Stars:
Imepangwa Kundi L, kundi ambalo Watanzania wengi wameanza mjadala kuonyesha Stars imepangwa kundi rahisi na kuna uhakika wa kufuzu.

Wako ambao wametoa hoja kwamba Stars ni kundi laini kwa kuwa ukiachana na Kundi L, hakuna kundi jingine ambalo Stars ingepangwa kuanzia A hadi K, halafu nafuu yake ingefanana na ile ya kundi L.

Kila mmoja anaweza kusema lake lakini ukweli unabaki palepale kwamba kikosi cha timu ya taifa ni dhaifu na lazima kuwe na juhudi za makusudi na umakini wa hali ya juu maradufu kubadilisha hisia zote za kujiona sisi ni akina nani.

Hakuna anayeweza kusema kundi hilo ni jepesi, maana Lesotho ambao walikuwa dhaifu dhidi yetu, wakati wa Mart Nooij walitunyanyasa, tukaonekana hatuna letu kwa nchi hiyo ndogo.

Ukirudi kwa Uganda, tunajuana na kila mmoja anakumbuka rekodi zetu na wao. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne, ushindi wetu kwao ni sare.

Lakini ndani ya miaka miwili iliyopita, inaonekana wao si wenzetu kabisa. Michuano iliyopita ya Afcon, ilibaki pointi mmoja tu wafuzu, wakateleza. Michuano iliyofuatia ambayo ni ya Gabon inayoanza leo, wamefuzu. Sisi hauwezi kuzungumzia chochote kinachofanana na wao.

Leo wanashiriki watajua utamu wake, kikosi chao kitaimarika, wana wachezaji wengi zaidi nje ya nchi yao, uhakika unaonyesha watakuwa bora zaidi yetu zaidi wakati wa kuwania kwenda Cameroon.

Cape Verde nafikiri mnawakumbuka, mbele yetu walisonga mbele wakati huo Taifa Stars ikiwa chini ya Kocha Marcio Maximo. Nakumbuka nilisafiri hadi mji wa Praia, muda wa saa 11 kutoka Dar es Salaam kwenda kwenye mechi dhidi ya Stars, tukakutana na kipigo cha bao 1-0.

Sisi ndiyo dhaifu kuliko mwingine yeyote na uchambuzi wa wengi Afrika wanaona wenye kazi ngumu ya nafasi hiyo ni Uganda na Cape Verde ambao wana wachezaji karibu wote wa timu ya taifa wanaocheza Ulaya.

Sisi ni dhaifu ndiyo maana tunatafuta nafuu kwa nguvu zote, lakini hata kwenye nafuu bado Stars ni dhaifu na haina nafasi.

Unaweza kujiuliza kwa haki. Kwamba kupitia Kocha Salum Mayanga, itakuwa ni sahihi kwetu kuhakikisha tunaivuka safari hii?

Kama kawaida, TFF wako ‘busy’ na kampeni za uchaguzi na tumeona namna suala la kura linavyopewa kipaumbeke kuliko jambo jingine. Kuna baadhi ya mikoa mfano Iringa, ubabe umetawala, kila timu inayocheza huko inalazimishwa kufungwa na wachezaji wanapigwa hadi wanakimbizwa hospitali.

TFF haisemi lolote kukemea hilo na taarifa zinaeleza kwamba ili watoe kura, Iringa wameahidiwa timu ya ligi kuu, hivyo kinachofanyika wakubwa wanajua.

Unazikumbuka ahadi za Rais Jamal Malinzi wakati huo akipambana kuingia TFF na aliposhinda kila mmoja alisifia kwamba atafanya vizuri na ilionekana kama alibaniwa sana.

Waliokuwa wakimsifia na kulalamika anabaniwa, siku hizi hawazungumzi lolote kwa kuwa ukweli umechukua mkondo wake. Hakuna nafuu wala cha kujivunia.

Unaona, hata Ligi za Vijana na ile ya Wanawake, zimeanzishwa wakati wa kipindi cha kampeni. Hazikuanzishwa miaka yote miwili na nusu na hakuna ambacho TFF inaweza kusema ilikifanya.

Angalau, wakati wa Leodeger Tenga, Stars ilicheza michuano ya timu za taifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) iliyofanyika Ivory Coast mwaka 2009. Leo Stars haiko Chan, haiko Afcon, haina mpango na Kombe la Dunia.

Unaweza kujiuliza, viongozi walio TFF wanataka nini na mpira wa Tanzania. Kama wameshindwa kila kitu na ahadi zao ni maneno tupu, vipi na inaendelea kubaki hapahapa.


Tuache kuurahisisha ukweli, sasa Tanzania imeingia kwenye kundi la vibonde na TFF haiwezi kulikwepa hili. Ukweli pekee ndiyo unaweza kutuondoa hapa, kama tunaendelea kuamini Kundi L ni laini na TFF ina mipango mizuri, tuombe uzima tufike salama mwishoni mwaka 2018, tutakumbushana.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV