January 23, 2017Na Saleh Ally
WAKATI fulani suala la klabu za soka nchini kuendeshwa kienyeji lilichukua nafasi kubwa sana na ilionekana klabu inaweza kuendeshwa kama duka la “Mangi”.

Yanga na Simba ni kubwa, kwa sasa unaona Azam FC nayo inaanza kupiga hatua katika makuzi, nayo inakua ingawa wahusika wengi hasa viongozi wao nao wangependa kuona wana ukubwa kama Yanga au Simba kwa maana ya idadi ya mashabiki, jambo ambalo ni kujidanganya.


Ukubwa wa Simba na Yanga, una nafasi wa kuzifanya klabu hizo kuwa tajiri wa kutupwa kutokana na kuingiza fedha nyingi.


Kuingiza fedha nyingi hakuwezekani kukatokea mtu akiwa amekaa chini na kusubiri bahati nasibu. Badala yake suala la ubunifu na mipango madhubuti inatakiwa ili kuanzisha mikakati chanya inayoweza kusaidia upatikanaji wa fedha hizo zitakazokuwa zinaingia.


Kama unakumbuka, baadaye wadau tulilia sana tukitaka klabu zijiendeshe kisasa ikiwa ni pamoja na kuongeza maofisa watakaokuwa wakishughulikia masuala ya masoko.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya hivyo, Yanga pia na kama sikosei na Simba walifuatia ingawa baadaye ilionekana vitengo hivyo vilikuwa vikisuasua.


Huenda vitengo hivyo havikufanya vizuri sana kutokana na mazoea. Kwamba viongozi walikuwa wakifanya bila ya vitengo hivyo,  hivyo kunaweza kukawa na mambo mengi yanatakiwa kufanyika na wakaona hayana maana.


Lakini inawezekana waliopewa vitengo hivyo nao wameingia na kulala. Wakaona mambo yanaweza kwenda kawaida bila ya wao kuwa na presha na kweli wamekwenda kwa kipindi kirefu mambo yakiwa hivyo.


Kipindi hiki kinaweza kuwa kibaya kwao kwa kuwa uchumi umeporomoka kwa kiwango kikubwa hata kama kutakuwa na wale wanaosema si hivyo.


Inawezekana kikawa ni kipindi cha mpito lakini lazima waajiri wao, Simba, Yanga, TFF au klabu nyingine ambayo ina watu wanaohusika na masoko watakuwa wamebanwa na ugumu wa mambo.

Januari imekuwa ngumu, lakini imekuwa ngumu zaidi kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, imefanya mabadiliko kadhaa na kuondoa vitu vingi vilivyokuwa vya mazoea. Wakati wowote wa mabadiliko lazima kunakuwa na ugumu.


 Kutokana na hali hiyo katika kipindi hiki, matumizi yanaweza yakaanza kuzidi kile wanachoingiza kwa kiasi kikubwa. Baada ya hapo waajiri wataanza kuwaza jambo moja tu, kupunguza matumizi kwanza.

Kama watawaza hivyo, kutakuwa na hatari kubwa kwa maofisa masoko ambao kama watakuwa hakuna walichowahi kukifanya kikawa faida na kuisaidia klabu kupunguza makali, haina shaka, watakuwa katika hatari ya mstari mwekundu.

Wataingia katika mstari mwekundu wa kupoteza ajira zao kwa kuwa mwajiri lazima ahakikishe Yanga inaendelea kusonga mbele na si kufa.
Fedha uwanjani zitaendelea kupungua na mashabiki wengi wataendelea kuchagua kuangalia mpira kwenye runinga kuliko kuangalia uwanjani.

Hii itazidi kuleta athari mara tatu au nne kwa upande wa klabu katika suala la mapato. Pamoja na yote, maofisa masoko, wataangaliwa kwa macho yote kama wana lolote, mfano kuleta wadhamini ambao wanaweza kuzikomboa klabu zao kutokana na hali ngumu zilizofikia.

Kama watashindwa kufanya lolote na hasa ukizingatia makampuni mengi yamebanwa. Maana yake maofisa masoko au wafanyakazi wengine ambao wanakuwa sehemu ya klabu, watatumika kama sehemu ya kupunguza matumizi ili kuzifanya klabu ziendelee kuishi hata kama hali ni ngumu. Maana yake iko hivi, wakati huu ndiyo wanaohusika na kuzitafutia klabu masoko, kuzitafutia wadhamini, kubuni namna ya kuingiza fedha za ziada wanatakiwa kufanya kazi yao kwa ufasaha wa juu na kuwa msaada kwa kuwa ndiyo kipindi cha kuonyesha umuhimu wao. Wakishindwa hivyo, ninaamini, ajira zao zitakuwa mashakani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV